BoT yawanoa watoa huduma ndogo za fedha kuhusu uzingatiaji wa sheria na weledi

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo ya Ithibati ya Uweledi kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha nchini (Certified Microfinance Professional-CMP), kwa lengo la kuwaongezea ujuzi na uelewa kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia shughuli za sekta hiyo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania, Dodoma, kuanzia tarehe 14 hadi 25 Septemba 2026, yaliandaliwa na Chuo cha Benki Kuu na yalihitimishwa kwa washiriki kutunukiwa vyeti.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo, Meneja Msaidizi wa Rasilimali Watu wa Tawi la Dodoma, Bw. Airenus Mlowe, aliwataka wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata katika mafunzo hayo kuimarisha uadilifu, uwazi na haki, pamoja na kuzingatia misingi ya kibinadamu katika kuwahudumia wananchi.
Aidha, aliwahimiza wahitimu kushirikisha ujuzi walioupata na wadau wengine katika sekta hiyo ili kusaidia kuleta maboresho katika utoaji wa huduma ndogo za fedha nchini.

“Ninyi ni jeshi, nendeni mkalete mabadiliko ya kweli katika sekta hii,” alisema Bw. Mlowe.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Bi. Mary Ngassa, aliwakumbusha wahitimu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na matakwa ya mamlaka zinazohusika katika usimamizi wa sekta ya fedha wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
Bi. Ngassa alisema,uzingatiaji wa matakwa ya kisheria na kiudhibiti ni muhimu katika kujenga sekta ya huduma ndogo za fedha yenye uwajibikaji, uaminifu na ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha, sambamba na kuhakikisha usalama wa huduma zinazotolewa.

Alieleza kuwa, sekta imara na yenye kuzingatia misingi ya udhibiti ina mchango mkubwa katika kukuza ustawi wa wananchi na kuunga mkono juhudi za Taifa za kupunguza umaskini kupitia upatikanaji wa huduma salama na zinazowajibika za kifedha.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Benki Kuu ya Tanzania na wadau wake katika kuimarisha uwezo wa wataalamu katika sekta ya huduma ndogo za fedha, hususan katika uelewa na utekelezaji wa matakwa ya kisheria na kiudhibiti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here