NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza rasmi kuwaondoa raia wa Shirikisho la Jamhuri ya Nigeria katika Utaratibu wa Visa Rejea (Referred Visa).
Tangazo hilo limetolewa Septemba 25, 2026 na Idara ya Uhamiaji chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, ACI Paul J. Mselle, uamuzi huo umefuatia marekebisho yaliyochapishwa katika Gazeti la Serikali Namba 246 la mwaka 2026.
"Idara ya Uhamiaji inapenda kuutaarifu umma na wageni wote kuwa raia wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria wameondolewa rasmi katika Utaratibu wa Visa Rejea (Referred Visa).
"Hatua hii imefikiwa kufuatia kufanyika kwa marekebisho ya Kanuni za Utekelezaji wa masuala ya Visa na kutangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Namba 246 la Mwaka 2026."
Kuanzia sasa, raia wa Nigeria wanaosafiri kuja Tanzania watafuata utaratibu wa kawaida wa maombi ya visa kulingana na Sheria na Miongozo iliyopo.
Awali, raia waliokuwa katika kundi hilo walilazimika kupata kibali maalum kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kabla ya kupewa visa, utaratibu uliokuwa mrefu na mgumu.
Hatua hii inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kibiashara, utalii, uwekezaji na mahusiano ya watu na watu baina ya Tanzania na Nigeria, ambayo ni nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Tags
Breaking News
Habari
Kimataifa
Rais wa Nigeria Tanzania
Tanzania na Nigeria
Uhamiaji Nigeria
Uhamiaji Tanzania
Visa Rejea
