SADC yawauma sikio wadau wa habari, mawasiliano na mahusiano katika ukanda huo

JUMUIYA ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umewataka wadau wa habari, mawasiliano na mahusiano katika ukanda huo kuongeza taarifa na simulizi zinazoeleza kwa kina namna ushirikiano wa kikanda unavyogusa maisha ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa SADC, Bi. Barbara Lopi, wakati akizungumza na wadau wa Mawasiiano na Mahusiano wa nchi wanachama katika kikao cha kujadili namna ya kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu shughuli, fursa na manufaa ya ushirikiano wa kikanda, kilichofanyika kwa njia ya Mtandao.

Bi. Lopi alisema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuunganisha sera na mipango ya SADC na maisha halisi ya wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuongeza habari zinazolenga kuonesha matokeo ya ushirikiano huo kwa jamii.

Alisema utekelezaji wa Mkakati wa Mawasiliano na Uhamasishaji wa SADC wa mwaka 2025–2030 unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu dhamira ya SADC, kuongeza mwonekano wa shughuli zake na kuimarisha uelewa wa manufaa ya ushirikiano wa kikanda.

“Vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuunganisha mipango ya kikanda na maisha ya kila siku ya wananchi. Kupitia kazi yenu, sera zinaeleweka, mafanikio yanaonekana na fursa zinapatikana kwa wananchi,” alisema Bi. Lopi.

Kwa mujibu wa Bi. Lopi, taarifa kuhusu mipango ya SADC zinapaswa kwenda zaidi ya kueleza sera na maamuzi, bali zioneshe namna utekelezaji wake unavyobadilisha maisha ya wananchi.

Alitoa mfano wa biashara za kikanda, akisema wananchi wanaposikia kuhusu mpango wa biashara wa kikanda, wanapaswa kuelewa unamaanisha nini kwa wafanyabiashara, ajira, kipato na maisha yao.

Aidha, alisema maboresho ya korido za usafirishaji na uanzishwaji wa vituo vya pamoja vya mipakani, maarufu kama One-Stop Border Posts, vinapaswa kuangaliwa pia kwa kuzingatia namna vinavyorahisisha biashara, kuongeza ufanisi na kuimarisha muunganiko wa nchi za SADC.

“Ushirikiano wa kikanda unakuwa na maana zaidi pale wananchi wanapoona athari zake katika maisha yao. Unakuwa na maana pale wakulima wanapopata taarifa za hali ya hewa na kuongeza uzalishaji, wafanyabiashara wanapofikia masoko mapya na wajasiriamali wanapopanua biashara zao,” alisema.

Bi. Lopi aliwataka waandishi wa habari kuongeza habari za kibinadamu (human-interest stories) zinazoonesha kwa uwazi matokeo ya ushirikiano wa kikanda katika maisha ya wananchi.

Pia aliwahimiza wahariri kuunga mkono uandishi unaoangazia changamoto pamoja na suluhisho, huku ukizingatia weledi, usahihi na uwajibikaji wa kiuandishi.

Kwa upande wa vyombo vya habari vya jamii, alisema kuna umuhimu wa kutumia lugha zinazofahamika na wananchi, ikiwemo lugha za maeneo husika, ili masuala ya kikanda yawe rahisi kueleweka na kuwafikia watu wa makundi mbalimbali.

Bi. Lopi alisema SADC Secretariat iko tayari kuimarisha ushirikiano na wadau wa habari kupitia utoaji wa taarifa kwa wakati, upatikanaji wa machapisho na bidhaa za mawasiliano za SADC, pamoja na kuwawezesha waandishi kupata wataalamu wa masuala mbalimbali ya kikanda.

Alisema ushirikiano huo pia utahusisha kuibua na kusambaza maudhui ya kikanda katika majukwaa mbalimbali ya habari na kushirikiana katika kutengeneza simulizi zinazowafikia wananchi kwa njia rahisi na yenye mvuto.

Vilevile Bi. Lopi, alisema kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yanayohitaji uelewa mpana wa wananchi ni SADC Vision 2050, Regional Indicative Strategic Development Plan (RISDP) 2020–2030 pamoja na SADC Communication Awareness and Visibility Strategy 2025–2030.

Alisema wadau wa mawasiliano wanaweza kusaidia wananchi kuelewa namna mipango hiyo inavyolenga kuchangia amani, maendeleo endelevu, ustawi na ustahimilivu wa nchi za ukanda wa SADC.

Bi. Lopi pia alitoa wito wa kuongezeka kwa habari zinazoangazia maendeleo, ubunifu, ustahimilivu na fursa zinazopatikana barani Afrika na katika ukanda wa SADC.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa hilo halimaanishi vyombo vya habari kuacha kuibua changamoto au kufanya taarifa za uchunguzi, badala yake, alisema kuna umuhimu wa kuwasilisha picha yenye uwiano, sahihi na pana kuhusu safari ya maendeleo ya Afrika kwa kuangazia changamoto pamoja na juhudi zinazofanyika kuzitatua.

“Si suala la kupuuza changamoto au kuepuka taarifa muhimu za ukosoaji, ni suala la kuwasilisha picha yenye uwiano, sahihi na pana kuhusu safari ya maendeleo ya Afrika,” alisema.

Alisema kupitia taarifa sahihi, za wakati na zenye athari, vyombo vya habari vinaweza kusaidia wananchi si tu kusikia kuhusu SADC, bali pia kuielewa, kutambua manufaa yake na kutumia fursa zinazotokana na kazi za jumuiya hiyo.

Bi. Lopi alisema matarajio ya kikao hicho ni kupata mapendekezo na hatua za vitendo zitakazosaidia kuimarisha mawasiliano, uhamasishaji na mwonekano wa SADC, pamoja na kujenga ushirikiano imara zaidi kati ya Sekretarieti ya SADC na wadau wa vyombo vya habari.

Alisisitiza kuwa kupitia ushirikiano huo, SADC na vyombo vya habari vinaweza kuendeleza simulizi kuhusu ukanda unaosonga mbele kupitia ushirikiano, unaotengeneza fursa kwa wananchi na kujenga mustakabali wa pamoja wenye amani, ustawi na ustahimilivu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here