LATRA yatoa wito malipo ya usafiri yafanyike kielektroniki, yawataka wadau kuzingatia tahadhari ya mvua za El Nino

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewataka wadau wa sekta ya usafirishaji nchini kuzingatia matakwa ya sheria yanayohusu matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika malipo ya huduma za usafiri, huku ikiweka mkazo katika hatua za usalama wa abiria na vyombo vya usafiri wakati wa mvua kubwa.
Wito huo umetolewa leo Septemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Dkt. Habib Suluo wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya mamlaka hiyo na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH).

Dkt.Suluo amesema,Serikali imeweka utaratibu wa matumizi ya njia za kielektroniki katika miamala mbalimbali, akieleza kuwa amri hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa Kifungu cha 13(C) cha Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442.

Amesema, utaratibu huo ulianza kutumika rasmi Julai 1, 2026 ukiwa na lengo la kurahisisha mifumo ya malipo na kuimarisha uwazi katika miamala ya huduma mbalimbali za kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, LATRA imeendelea kutoa elimu kwa wasafirishaji na wananchi kuhusu wajibu wa kuzingatia matakwa ya amri hiyo, hususan katika maeneo yanayohusisha huduma za usafiri ardhini.

Miongoni mwa maeneo hayo ni malipo ya ada, tozo na ushuru unaohusiana na huduma za usafiri, pamoja na nauli za mabasi ya usafiri wa mijini,mabasi yaendayo haraka (BRT), vivuko na madaraja.

Aidha, mabasi yanayotoa huduma za masafa marefu kati ya mikoa yanatakiwa kutumia mifumo ya kielektroniki katika upokeaji wa nauli badala ya kutegemea fedha taslimu.

Dkt.Suluo amesema,utaratibu huo pia unahusu huduma za teksi mtandao, ambapo malipo yanafanyika kupitia mifumo ya kielektroniki pamoja na huduma za usafiri wa reli na malipo ya maegesho ya magari.

Katika sekta ya usafirishaji amesema, wamiliki na waendeshaji wa magari wanapaswa kutumia njia za kielektroniki wanapolipia mafuta katika vituo vya huduma za mafuta.

Utaratibu huo pia unahusisha baadhi ya huduma za hoteli, migahawa, huduma za utalii, pamoja na miamala inayohusu ununuzi na uuzaji wa magari, kwa mujibu wa matakwa yaliyowekwa katika amri hiyo.

LATRA YATOA TAHADHARI YA MVUA KUBWA

Wakati huo huo, LATRA imewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri, madereva na abiria kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa mvua kubwa, kwa kuzingatia taarifa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Dkt.Suluo amesema,usalama wa abiria na mali zao unapaswa kupewa kipaumbele, hasa katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko, maji yanayotiririka kwa kasi na uharibifu wa miundombinu.

Amewataka wamiliki na madereva kuhakikisha magari yao yako katika hali nzuri kabla ya kuanza safari, akitaja umuhimu wa kukagua matairi, mfumo wa breki, vioo, mfumo wa kufuta maji kwenye kioo (wipers) pamoja na taa za magari.

Vilevile, amesisitiza kuwa ukaguzi huo ni muhimu zaidi wakati wa mvua, kwa kuwa hali ya hewa inaweza kupunguza muonekano wa dereva na kuongeza changamoto katika uendeshaji wa magari.

Dkt.Suluo pia amewataka madereva kuepuka kujaribu kuvuka maeneo yenye maji yanayotiririka kwa kasi au madaraja yaliyofunikwa na maji.

Amesema, kabla ya kuvuka maeneo hayo, dereva anapaswa kuhakikisha kina cha maji na uimara wa daraja viko salama, akieleza kuwa katika baadhi ya mazingira maji yanaweza kuwa yamesababisha mmomonyoko wa udongo chini ya miundombinu bila kuonekana kwa urahisi.

Kwa upande wa usafiri wa reli, LATRA imezitaka kampuni na wasimamizi wa reli kufanya ukaguzi wa kina wa njia za treni, ikiwamo reli za zamani za meter gauge ili kuhakikisha kingo za reli na udongo unaozunguka njia hizo vina uimara unaohitajika.

Mkurugenzi Mkuu amesema, ukaguzi huo unapaswa kuzingatia hali ya njia kabla na baada ya mvua kubwa ili kupunguza uwezekano wa madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mmomonyoko wa udongo au kuharibika kwa miundombinu ya reli.

LATRA pia imewasihi wananchi kupanga safari zao kwa kuzingatia hali ya hewa na kuahirisha safari zisizo za lazima pale kunapokuwa na mvua kubwa au mazingira hatarishi.

Aidha, wazazi na walezi wanaosafiri na watoto wametakiwa kutumia programu ya LATRA App kufuatilia usalama na mwenendo wa magari wanayosafiria, hususan katika safari za kati ya miji.

Dkt.Suluo amesema, magari ya abiria yana mifumo ya ufuatiliaji inayowezesha kufuatwa kwa mwenendo wa safari, hivyo abiria wanaweza kutumia teknolojia hiyo katika kupata taarifa zinazohusiana na safari zao.

LATRA imeeleza pia kuwa mfumo wake wa huduma kwa wateja utaendelea kupatikana saa 24 kwa ajili ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi, kutoa msaada na kufuatilia masuala ya usalama wa usafiri nchini.
Akizungumzia mwenendo wa sekta ya usafirishaji, Dkt. Suluo amesema,idadi ya leseni za magari yaliyosajiliwa na kutolewa na LATRA imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitano.

Amesema,leseni hizo zimeongezeka kutoka 239,953 mwaka wa fedha 2021/22 hadi 590,498 mwaka 2025/26.

Dkt.Saluo amefafanua kuwa, magari hayo yanajumuisha makundi mbalimbali ya magari binafsi na ya biashara yakiwemo magari ya abiria,magari ya mizigo na magari ya kukodi.

Kwa upande wa magari ya kukodi, Dkt.Suluo amesema, zaidi ya asilimia 70 ya vyombo vilivyosajiliwa ni pikipiki na magari ya miguu mitatu maarufu kama bajaji.

Dkt.Suluo amesema, ongezeko hilo linaonesha kuendelea kupanuka kwa shughuli za usafirishaji ardhini na umuhimu wa kuimarisha mifumo ya udhibiti na usalama sambamba na ukuaji wa sekta hiyo.

USAFIRI WAENDELEA KUPEWA UZITO KATIKA DIRA 2050

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina,Bw.Sabato Kosuri amesema,uhusiano kati ya ofisi hiyo, taasisi inazosimamia na wahariri wa vyombo vya habari nchini umeendelea kuimarika.

Bw.Kosuri amesema, sekta ya usafirishaji ina nafasi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kutokana na mchango wake katika kuwaunganisha wananchi, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Amesema,ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu huduma, mabadiliko ya mifumo na fursa zinazopatikana katika sekta ya usafirishaji.

Wakati huo huo, LATRA imeeleza kuwa, itaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia na uwekezaji katika usafiri unaozingatia mazingira ikiwemo magari ya umeme, usafiri wa waya na matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira, kama sehemu ya mwelekeo wa maendeleo unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here