Nchi 22 za Afrika zimekutana Tanzania kubadilishana uzoefu wa mtaala unaozingatia umahiri-Profesa Shemdoe

DAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema nchi 22 za Afrika zimekutana nchini katika Mkutano wa Sita wa Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kuhusu namna mabadiliko ya mitaala inayozingatia umahiri yanavyotekelezwa katika mataifa yao.
Prof. Shemdoe amesema hayo leo Septemba 22, 2026 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, mara baada ya kufungua Mkutano wa Sita wa Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ambapo Tanzania ni nchi mwenyeji kwa mwaka huu.

“Mataifa haya ya Afrika yatabadilishana uzoefu wa mitaala inayozingatia stadi na umahiri, hivyo mwanafunzi akihitimu anakuwa amepata ujuzi ambao utamwezesha kuutumia katika fani mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuendesha maisha yake,” amesema Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amesema katika mkutano huo pia yanashiriki mataifa kutoka nje ya bara la Afrika kwa ajili ya kujionea namna mataifa ya Afrika yanavyotekeleza mitaala inayozingatia umahiri, ikiwemo Tanzania ambayo imeachana na Mtaala wa mwaka 2014 na sasa inatekeleza Mtaala mpya wa mwaka 2023 unaolenga kumpa mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari ujuzi unaohitajika katika maisha na shughuli mbalimbali.
"Sote ni mashahidi kwamba Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule 103 za amali ambazo zimejengwa nchi nzima, na shule hizi ndizo zitakazowezesha utekelezaji wa mtaala huu wa mwaka 2023 unaozingatia umahiri. Hivyo, washiriki wa mkutano huu watapata fursa ya kujionea hatua tuliyoipiga katika utekelezaji wa mtaala huo,” Prof. Shemdoe amesisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Taaluma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bi. Mwanahamis Adam Ameir, amesema mkutano huo ni muhimu sana katika kipindi hiki ambacho mageuzi mbalimbali yanahitajika katika mifumo ya elimu, hivyo Tanzania itapata fursa ya kubadilishana uzoefu na kupata uelewa wa mambo muhimu ya kuzingatia katika utekelezaji wa Mtaala mpya unaozingatia umahiri.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth Komba, amesema mkutano huo wa siku nne unatarajiwa kuzaa Azimio la Dar es Salaam kuhusu Mitaala ya Afrika, Mwongozo wa Uandaaji wa Mitaala Barani Afrika, pamoja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji na uandaaji wa mitaala barani Afrika.

Ameongeza kuwa, siku ya mwisho, wageni watapelekwa katika shule mbalimbali ili kujionea namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza Mtaala mpya wa Elimu wa mwaka 2023.
Kupitia mkutano huo, Tanzania inatarajia kupata maarifa, uzoefu na ubunifu wa kimitaala utakaosaidia kuimarisha mfumo wa elimu unaozalisha wananchi wenye maarifa, ujuzi, ubunifu na maadili, pamoja na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa kisasa.

Kwa msingi huo, mkutano huo una umuhimu katika kufanikisha matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha elimu inayojenga rasilimali watu yenye ujuzi, umahiri na uwezo wa kutumia maarifa na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here