NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi katika misako na operesheni zilizofanyika kwa kipindi cha miezi miwili limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 441 kwa makosa mbalimbali ikiwemo makosa ya wizi wa pikipiki, unyang'anyi wa kutumia silaha, uvunjaji, udhalilishaji, dawa za kulevya na pombe za kienyeji (gongo).
Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Madema, Wilaya ya Mjini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Elthon P. Banzi, amesema katika operesheni hiyo walifanikiwa kukamata pikipiki 29 na bajaji ambazo ziliibiwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na nje ya Mkoa. Hivyo amewataka wananchi kufika kituoni hapo ili kutambua pikipiki hizo.
Katika hatua nyingine, kupitia operesheni hizo zilifanikisha kuwakamata watuhumiwa watatu kwa kosa la kujifanya wafanyakazi wa serikali jambo ambalo ni kosa kisheria.
Watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa upekuzi walipatikana na sare zinazofanana na Jeshi la Polisi Tanzania, Sare za Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, bunduki bandia yenye muundo wa Ak 47, bastola ya bandia, pingu, filimbi na vifaa vingine vinavyotumiwa na maafisa wa majeshi mbalimbali nchini.
Kamanda Banzi amewataja watuhumiwa hao ni Nassir Ahmed Salum, miaka 25, Mshirazi wa Fuoni Migombani na Haji Issa Faki, miaka 39, Mshirazi wa Kianga Domoni wilaya ya Mjini, na Zahran Masoud Zahran, miaka 24, Mshirazi wa Fuoni Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.
Watuhumiwa wengine walikamatwa mnamo tarehe 26/08/2026 majira ya saa 2.00 usiku huko maeneo ya njia ya Miwani shehia ya Kizimbani wilaya magharibi A na Mkoa Mjini Magharibi, watuhumiwa watatu ambao ni (1) Saleh Jangiani Ibrahim maarufu Madenge, miaka 25, mshirazi wa Sharifumsa.
(2) Khamisi Haji Khamisi maarufu Kanji, miaka 38, mshirazi wa Mtoni na (3) Khamisi Majala Suleiman, miaka 27, mshirazi wa Magogoni wote kwa pamoja walimjeruhi na vitu vyenye ncha kali sehemu ya shingoni mtu aliyefahamika kwa jina la Hassani Khamisi Rashid, miaka 25, mshirazi wa Betras kisha kumnyang’aya pikipiki yake aina ya Tvs yenye namba za usajili M 980 ABN.









