NA DIRAMAKINI
UJUMBE wa maafisa na wakufunzi wakuu 30 kutoka Chuo cha Kamandi na Mafunzo ya Maafisa wa Namibia (Namibia Command and Staff College) umeanza ziara ya wiki moja nchini Rwanda.

Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu wa kijeshi na kujifunza uzoefu wa Rwanda katika mageuzi ya sekta ya ulinzi na usalama, utawala pamoja na ujenzi wa taifa baada ya migogoro.
Ujumbe huo, kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Rwanda unaongozwa na Kamanda wa Chuo hicho, Brigedia Jenerali Erastus Benhard Nathinge ambaye pamoja na wajumbe wengine Septemba 15,2026 wametembelea Wizara ya Ulinzi ya Rwanda na Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF).
Katika ziara hiyo, ujumbe huo umepewa maelezo kuhusu historia, maendeleo na mabadiliko ya RDF katika kikao kilichoongozwa na Brigedia Jenerali Patrick Karuretwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kijeshi na Msemaji wa Ulinzi.
Brigedia Jenerali Karuretwa ameandamana na Brigedia Jenerali Louis Kanobayire, anayesimamia masuala ya elimu na mafunzo ya kijeshi ndani ya RDF.

Pia,wajumbe wameelezwa kuhusu safari ya mabadiliko ya RDF kutoka katika harakati za ukombozi na kuwa taasisi ya kijeshi ya kisasa na yenye weledi, inayolenga kuchangia maendeleo ya taifa, amani ya kikanda na usalama wa kimataifa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Brigedia Jenerali Karuretwa amesisitiza uhusiano mzuri wa kiulinzi na kijeshi uliopo kati ya Rwanda na Namibia, akieleza kuwa ziara hiyo inatoa fursa muhimu kwa pande hizo mbili kubadilishana uzoefu na mbinu bora, hususan katika eneo la elimu na mafunzo ya kijeshi.
Amesema,ushirikiano huo ni sehemu ya mahusiano mapana ya nchi hizo mbili, huku ziara hiyo ikiwa fursa kwa maafisa wa Namibia kujifunza uzoefu wa Rwanda katika kujenga taasisi za ulinzi na usalama.
Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Nathinge ameeleza kuwa, ziara hiyo inalenga kuongeza uelewa na kubadilishana uzoefu katika masuala ya kijeshi, akisisitiza pia uhusiano wa muda mrefu kati ya Rwanda na Namibia.
Amerejea ziara ya kiserikali iliyofanywa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame nchini Namibia mwaka 2019, akitaja hatua hiyo kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa Nathinge, majeshi ya ulinzi ya nchi hizo mbili yanaendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali, yakiwamo mafunzo ya kijeshi na utayari wa kufanya operesheni kwa pamoja, hasa katika utekelezaji wa majukumu ya kimataifa ya kulinda amani.

Mbali na shughuli za kijeshi, ujumbe huo umetembelea Kigali Genocide Memorial, ambako uliweka heshima kwa waathirika wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea Rwanda mwaka 1994.
Baada ya hapo, wajumbe walitembelea Campaign against Genocide Museum ikiwa ni sehemu ya kujifunza zaidi kuhusu historia ya Rwanda, matukio yaliyosababisha mauaji hayo na mchakato wa nchi hiyo katika kukabiliana na athari za mauaji ya kimbari.

Ziara hiyo inaendelea kwa wiki moja na ratiba yake inatarajiwa kuwapeleka wajumbe katika Chuo cha Kamandi na Mafunzo ya Maafisa cha RDF, pamoja na taasisi zinazohusika na ustawi wa wanajeshi.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Zigama CSS na Military Medical Insurance, pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali ya Rwanda.
Ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa kwa maafisa hao wa Namibia kujifunza uzoefu wa Rwanda katika uendeshaji wa taasisi za kijeshi, elimu na mafunzo ya maafisa, ustawi wa wanajeshi, pamoja na mchango wa jeshi katika masuala ya amani na usalama wa kikanda na kimataifa. (MoDR)