NA JOHN MAPEPELE,
WAF-New York
TANZANIA imetoa wito kwa nchi za Afrika na wadau mbalimbali wa sekta ya kuweka mikakati endelevu ili kuharakisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika jijini New York leo kuhusu kuimarisha ubunifu wa ndani na kuharakisha matumizi ya zana mpya za kukabiliana na malaria,Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema nchi za Afrika zinapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kuendeleza, kugharamia na kuhakikisha upatikanaji wa zana zinazohitajika kuondokana na malaria.
Alisema umuhimu wa jambo hilo ni mkubwa, akieleza kuwa malaria inaendelea kusababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu kila mwaka, huku Afrika ikibeba sehemu kubwa zaidi ya mzigo huo.
“Ni vigumu kupata familia Tanzania ambayo haijawahi kukesha usiku mzima na mtoto akiwa na homa, wakitumaini kuwa ni homa ya kawaida tu. Mara nyingi huwa ni malaria,” Mchengerwa alisema.
Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya malaria hayawezi tena kutegemea pekee teknolojia zinazoagizwa kutoka nje au ufadhili wa kimataifa, akisema nchi za Afrika zinahitaji kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa muhimu za afya karibu na jamii zinazozihitaji.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, Tanzania tayari imejijengea historia katika kuchangia ubunifu na maendeleo ya teknolojia za kukabiliana na malaria.
Alieleza kuwa Tanzania ilianza mapema kuzalisha vyandarua vyenye dawa za kuua mbu jijini Arusha, huku Kibaha kukiwa na uzalishaji wa viuatilifu vya kibiolojia vinavyolenga kuua mazalia ya mbu kabla ya mbu hao kukua na kuwa mbu kamili.
Tanzania pia imekuwa ikishiriki katika tafiti za kutathmini teknolojia mpya za kuzuia malaria. Mchengerwa alitaja utafiti mkubwa uliofanyika Misungwi, Mkoa wa Mwanza, ambao ulisaidia kutoa ushahidi kuhusu ufanisi wa vyandarua vyenye viambata viwili vya kuua mbu.
Waziri huyo alisema uzoefu huo unaonyesha kuwa nchi za Afrika hazipaswi kuwa watumiaji pekee wa ubunifu unaozalishwa katika maeneo mengine duniani, bali zinapaswa kuendelea kuwa vituo ambako teknolojia mpya zinafanyiwa utafiti, majaribio, uzalishaji na hatimaye kutumika.
Mchengerwa pia alizungumzia utafiti unaofanywa na wanasayansi wa Tanzania kuhusu teknolojia ya gene drive, ambayo ni mbinu mpya inayoweza kutumika kubadilisha idadi ya mbu au uwezo wao wa kusambaza malaria.
Katika Taasisi ya Afya ya Ifakara, kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), watafiti wa Tanzania wanafanya utafiti kuhusu mbu waliobadilishwa vinasaba.
Mchengerwa alisema kazi hiyo inaonyesha kuongezeka kwa uwezo wa wanasayansi vijana wa Tanzania na kuwaalika viongozi wa kimataifa pamoja na washirika wa maendeleo kutembelea taasisi za utafiti nchini.
Hata hivyo, alikiri kuwa teknolojia kama gene drive zinaibua maswali muhimu kuhusu usalama, udhibiti wa kisheria na kukubalika na jamii.
“Watu hawatakubali aina mpya ya mbu karibu na makazi yao kwa sababu tu waziri amewaambia kuwa ni salama,” alisema, akisisitiza kuwa jamii lazima ihusishwe na ushahidi uwekwe wazi kabla ya teknolojia hizo kuanza kutumika.
Alisema Wizara zinazohusika na afya, mazingira na kilimo nchini Tanzania zinafanya kazi kwa pamoja katika masuala ya udhibiti na kanuni zinazohusiana na teknolojia hiyo.
“Kuaminiana huchukua muda mrefu zaidi kujengwa kuliko kujenga maabara. Lakini muda huo unastahili kutumika,” Mchengerwa alisema.
Mchengerwa alisema mafanikio ya kisayansi yatakuwa na manufaa madogo ikiwa teknolojia hizo zitashindwa kuwafikia watu wanaoathirika zaidi na malaria.
Alieleza kuwa matumizi ya vyandarua vyenye viambata viwili vya kuua mbu yameongezeka kwa kasi barani Afrika, huku idadi ya nchi zinazoanza kutoa chanjo dhidi ya malaria ikiendelea kuongezeka.
Pia alirejea hatua ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kuidhinisha matumizi ya spatial repellents, teknolojia inayolenga kuzuia mbu kuwafikia watu, kama sehemu ya zana zinazopanua uwezo wa kukabiliana na malaria.
Hata hivyo, Mchengerwa alisisitiza kuwa mafanikio ya teknolojia mpya ya afya yanapaswa kupimwa kwa kuangalia iwapo inawafikia wananchi majumbani mwao.
“Zana mpya huhesabika pale tu inapofika ndani ya nyumba ya mtu,” alisema.
Alisema msingi huo ndio unaoifanya Tanzania kusisitiza umuhimu wa uzalishaji wa bidhaa za afya nchini.
Tanzania inaendelea kutekeleza sera zinazolenga kuvutia uwekezaji katika sekta ya dawa, ikiwamo Mkakati wa Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa, kuanzishwa kwa kikosi kazi kinacholenga kuendeleza miradi ya uzalishaji, pamoja na utaratibu maalumu wa Green Lane kwa uwekezaji wa kimkakati.
Pia, Tanzania inaandaa mipango ya kuanzisha maeneo maalumu ya uzalishaji wa dawa.
Mchengerwa alisema lengo ni kupunguza ucheleweshaji usio wa lazima kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda vya dawa nchini.
Waziri huyo pia alionya kuwa mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya malaria yanaweza kurudi nyuma iwapo ufadhili wa programu hizo utapungua.
Akinukuu makadirio ya Umoja wa Afrika, alisema kupungua kwa asilimia 30 kwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya malaria kunaweza kusababisha ongezeko la visa vya malaria milioni 146 na vifo 397,000 ifikapo mwaka 2030, huku uchumi wa nchi za Afrika ukikabiliwa na hasara inayokadiriwa kufikia dola bilioni 37.
Alitoa wito wa kuwepo kwa ufadhili unaofuatana na hatua zote za kukabiliana na malaria-kuanzia utafiti, upatikanaji wa vibali vya udhibiti, uzalishaji na ununuzi wa bidhaa, hadi kuzifikisha kwenye kaya ya mwisho.
Mchengerwa pia alikiri umuhimu wa serikali za Afrika kuongeza mchango wao wenyewe katika kugharamia programu za malaria, huku zikiendelea kushirikiana na washirika wa kimataifa na sekta binafsi.
“Programu inayotegemea kabisa bajeti ya mtu mwingine inaweza kuzimwa na mtu huyo huyo,” alisema.
Mchengerwa alieleza kuwa mkakati wa Tanzania ni sehemu ya azma pana ya Afrika ya kuimarisha uzalishaji wa dawa na chanjo ndani ya bara.
Tanzania, ambayo inahifadhi Sekretarieti ya Muungano wa Viongozi wa Afrika wa Kupambana na Malaria (ALMA), inataka kushirikiana na nchi nyingine za Afrika kuendeleza ajenda hiyo, alisema.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, ili zana mpya ya kukabiliana na malaria ifanikiwe, mambo kadhaa yanapaswa kuzingatiwa: sayansi yenye ushahidi thabiti, udhibiti madhubuti, ufadhili endelevu, uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo ndani ya nchi pale inapowezekana na imani ya jamii.
“Ukiondoa hata moja kati ya hayo, maendeleo yanasimama,” alisema.
Akinukuu methali ya Kiswahili, “Kidole kimoja hakivunji chawa,” Mchengerwa alisisitiza umuhimu wa nchi kushirikiana katika mapambano dhidi ya malaria.
“Hakuna nchi itakayomaliza tatizo hili peke yake,” alisema.
Mchengerwa alihitimisha hotuba yake kwa kurejea maneno ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliyesema mwaka 1959 kuhusu kuwasha mshumaa juu ya Mlima Kilimanjaro ili mwanga wake uangaze nje ya mipaka ya Tanzania na kutoa matumaini na heshima.
Kwa Mchengerwa, maono hayo bado yana umuhimu katika mapambano dhidi ya malaria.
Alisema ana matumaini kuwa uwekezaji wa Tanzania katika sayansi, uzalishaji na mifumo ya afya utachangia kujenga siku zijazo ambazo malaria haitakuwa tena tishio kubwa kwa familia za Afrika.
“Natumaini siku moja mwanga huo utafikia mwisho wa malaria, na wajukuu zetu watakutana na ugonjwa huu katika vitabu vya historia pekee na kujiuliza kwa nini ilituchukua muda mrefu kiasi hicho,” alisema.



