NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kalenda ya minada ya dhamana za Serikali kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa Serikali wa kukopa kupitia hati fungani na dhamana nyingine za muda mfupi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu Septemba 15, 2026, minada hiyo itafanyika kwa dhamana za Serikali zenye muda wa siku 35, 91, 182 na 364, pamoja na hati fungani za Serikali zenye muda wa ukomo wa miaka miwili, mitano, 10, 15, 20 na 25.Taarifa hiyo imeeleza kuwa,kiwango cha riba kwa hati fungani, pamoja na taarifa nyingine muhimu kuhusu dhamana husika, kitaainishwa katika tangazo la kila mnada wakati mwaliko wa kuwasilisha zabuni utakapotolewa.
Kwa mujibu wa kalenda hiyo, minada ya dhamana za Serikali kwa robo hiyo itaanza Oktoba 7, 2026, na kuendelea hadi Desemba 16, 2026.
Katika kipindi hicho, mnada wa Oktoba 7 utahusisha dhamana za Serikali za muda mfupi, huku Oktoba 14 kukiwa na mnada wa hati fungani ya miaka 25. Oktoba 21 kutakuwa na mnada mwingine wa dhamana za muda mfupi, kabla ya mnada wa hati fungani ya miaka miwili kufanyika Oktoba 28.
Kwa upande wa Novemba, minada imepangwa kufanyika Novemba 4, 11, 18 na 25. Dhamana zitakazotolewa katika minada hiyo ni pamoja na hati fungani za miaka miwili, 10 na 15, sambamba na dhamana za Serikali za muda mfupi.
Minada ya mwezi Desemba imepangwa kufanyika Desemba 2, 10 na 16, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kalenda hiyo kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2026/27.
Benki Kuu imeeleza kuwa, ratiba hiyo inaweza kubadilishwa kutokana na mahitaji ya utoaji wa dhamana endapo mazingira ya soko yatahitaji, ikiwemo mahitaji ya kukopa na mwenendo wa hali ya soko.
Aidha, Benki Kuu imewataka wadau kuzingatia kwamba Serikali inaweza kufanya mabadiliko katika kalenda ya utoaji wa dhamana endapo kutakuwa na mahitaji yanayohusiana na ununuzi na mwenendo wa hali ya soko.