DCEA yakamata tani 18.08 za dawa za kulevya katika mikoa 14 nchini

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 18,078.41 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika katika mikoa 14 nchini katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2026.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Septemba 29,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dara wa Salaam.

Amesema, operesheni hizo zilifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.

"Kati ya kiasi hicho, kilogramu 11,504.76 zilikuwa bangi, kilogramu 6,529.5 mirungi, kilogramu 44.45 bangi aina ya skanka na gramu 41.25 heroin."

Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, katika operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 289 walikamatwa, ambapo 169 wamefikishwa mahakamani huku taratibu za kisheria zikiendelea dhidi ya watuhumiwa wengine.

Aidha, operesheni hizo zimewezesha kukamatwa kwa magari nane, bajaji moja na pikipiki 40 ambazo zilitumika katika shughuli zinazohusiana na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Amesema, kufuatia operesheni hizo, bangi imeendelea kuongoza kwa kiwango cha uzalishaji na ukamataji, hususan katika mikoa ya Morogoro na Tabora.

Mkoani Morogoro, jumla ya kilogramu 6,299.24 za bangi pamoja na kilogramu 226 za mbegu za bangi zilikamatwa, huku mkoani Tabora kilogramu 4,650.86 za bangi pamoja na kilogramu 203 za mbegu za bangi zilikamatwa.

Kwa upande wa mirungi, operesheni zimebaini matumizi ya pikipiki na mabasi ya abiria katika usafirishaji wa dawa hiyo, hususan katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma, ambapo jumla ya kilogramu 6,412.89 za mirungi zilikamatwa.

Katika moja ya matukio hayo, amesema watuhumiwa watatu walikamatwa wakisafirisha bunda 238 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 125.33 kwa kutumia basi la kampuni ya RATCO, lenye namba za usajili T.443 EMG, lililokuwa likifanya safari kati ya Tanga na Dar es Salaam

Aidha, mkoani Tabora, Wilaya ya Uyui, kilogramu 21.95 za bangi zilikamatwa katika gari aina ya TATA lenye namba za usajili T.381 DWU, lililokuwa likifanya safari kati ya Uyui mkoani Tabora na Kahama. Watuhumiwa watano walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Kutokana na hali hiyo,mamlaka inawataka wamiliki na waendeshaji wa mabasi na magari ya abiria kuimarisha udhibiti wa mizigo, ukaguzi wa vyombo vya usafiri pamoja na usimamizi wa wafanyakazi, ili kuzuia vyombo vyao kutumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya.

Katika eneo la ukaguzi wa abiria katika Bandari ya Dar es Salaam, Mamlaka ilibaini matukio ya usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia abiria.

Mbali na watanzania waliokamatwa, Mamlaka iliwakamata raia wa Uturuki akiwa na gramu 1.87 za bangi aina ya skanka, raia wa Kenya akiwa na gramu 3.89 za mirungi na raia wa Nigeria akiwa na gramu 4.6 za bangi.

Aidha, katika operesheni zilizofanyika mkoani Arusha, raia wawili wa Afrika Kusini walikamatwa wakiwa na jumla ya gramu 65.8 za bangi aina ya skanka.

Aidha, katika operesheni hizo, pikipiki 40, bajaji moja (1) na magari nane (8) yaliyohusishwa na tuhuma za usafirishaji wa dawa za kulevya yalikamatwa. Magari hayo ni pamoja na Toyota Harrier yenye namba T.878 ASJ, Toyota Land Cruiser yenye namba T.234 BUR, Toyota IST yenye namba T.215 DCJ, Toyota Noah yenye namba T.231 AWP, Toyota Alphard yenye namba T.870 EDE na Toyota Discovery.

"Ukamataji wa vyombo hivyo, unaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha udhibiti wa mizigo, ukaguzi wa vyombo vya usafirishaji na usimamizi wa wafanyakazi, pamoja na kuongeza uwajibikaji wa wamiliki na waendeshaji wa vyombo hivyo ili kuzuia kutumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya."

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, katika eneo la udhibiti wa kemikali, kupitia uchambuzi wa mfumo wa kielektroniki, Mamlaka ilizuia kuingia nchini kwa shehena ya sulphuric acid yenye uzito wa kilogramu milioni 64 baada ya kubaini kuwa taarifa zilizowasilishwa kuhusu uingizaji wa kemikali hiyo hazikuwa sahihi na matumizi yake halali hayakuwa yamebainishwa.

Aidha, pikipiki zimeendelea kutumika katika usafirishaji wa mirungi, hasa katika ukanda wa kaskazini unaojumuisha Tanga, Kilimanjaro na Arusha, huku mabasi na magari ya abiria yakibainika katika baadhi ya matukio ya usafirishaji wa dawa za kulevya.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mamlaka imebaini kuwepo kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu walio nje ya Mamlaka, wanaodaiwa kutumia mwanya udhibiti wa biashara ya dawa za kulevya kujihusisha na vitendo vya rushwa na uhalifu.

"Baadhi ya watu hao wamekuwa wakiwalenga wahalifu wa biashara ya dawa za kulevya, kuwakamata na kuwanyang'anya dawa hizo, kisha kuwashinikiza kutoa rushwa."

Aidha, katika baadhi ya matukio, wamekuwa wakiwatishia kuwafikisha katika Mamlaka endapo watakataa kutekeleza matakwa yao.

"Mamlaka inatoa onyo dhidi ya vitendo hivyo na kuwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na dawa za kulevya kwa namna yoyote ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here