NA DIRAMAKINI
WAKALA wa Vipimo nchini (WMA) umeeleza safari ndefu ya kihistoria ya usimamizi wa vipimo nchini Tanzania, ikifichua jinsi taasisi hiyo ilivyotoka katika mfumo wa usimamizi wa kisheria na kipolisi kabla ya Uhuru hadi kuwa wakala wa kisasa unaolinda haki za walaji na wafanyabiashara kitaifa na kimataifa.
Hayo yamebainika leo Septemba 23,2026 wakati Afisa Vipimo Mwandamizi wa WMA, Bw.Malaki Nyangasi akifanya mahojiano katika kipindi cha BIG CITY BREAKFAST kupitia MJINI FM RADIO.
Afisa Vipimo Mwandamizi huyo kutoka Kitengo cha Bidhaa Zilizofungashwa cha Wakala wa Vipimo ameeleza kuwa, mfumo wa vipimo nchini una historia ndefu iliyoanzia kabla ya nchi kupata uhuru wake.
Bw.Nyangasi amebainisha kuwa, kabla ya Uhuru, taasisi ya usimamizi wa vipimo ilikuwa ikiendeshwa moja kwa moja chini ya Jeshi la Polisi. Lengo kuu wakati huo lilikuwa kuzuia ubadhirifu na utapeli wa kibiashara kupitia mkono wa sheria na ulinzi.
Aidha,baada ya nchi kupata Uhuru, usimamizi huo ulihamishiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo ulifanya kazi kama kitengo cha kawaida cha serikali.
Ilipofika mwishoni mwa miaka ya 1960, kitengo hicho kilirasimishwa na kuwa Idara au Kurugenzi rasmi ya Serikali iliyoongozwa na Sheria ya Vipimo Namba 30 ya miaka hiyo.
Hata hivyo, ili kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika sekta ya biashara na viwanda, Serikali mnamo Mei mwaka 2002 ilirasimisha na kuunda rasmi Wakala wa Vipimo (WMA) chini ya Sheria ya Mawakala wa Serikali Namba 340.
Katika mahojiano hayo, Bw. Nyangasi ameeleza jinsi mfumo wa vipimo ulivyopitia hatua tofauti za mabadiliko ya kitaifa na kimataifa.
Amesema, wakati wa utawala wa Kijerumani, mifumo ya mwanzo ya kimetric ilianza kuingizwa nchini kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali na biashara.
Pia,Waingereza walipoingia, walileta mfumo wa Imperial ambao ulitumia vipimo vya ratili (pounds), yadi (yards) na futi (feet).
Mfumo huo uliendelea kwa miaka mingi na kuleta changamoto za ulinganifu wa kibiashara kimataifa.
Hata hivyo, baadaye, mataifa ya duniani yalifikia makubaliano ya pamoja ya kutumia mfumo mmoja unaosomana na unaokubalika kimataifa unaojulikana kama Systeme International d'Unites (SI\ Units).
Kupitia mfumo huu, kipimo cha kilo moja au mita moja nchini Tanzania kikawa na thamani na uzito sawa na kilo au mita hiyo nchini Uingereza, Ujerumani au Marekani.
Bw. Nyangasi ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miongo mitatu katika sekta hiyo tangu alipojiunga mnamo miaka ya 1990 amesisitiza kuwa, jukumu kubwa la Wakala wa Vipimo hivi sasa ni kuhakikisha kuwa bidhaa zote zilizofungashwa na vipimo vyote vinavyotumika masokoni vinazingatia kanuni halisi ili kumlinda mwananchi dhidi ya kupunjwa na kumwezesha mfanyabiashara kupata haki yake stahiki.
Vilevile kupitia mabadiliko hayo, Tanzania inaendelea kuwa sehemu ya mfumo wa kibiashara wa kimataifa unaojiendesha kwa uaminifu, uwazi na usahihi wa viwango vya vipimo.
