TANGA-Mahakama ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga mbele ya Hakimu, Mheshimiwa Kavumo Masewa Mndeme SRM katika shauri la Rushwa namba 14673/2026 imemtia hatiani,Bw. Salieli Dunstan Kimambo ambaye ni Mkandarasi na Mkurugenzi wa Saljos Construction Co. Ltd kwa kosa la kuisababishia mamlaka hasara kwa kutoa risiti ya EFD ya kughushi ya Shilingi 1,458,000.
Hatua hiyo imechukuliwa Septemba 15,2026 ambapo mshatakiwa alishtakiwa kwa shtaka la kuisababishia mamlaka hasara kinyume na Aya ya 10(1)(4) ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [R:E 2002].
Mshtakiwa alikutwa na hatia na kumrejeshea muathirika ambaye ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jumla ya Shilingi 4,374,000 ikiwa Shilingi 1,458,000 ni adhabu ya kutotoa risiti kwa wakati na Shilingi 2,916,000 adhabu ya kutoa risiti ya kughushi.
Shauri hilo limeendeshwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Wilaya ya Lushoto, John Chihangala.
