Utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Safari kwa Wageni wanaoingia Tanzania Bara kuanza rasmi Oktoba 1,2026

KUFUATIA kuchapishwa kwa Kanuni za Bima ya Safari kwa wageni wanaoingia Tanzania Bara kupitia Tangazo la Serikali (GN) Na. 256 la Mwaka 2026 tarehe 4 Septemba, 2026, zilizotokana na marekebisho ya Kifungu cha 134A cha Sheria ya Bima, Sura 394 yaliyofanywa kupitia Sheria ya Fedha ya 2025, Wizara ya Fedha inapenda kuutaarifu umma, wasafiri wa kimataifa, wadau wa utalii na taasisi zote husika kuwa utekelezaji wa Bima ya Safari kwa raia wa kigeni wanaoingia Tanzania Bara utaanza rasmi tarehe 1 Oktoba, 2026.
Katika kutekeleza matakwa ya sheria, umma unajulishwa kwamba:

1. Bima hii itakuwa ya lazima kwa wageni wote wanaoingia nchini, ikitoa kinga dhidi ya dharura za kimatibabu na itakuwa halali kwa muda usiozidi siku tisini na mbili (92), kwa ada ya bima (premium) ya Dola za Marekani arobaini na nne (USD 44) kwa kila mgeni.

2. Mashirika ya Bima ya Taifa (NIC) na lile la Zanzibar (NIC) yameteuliwa kutoa huduma ya Bima ya Safari kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar mtawalia.

Hivyo, raia wa kigeni atakayeingia nchini kupitia Tanzania Bara, atakata Bima ya Safari NIC, wakati raia wa kigeni atakayeingia nchini kupitia Zanzibar atakata Bima ya Safari ZIC.

Mashirika hayo yatawahudumia raia wa kigeni waliokata bima endapo majanga ya dharura yatatokea ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

3. Wageni wote wanahimizwa kufanya mipango inayohitajika na kupata bima kabla ya kuingia nchini, ili kurahisisha taratibu za kuingia na kuepuka usumbufu au ucheleweshaji wowote usio wa lazima utakaotokea mara baada ya kuwasili nchini.

Taarifa za kina kuhusu taratibu za ununuzi, maelezo ya kinga ya bima, njia za malipo na mifumo ya uhakiki zinapatikana kwenye Tovuti ya Shirika la Bima la Taifa (NIC): https://inbound.nicinsurance.co.tz/ na Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC): https://inbound.visitzanzibar.go.tz.

Wizara ya Fedha inathamini ushirikiano kutoka kwa wadau wote katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo na kuhakikisha wageni wanapata uzoefu mzuri na usio na kikwazo wanapotembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imetolewa na:

Dkt. Natu El-Maamry Mwamba

KATIBU MKUU NA MLIPAJI MKUU WA SERIKALI
WIZARA YA FEDHA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here