Mradi wa maji miji 28 Chato ni historia iliyojaa mahaba

NA ANNAMARIA BONDA

MAJI hayana mbadala, wakati hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ikiendelea kuimarika katika maeneo mbalimbali hapa nchini,kalamu yangu inasafiri kwa umbali wa takribani kilomita 785 kutoka mji mkuu wa Tanzania, jiji la Dodoma hadi wilayani Chato.

Huu ni kati ya wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Geita ulioanzishwa mwaka 2012 ukijumuisha Wilaya ya Geita Mjini, Chato, Bukombe, Mbogwe na Nyang’hwale.
Mradi wa maji wa miji 28 Chato unaotarajiwa kuanza kutoa huduma muda si mrefu ukiwa ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa wananchi.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, Wilaya ya Chato ilikuwa na wakazi 584,963 na kutegemea shughuli mbalimbali za uzalishaji kama vile uvuvi kwa kutumia Ziwa Victoria, uchimbaji wa madini, ufugaji, kilimo na biashara.

Historia haidanganyi, ni Mwalimu mzuri katika kuelezea mambo yaliyokuwepo kabla na mabadiliko yaliyojiri hivi sasa, hususani katika suala la hali ya upatikanaji wa maji mjini na vijijini.

Katika Wilaya ya Chato, hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa ni asilimia 75, uzalishaji ukiwa ni lita milioni nne kwa siku na mahitaji ni lita millioni 8.

Serikali kwa kutambua hilo ilitia saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa miji 28 ambao unajumuisha miji ya Kayanga, Chato na Geita.

Lengo likiwa kuleta mapinduzi na kuongeza hali ya upatikanaji maji kwa wananchi. Gharama za utekelezaji wa mradi katika mji wa Chato ni kiasi cha Dola za Marekani milioni 17.6 ambazo ni takribani Shilingi bilioni 41.013.

Mradi huu utakapokamilika unatarajiwa kuhudumia wananchi wapatao 185,333 katika kata za Muungano, Chato, Bwina, Nyamirembe, Ilemela, Katende, Ilyamchele, Bukome na Nyamigogo zenye Vijiji 29.

Hivi sasa ujenzi wake umefika asilimia 85. Kazi zilizokamilishwa katika mradi hadi sasa ni Ujenzi wa chanzo (intake) chenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha lita 11,000,000 kwa siku yanayotoka katika Ziwa Victoria.

Ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji (WTP) wenye uwezo wa kuzalisha maji lita 10,000,000 kwa siku, ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 31.4, Ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 3,000,000.

Ulazaji wa bomba za usambazaji wa maji kwa urefu wa kilomita 30 na ununuzi wa pampu za kusukuma maji kutoka kwenye chanzo (Intake) Pamoja na Pampu za kusukuma maji kutoka eneo la mtambo wa kuchuja na kutibu maji.

Kwa kazi zilizofanyika na zinazoendele ili kukamilisha mradi huu ni kuleta tabasamu na kuchochea maendeleo katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na wakazi wa wilaya hiyo na wilaya za jirani kwa kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali na kuondoa adha walizozipata kuhusu huduma ya maji ikiwemo kutembea umbali mrefu,changamoto ya mgao wa maji, migogoro katika familia, maji ya kunyweshea mifugo na kuondosha adha yam aji yasiyokuwa na ubora kwa baadhi ya maeneo.

Mradi wa maji wa miji 28 ni safari ya mabadiliko yenye mwanga unaojaza tumaini katika mioyo ya wananchi wa eneo hilo ambao hauwezi kuzima na simulizi ambayo sio ya kupita kwa kuandikwa kwa kalamu yangu, lakini kumbukumbu na tabasamu la dhahabu kutoka katika uso wa kila wananchi.

Mabadiliko yote yanayotekea ni kujitoa na juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa muda mrefu amenui “kumtua mama ndoo yam aji kichwani” na kutafuta fedha zitakazo tumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya maji kwa diplomasia kubwa kwa nchi washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kwa wananchi na wanufaika, yapo mambo ya msingi katika tabasamu la kupata huduma ya maji safi. 

Kukamilika kwa mradi ni jambo moja na utunzaji wa mradi huo ni jambo jingine kwasababu serikali inajenga miradi kwa wananchi ikitumia gharama kubwa hivyo ili kudumisha tabasamu hili lizidi kung’aa ni jukumu la kila mwananchi kulinda miundombinu ya maji kuendeleza huduma ya upatikanaji wa maji kuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na baadae.

Umoja wa Afrika (AU) suala la maji umelipa angalizo kubwa kwa tafiti ikionesha kuwa takriban watu Milioni 400 Afrika wanakosa huduma ya maji, na wengine Milioni 800 huduma za msingi kabisa za usafi wa mazingira ni za kusuasua.

AU imeamua kuwa na Agenda 2063 ili kuondosha tatizo hili na maji ni namba moja katika kuondosha umasikini na kuinua jamii.

Hapa Tanzania si haba, huduma ya maji inaimarika na maji yanawafikia wananchi kwa uwekezaji wa Serikali, hata hivyo ni muhimu kutunza huduma.

Miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni pamoja na makatazo yanayotolewa na mamlaka husika katika uendeshaji wa mradi, utoaji wa elimu kuhusu utunzaji wa miundombinu hiyo, uthibiti wa shughuli zinazofanywa karibu na miundombinu kama vile mabomba, matenki ya maji na eneo la chanzo cha maji ambacho ni roho ya mradi.

Hadi sasa wataalamu na wakandarasi wanaohusika na utekelezaji wa mradi huu wapo kazini kwa saa 24 kufanikisha huduma kwa wananchi.

Aidha, kutembea na maelekezo ya Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) kuhusu ukamilikaji wa mradi huo ili wananchi wa Chato waweze kupata huduma ya majisafi na salama ya uhakika kablam waka 2026 haujaisha.

“Dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “kumtua mama ndoo maji kichwani” sio hadithi za kufikirika, watendaji na wakandarasi mnatakiwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huu unakamilika na kuanza kutoa huduma na kuhusu jambo hili hatutasita kuchukua hatua kwa wakandarasi na watendaji wazembe watakao jaribu kukwamisha ukamilishwaji wa mradi huu”.

Hayo ni matamanio yalitolewa na Waziri Mhe. Aweso alipofanya ziara ya kikazi wilayani Chato mtaa wa Buzirayombo ili kuona maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mapema Septemba 2026 akimtaka mkandarasi kampuni ya AFCONS na VIJETA zote za India kuanza majaribio ya kusukuma maji mapema mwezi Oktoba 2026.

Kwa uchache ni kusema watendaji na wataalamu kutoka Sekta ya Maji ‘hawajapoa bado wapo eneo la kazi’ na kwasasa nguvu kubwa inaelekezwa katika ukamilishwaji wa miradi mbalimbali, miongoni mwake ukiwemo mradi wa maji wa miji 28, mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, Mradi ujenzi wa bwawa la Farkwa, mpango wa Gridi ya taifa ya maji na kuhakikisha huduma ya maji kwa miumndo mbinu rasmi inafika katika vijiji 1,575 ambavyo vimesalia hapa nchini, ambapo Sera ya Maji inaalika wadau mbalimbali kushirikiana na serikali, ikiwamo Sekta Binafsi.

Jambo linahusu maji ni muhimu katika kuleta utulivu katika jamii, pia usalama na sio hapa Tanzania peke yake, ni suala linaloigusa Dunia ikiwemo kuleta usawa katika upatikanaji wa huduma hiyo, kuzingatia anuai za jamii, maeneo ya vijijini na mijini.

Lengo ikiwa ni uhakika wa maji safi, salama nay a kutosha kwa maendeleo watu. Hivyo uhakika wa maji una uhusiano mkubwa na ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.
Ukweli unasimama kuwa uwekezaji katika huduma ya maji unaweza kuonekana siyo tu kwa gharama ya kutoa huduma kwa wananchi bali kama uwekezaji katika uzalishaji, ajira, afya, biashara, viwanda na maendeleo ya Taifa.

Maji ni roho inayosukuma uimara wa sekta nyingine katika jamii. “Tumesubiri kwa muda hamu tuliyonayo kwasasa sisi wananchi wa Chato ni kuona maji yakiwa yanatoka, tunayo matumaini kuwa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Maji yatafanyiwa kazi” mkazi wa Buzirayombo amesema hayo.

Hakika kila tone la maji litakalo toka katika mradi wa maji wa miji 28 Chato limebeba historia iliyojaa mahaba na tabasamu kutoka kwa Rais Mhe. Dkt. Samia .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here