LATRA yaweka mikakati mipya kuimarisha usafiri wa ardhini nchini

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeeleza hatua mbalimbali ilizochukua katika kuboresha huduma za usafiri nchini ikiwemo kuimarisha matumizi ya teknolojia, mifumo ya tiketi mtandao, usajili na mafunzo ya madereva na wahudumu, pamoja na maandalizi ya kuelekea matumizi mapana ya malipo ya kielektroniki.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Dkt. Habib Suluo ameyasema hayo Septemba 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Dkt.Suluo amesema,mabadiliko ya teknolojia na ukuaji wa sekta ya usafiri vinahitaji mifumo ya uendeshaji kwenda sambamba na uwekezaji unaofanyika katika miundombinu ili wananchi wapate huduma salama, bora na zenye ufanisi.

Amesema kuwa, ujenzi wa miundombinu pekee haukamilishi mahitaji ya sekta ya usafiri, bali unapaswa kuambatana na mifumo bora ya TEHAMA, uendeshaji na huduma.

“Kwa lugha rahisi tunaweza kusema, hardware is ready, but what about software?,” amehoji huku kauli hiyo ikilenga kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uendeshaji na teknolojia ili iendane na kasi ya maendeleo ya miundombinu ya usafiri nchini.

Wakati huo huo, LATRA imewataka watoa huduma za usafiri kujiandaa na kutekeleza kikamilifu matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika malipo ya nauli, ada na tozo.

Dkt.Suluo amesema, mabadiliko hayo yanaendana na matakwa ya kisheria yaliyowekwa kuhusu matumizi ya miamala ya kielektroniki, akiwataka wadau wa sekta hiyo kusoma, kuelewa na kujiandaa kutekeleza masharti yanayowahusu.

Amesema, matumizi ya mifumo hiyo yanahusu maeneo mbalimbali ya usafiri, yakiwemo malipo ya nauli za mabasi, huduma za usafiri wa mijini, vivuko, usafiri wa mtandao na huduma nyingine zinazohusiana na usafiri ardhini.

Dkt.Suluo amesema, takwimu zilizokusanywa na LATRA zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 hadi mwaka wa fedha uliopita, jumla ya abiria milioni 62.2 walisafiri kwa mabasi nchini na kutumia kiasi cha takribani Shilingi trilioni 2.13 kwa nauli.

Amesema, kati ya fedha hizo, takribani Shilingi trilioni 1.9 zililipwa kwa njia ya fedha taslimu, licha ya kuwepo kwa mifumo ya kielektroniki inayoweza kutumika kufanya malipo.

Kwa msingi huo, LATRA imewataka watoa huduma kuanza maandalizi mapema ya mifumo itakayowawezesha kukidhi mahitaji ya mabadiliko hayo na kuhakikisha huduma kwa abiria inaendelea kuwa rahisi na yenye ufanisi.

Vilevile,Dkt.Suluo amesema,matumizi ya teknolojia katika sekta ya usafiri yameendelea kupanuka kupitia huduma ya tiketi mtandao kwa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani iliyoanza kutolewa mwaka 2022.

Amesema, huduma hiyo imewawezesha abiria kukata tiketi za mabasi na treni kupitia mifumo ya kidijitali ikiwemo Safari Tiketi App.

Kwa mujibu wa Dkt. Suluo, hadi Juni 2026, watoa huduma 14 walikuwa wameunganisha mifumo yao na LATRA.

Amesema, mfumo huo umesaidia abiria kupata huduma za tiketi bila kulazimika kufika moja kwa moja katika vituo vya mabasi, huku ukiwawezesha kuchagua muda wa safari na aina ya basi kulingana na mahitaji yao.

Aidha, mfumo huo umesaidia kuwezesha malipo ya nauli kwa njia ya mtandao, huku abiria wanaofika katika ofisi za mawakala au kampuni za usafirishaji wakiendelea kuwa na fursa ya kufanya malipo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Dkt.Suluo amesema,huduma za safari za usiku pia zimekuwa na umuhimu kwa baadhi ya wasafiri, kutokana na kuwawezesha kutumia muda wa usiku kusafiri na kufika wanakokwenda bila kutumia muda mwingi wa mchana.

BODABODA NA BAJAJI

Akizungumzia mwenendo wa sekta hiyo, Dkt. Suluo amesema,mazingira ya usafiri nchini yamebadilika kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya pikipiki na bajaji, hali iliyopanua wigo wa huduma zinazopatikana kwa wananchi.

Amesema, LATRA inasimamia makundi makuu matatu ya vyombo vya usafiri ambayo ni magari ya abiria (PSV), magari ya mizigo (GSV) na magari ya kukodi.

CPA Dkt.Saluo amesema, kundi la magari ya kukodi limeendelea kukua na linajumuisha bodaboda, bajaji, teksi, magari ya shule, magari ya watalii pamoja na magari yanayotoa huduma maalumu ikiwemo usafirishaji wa abiria kwenda na kutoka viwanja vya ndege.

Amesema, mabadiliko hayo yanaongeza chaguo la usafiri kwa wananchi na yanaendelea kubadilisha muundo wa soko la usafiri ardhini.

LESENI ZA USAFIRISHAJI 

Dkt.Suluo amesema,katika kipindi cha miaka mitano, idadi ya leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya abiria, mizigo na magari ya kukodi imeongezeka kutoka 239,953 mwaka 2021/22 hadi 590,468 mwaka 2025/26.Hii ni sawa na ongezeko la leseni 350,515 katika kipindi hicho.

Amesema,ongezeko hilo linaonesha kupanuka kwa shughuli za usafiri na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika kundi la magari ya kukodi, pikipiki na bajaji zimeendelea kuwa sehemu kubwa ya vyombo vilivyosajiliwa, jambo linaloonesha nafasi inayoongezeka ya usafiri huo katika kuwahudumia wananchi.

MADEREVA 15,547 WAFANYA MITIHANI

Katika eneo la usalama wa usafiri, Dkt. Suluo amesema, LATRA imeendelea kusimamia usajili na uthibitishaji wa madereva wanaotoa huduma za usafiri wa umma na mizigo.

Amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 hadi 2025/26, jumla ya madereva 15,547 walisajiliwa na kufanya mtihani wa kuthibitishwa na LATRA kupitia Mfumo wa Kutahini Madereva (DTS).

Kati yao, madereva 8,642 sawa na wastani wa asilimia 56 walifaulu na kuthibitishwa.

Dkt.Suluo amesema, LATRA imeweka pia utaratibu wa madereva wa safari za usiku kwa mabasi ya abiria na mabasi ya kukodishwa kutumia kitufe maalumu cha utambuzi (i-button).

Amesema,mifumo ya Vehicle Tracking System (VTS) pamoja na i-button imeendelea kutumika katika kufuatilia mienendo ya madereva barabarani na kusaidia kuimarisha usalama wa huduma za usafiri.

WAHUDUMU 7,216 WAPATIWA MAFUNZO

Kwa upande wa wahudumu wa magari, Dkt. Suluo amesema,LATRA iliandaa mtaala wa kozi fupi ya wiki moja kwa kushirikiana na taasisi za elimu zikiwemo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Biashara (CBE), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

Amesema,mafunzo hayo yanawajengea wahudumu uwezo wa kuelewa sheria, kanuni na taratibu zinazohusu huduma za usafiri, pamoja na namna ya kuwahudumia abiria na wateja.

Dkt.Suluo amesema, utekelezaji wa jukumu hilo ulianza mwaka 2023/24, ambapo wanafunzi 656 walipata mafunzo na kufaulu.

Idadi hiyo imeendelea kuongezeka na kufikia 7,216 hadi Juni 2026, huku wahudumu wanaofaulu wakitakiwa kuwasilisha maombi ya usajili kupitia Mfumo wa Usajili na Udhibiti wa Usafiri (RRIMS).

LATRA YASAJILI KAMPUNI 22 ZA TEKSI MTANDAO

Katika huduma za teksi mtandao, Dkt. Suluo amesema,LATRA imesajili kampuni 22 zinazowaunganisha watoa huduma wenye magari 23,532 yenye leseni hai.

Amesema, hatua hiyo imeongeza wigo wa huduma za usafiri zinazopatikana kupitia teknolojia na kuwawezesha wananchi kupata huduma za usafiri kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

Aidha, katika kipindi cha mwaka 2023/24 hadi 2025/26, LATRA ilitoa vyeti kwa mawakala 100 wakiwemo kampuni 69, vyama vya ushirika saba, taasisi za umma 23 na mtu mmoja binafsi.

Mawakala hao walihusika katika utoaji wa sehemu kubwa ya leseni za pikipiki, huku wakikusanya jumla ya Shilingi bilioni 7.9 na kulipwa kamisheni ya Shilingi bilioni 2.

USAFIRI WAGUSA SEKTA NYINGI ZA UCHUMI

Dkt. Suluo amesema,mchango wa sekta ya usafiri hauishii katika kusafirisha abiria kutoka eneo moja kwenda jingine, bali una uhusiano mpana na shughuli nyingine za kiuchumi.

Ametoa mfano wa msafiri wa masafa marefu ambaye anapofika katika eneo analokwenda anaweza kutumia huduma za hoteli, migahawa, teksi, magari ya kukodi na huduma nyingine za kibiashara.

Kwa mantiki hiyo, amesema ukuaji wa sekta ya usafiri unaweza kuendelea kuchochea shughuli katika sekta nyingine zinazotegemea mwendo wa watu na bidhaa.

MAANDALIZI YA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU

Dkt.Suluo pia ametangaza maandalizi ya Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2026, yatakayofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 24 hadi 26, 2026.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Kuharakisha Usafiri Endelevu: Usafiri Salama, Rafiki kwa Mazingira na Jumuishi.”

Kwa mujibu wa LATRA, washiriki wapatao 2,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wameomba kushiriki katika maadhimisho hayo.

Tukio hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya majadiliano kuhusu mwelekeo wa sekta ya usafiri, usalama wa safari, matumizi ya teknolojia na ujenzi wa mifumo ya usafiri inayozingatia mazingira na mahitaji ya makundi mbalimbali ya wananchi.

TAHADHARI KIPINDI CHA MVUA ZA EL NINO

Akizungumzia maandalizi ya kipindi cha mvua, Dkt. Suluo amewataka wadau wa usafiri ardhini wakiwemo wamiliki wa vyombo vya usafiri, madereva, abiria na watoa huduma kuchukua tahadhari kabla, wakati na baada ya safari.

Pia,amewataka wananchi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kutoka mamlaka husika na kuzingatia maelekezo yanayotolewa kuhusu hali ya barabara, miundombinu na usalama wa safari.

Amesisitiza kuwa, maandalizi ya mapema, matumizi sahihi ya teknolojia na uzingatiaji wa taratibu za usalama ni miongoni mwa mambo muhimu katika kuhakikisha sekta ya usafiri inaendelea kutoa huduma kwa ufanisi, hasa katika vipindi vya mabadiliko ya hali ya hewa.

Vilevile, LATRA imeeleza kuwa, mwelekeo wa sekta ya usafiri ardhini unaendelea kuelekea katika matumizi makubwa zaidi ya teknolojia, huduma za kidijitali, mifumo ya ufuatiliaji na usafiri endelevu, huku wadau wakihimizwa kujiandaa na mabadiliko hayo ili kuendana na mahitaji ya uchumi na wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here