NA GODFREY NNKO
WASOMI wa vyuo vikuu nchini wamejipanga kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika kuzuia na kukomesha matumizi, usambazaji na biashara ya dawa za kulevya katika taasisi za elimu ya juu, wakisisitiza kuwa hawatarudi nyuma katika vita hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Katiba, Sheria na Utawala Bora wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Aron Mzelela Seni leo Septemba 1, 2026 wakati wa uzinduzi wa Klabu za Kupiga Vita Dawa za Kulevya Vyuoni uliofanyika katika Ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali za Wanafunzi kutoka vyuo na vyuo vikuu mbalimbali jijini Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akiwa Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo.
Seni amesema,mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano mpana wa mamlaka za Serikali, taasisi za elimu na wadau mbalimbali, akisisitiza kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu ni sehemu muhimu ya suluhisho la tatizo hilo.
Amesema,TAHLISO imedhamiria kuunga mkono juhudi za DCEA kwa kuhakikisha elimu ya kinga, uhamasishaji na ulinzi dhidi ya dawa za kulevya inawafikia wanafunzi katika taasisi za elimu ya juu nchini.
“Vita hivi vinahitaji ushirikiano mkubwa kati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na wadau mbalimbali, ikiwemo jeshi hili la wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini,”amesema.
Seni amesema, wanafunzi hawapaswi kujiona kuwa watazamaji katika mapambano hayo, bali wanapaswa kuwa sehemu ya msingi ya juhudi za kuzuia matumizi na biashara ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana.
“Tunaamini kwamba sisi vijana si watazamaji katika vita hii, bali ni sehemu muhimu kabisa ya suluhisho. Katika kufikia malengo ya kuanzisha klabu hizi, tunataka kuwapa wanafunzi nafasi ya kupata elimu ya kinga, uhamasishaji na kujenga mazingira salama ndani ya taasisi zetu za elimu ya juu,”amesema.
Pia,Seni amesema mpango wa kuanzisha klabu hizo haukuibuka ghafla, bali ulitokana na tafakuri ya pamoja ndani ya TAHLISO kuhusu namna bora ya kuwasaidia wanafunzi kujiepusha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Amesema,takribani miezi miwili iliyopita, yeye akiwa Kamishna wa Katiba, Sheria na Utawala Bora kwa kushirikiana na Kamati Maalum ya Katiba na Sheria, walianza kutafuta njia ya kupata suluhisho litakalowasaidia wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu kujiepusha na dawa za kulevya.
Amesema,hatua hiyo ilichukuliwa pia kwa kuzingatia Ibara ya 5(6) ya Katiba ya TAHLISO, inayowataka kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira salama yasiyo na viashiria vya uvunjifu wa haki na sheria za Tanzania.
“Hapo ndipo tulipopata wazo la kuanzisha klabu mahususi kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wetu waliopo vyuoni,”amesema.
Seni amesema,baadaye waliomba kukutana na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ambaye licha ya kuwa na majukumu mengi aliwapa nafasi ya kueleza hoja yao na kuridhia wazo la kuanzishwa kwa klabu hizo katika vyuo vikuu nchini.
Amesema,hatua hiyo iliwapa somo kubwa la uongozi, akimtaja Lyimo kuwa kiongozi anayesikiliza na kujali changamoto za wananchi na wadau mbalimbali.
Seni amesema,vyuo vikuu na vyuo vya kati ni vituo muhimu vya kuzalisha maarifa na wataalamu watakaoliongoza na kuliendeleza Taifa katika sekta mbalimbali.
Amesema,katika taasisi hizo ndipo wanapotoka wataalamu wa fani mbalimbali wakiwemo madaktari, wanasheria, walimu, waandishi, wachumi na viongozi wa baadaye, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanafunzi wanalindwa dhidi ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, amesema baadhi ya mazingira yanayowazunguka vijana yakiwemo changamoto za maisha na ushawishi unaoweza kujitokeza katika mazingira ya uhuru wa maisha ya chuoni, yanaweza kuwafanya baadhi yao kujiingiza katika matumizi au biashara ya dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Seni, baadhi ya wanafunzi wamejikuta wakikabiliwa na madhara makubwa ya kisheria baada ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, huku wengine wakianza kutumia dawa hizo kwa majaribio, kushawishiwa na marafiki au kutokana na changamoto mbalimbali za maisha.
Amesema, hali hiyo inahitaji hatua za mapema za elimu, kinga na uhamasishaji ili kuwaokoa wanafunzi ambao tayari wako katika mazingira hatarishi.
“Hata leo hii tunapozungumza, wapo baadhi ya wanafunzi wenzetu ambao wanatumia, wapo katika mazingira ya kutumia na wengine katika hatua mbalimbali, hivyo tunapaswa kuchukua hatua za mapema ili kuwaokoa,”amesema.
Akizungumzia umuhimu wa klabu hizo, Seni amesema hazipaswi kugeuka kuwa vikundi vya kawaida visivyo na matokeo, bali zinapaswa kuwa sehemu ya msingi ya kutoa elimu, ulinzi na msaada kwa wanafunzi.
“Klabu hizi tunazozindua leo si majengo ya matofali, wala si vikundi vya kupiga picha na kuweka machapisho katika mitandao ya kijamii ili tuweze kupata ‘likes’; hizi ni nguzo za ulinzi, elimu na ukombozi kwa kizazi chetu,”amesema.
Amesema, klabu hizo pia zitakuwa jukwaa la wanafunzi kuhamasishana kwa upendo kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa kujiepusha na matumizi na biashara yake.
Aidha, amesema klabu hizo zinapaswa kutoa mazingira salama kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto za matumizi ya dawa za kulevya kupata elimu, ushauri na msaada bila kuhukumiwa.
“Klabu hizi zitatoa nafasi salama kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto za matumizi ya dawa za kulevya kupata elimu, ushauri na msaada bila kuhukumiwa. Tunaishukuru DCEA kwa ushirikiano uliowezesha kufanikisha mchakato huu,” amesema.
Ni uzinduzi wa kihistoria
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema,uzinduzi wa Klabu za Kupiga Vita Dawa za Kulevya Vyuoni ni hatua ya kihistoria katika juhudi za mamlaka hiyo kuwafikia wasomi na kuwashirikisha katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Amesema,dawa za kulevya ni tatizo linaloathiri jamii duniani kote na linahitaji ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, wakiwemo wanafunzi na taasisi za elimu ya juu.
“Tatizo la dawa za kulevya ni janga la dunia ambalo sisi sote hapa tunapaswa kuhakikisha kwamba tunalipiga vita,” alisema.
Lyimo amesema,uamuzi wa kupeleka mapambano hayo katika ngazi ya vyuo vikuu umetokana na umuhimu wa taasisi hizo katika kujenga wataalamu na Taifa kwa ujumla.

Amesema,taifa lisilo na wasomi imara linakuwa katika hatari ya kushindwa kukabiliana na changamoto zake za maendeleo, hivyo ni muhimu kuwalinda wanafunzi dhidi ya dawa za kulevya ili waweze kutumia maarifa yao kulijenga Taifa.
“Kwa hiyo, kama wasomi ni kitovu na vyuo vikuu ni vitovu vya kuhakikisha kwamba nchi inasimama imara, ukishakuta dawa za kulevya zimeingia, zimeharibu wale wasomi, mwisho wa siku tutakuja kukosa watu ambao ni imara, watu ambao tunaweza kuwatumia sasa ili kuhakikisha wanaleta mawazo chanya, mawazo ya kuweza kulikuza Taifa na kuliendeleza Taifa,”amesema.
Tags
Dawa za Kulevya Vyuoni
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
TAHILISO




