NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kupokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mama Fatma Karume.
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kilichotokea leo tarehe 21 Septemba, 2026."
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa leo Septemba 21,2026 huku akitoa pole kwa familia kwa kuondokewa na mpendwa wao.
"Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, familia yangu na kwa niaba yangu binafsi, natoa pole na rambirambi zangu za dhati kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe.Amani Abeid Karume, familia ya Hayati Sheikh Karume, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote walioguswa na msiba huu."
Rais Dkt.Mwinyi amesema, kifo cha Mama Fatma Karume ni pigo kwa familia na Taifa kwa ujumla. "Tutamkumbuka kwa heshima na kuthamini mchango wake katika jamii na katika historia ya Zanzibar.
"Namwomba Mwenyezi Mungu awajalie subira, faraja na uvumilivu familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
"Aidha, namwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mama Fatma Karume mahali pema peponi.Amina."
Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.
