Tanzania yaalika wawekezaji kutoka Vietnam

DAR-Tanzania imewaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Vietnam kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali za Uchumi ikiwemo kilimo, miundombinu, madini, teknolojia na mawasiliano na Uchumi wa buluu.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb.) wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Vietnam uliofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 22, 2026 ukilenga kuwaunganisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania na Vietnam.

Amesema,Tanzania iko tayari kushirikiana na kampuni za Vietnam katika maeneo mbalimbali yenye fursa za uwekezaji ikiwemo kilimo, usindikaji wa mazao, biashara, teknolojia, miundombinu, madini, kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa samaki na sekta nyingine za uzalishaji, huku akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kimkakati kama Reli, Bandari, Nishati ya Umeme na Kongani za Viwanda na Usafiri wa Anga ili kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
"Tunawakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam kuja Tanzania na kutumia fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali ya uchumi. Tanzania iko tayari kushirikiana nao katika kukuza biashara na uwekezaji wenye manufaa kwa pande zote,”amesema Mhe. Millya.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Vietnam kwenye Mkutano huo ambaye ni Naibu Waziri wa Kilimo na Mazingira, Mhe. Nguyen Hoang Hiep, amesema nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania sio kwenye sekta ya mawasiliano peke yake bali pia katika maeneo mengine ikiwemo kukuza kilimo kupitia teknolojia ya kisasa na kwamba kinachohitajika ni pande hizi mbili kuandaa Mpango mzuri wa utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa.
Jukwaa hilo la Biashara lilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Burhani na wadau wengine kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Vietnam ambao pia walitumia nafasi hiyo kunadi fursa zilizopo kwenye maeneo yao ikiwemo TISEZA, Bodi ya Korosho, Kampuni ya Uzalishaji Kahawa ya Tanganyika (TANICA), Tume ya Taifa ya Umwagiliji (NIRC) na Kampuni za Vietnam za Intimex, VinGroup na Philimex.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here