NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imezindua Klabu za Kupiga Vita Dawa za Kulevya katika vyuo na vyuo vikuu kote nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Hatua hiyo inalenga kuwakinga wasomi dhidi ya madhara yanayotokana na dawa za kulevya na kuwawezesha kutumia maarifa,ubunifu na taaluma zao katika kutoa mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa.
Uzinduzi wa klabu hizo umefanyika leo Septemba 1,2026 katika Ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wanafunzi pamoja na viongozi wa Serikali za Wanafunzi kutoka vyuo na vyuo vikuu mbalimbali jijini humo.
Akizungumza katika uzinduzi huo mgeni rasmi, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema,tukio hilo ni la kihistoria kwa mamlaka hiyo kwa kuwa linafungua ukurasa mpya katika kuwafikia wasomi wa vyuo vikuu na kuwashirikisha kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Amesema, tatizo la dawa za kulevya ni janga la kimataifa linalohitaji ushiriki wa kila mmoja katika kulikabili, huku akisisitiza umuhimu wa kuanzia katika vyuo vikuu kutokana na nafasi yake katika kuandaa wataalamu na viongozi wa Taifa.
“Tatizo la dawa za kulevya ni janga la dunia ambalo sisi sote tunapaswa kuhakikisha kwamba tunalipiga vita. Lengo la kuja kwenye ngazi ya vyuo vikuu ni kutokana na kwamba wale wote wanaozalishwa vyuo vikuu tunajenga taaluma,tunajenga nchi,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, Taifa haliwezi kuwa imara bila kuwa na wasomi wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, kuchambua changamoto na kubuni suluhisho zitakazochochea maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Amesema, vyuo vikuu ni kitovu cha uzalishaji wa wataalamu na maarifa, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanafunzi wanalindwa dhidi ya athari za dawa za kulevya ambazo zinaweza kudhoofisha uwezo wao wa kitaaluma na hatimaye kuathiri maendeleo ya Taifa.


Amesema,endapo dawa za kulevya zitaingia katika mazingira ya vyuo vikuu na kuwaathiri wanafunzi, Taifa linaweza kupoteza nguvu kazi yenye uwezo wa kuzalisha mawazo mapya na suluhisho za changamoto mbalimbali.
“Kwa hiyo, kama wasomi ni kitovu na vyuo vikuu ni vitovu vya kuhakikisha kwamba nchi inasimama imara, ukishakuta dawa za kulevya zimeingia na kuwaangamiza wale wasomi, mwisho wa siku tutakuja kukosa watu ambao ni imara, watu ambao tunaweza kuwatumia ili kuhakikisha wanaleta mawazo chanya, mawazo ya kulikuza Taifa na kuliendeleza Taifa,” amesema.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, umuhimu wa wanafunzi wa vyuo vikuu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya hauishii katika kujilinda dhidi ya matumizi ya dawa hizo, bali pia kutumia taaluma na ubunifu wao kutafuta suluhisho la tatizo hilo.
Amesema, vyuo vikuu ni vituo muhimu vya kuzalisha wataalamu na maarifa yanayoweza kutumika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa, ikiwemo tatizo la dawa za kulevya.
Kwa msingi huo, amesema elimu inayotolewa kwa wanafunzi kuhusu dawa za kulevya inalenga zaidi kuzuia matumizi ya dawa hizo miongoni mwa vijana na wakati huohuo kujenga kizazi cha wataalamu kinachoweza kulielewa tatizo hilo kwa mtazamo wa kitaaluma na kisayansi.
Amesema,uelewa huo unaweza kusaidia Taifa kupata suluhisho linalotokana na ushahidi wa kisayansi, huku akibainisha kuwa DCEA inafikiria kutumia ubunifu wa wanafunzi katika teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Unde (AI) katika kukabiliana na tatizo hilo.
“Suluhisho ambalo linatumia Akili Unde (AI) na teknolojia katika kupunguza tatizo la dawa za kulevya nchini. Tunafikiria pia hapo baadaye tuanzishe mashindano kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wanaweza kubuni suluhisho kwa kutumia AI, teknolojia na taaluma mbalimbali zinazopatikana kwenye vyuo vikuu,”amesema.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mashindano hayo yanaweza kuwa jukwaa muhimu la kupata mawazo na ubunifu wa wanafunzi katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.
Amesema, eneo la vyuo vikuu na uwezo wa wasomi bado halijatumika kikamilifu katika mapambano hayo, hivyo Serikali kupitia DCEA inalenga kuimarisha ushiriki wa wanafunzi kwa kuwahamasisha kutumia uwezo wao wa kiakili na kitaaluma kutafuta majawabu ya changamoto hiyo.
“Wako watu wenye uwezo mkubwa sana, wako watu wenye ubunifu mkubwa kuliko hata kile walichofundishwa, ambao wanaweza kuja na suluhisho ambalo linaweza kuwa suluhisho la kudumu katika Taifa letu,”amesema.
Ameongeza kuwa, ubunifu wa wanafunzi unaweza kusaidia katika kudhibiti matumizi na uzalishaji wa dawa za kulevya, pamoja na kuzuia vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo.




"Tunataka kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya, kudhibiti uzalishaji wa dawa za kulevya, lakini pia kudhibiti watu kutojiingiza kirahisi kwenye matumizi ya dawa za kulevya ili tuweze kuokoa hiki kizazi cha wasomi ambao tunawategemea katika Taifa hili, ambao tunawategemea katika kukuza uchumi wa nchi yetu na katika sekta mbalimbali zinazoliunganisha Taifa na kuwa Taifa moja imara,”amesema.
Amesema,DCEA itaendelea kutumia kikamilifu fursa inayopatikana katika vyuo na vyuo vikuu kwa kuimarisha ushirikiano na wanafunzi, viongozi wa Serikali za Wanafunzi na wadau wengine, kwa lengo la kupata mbinu madhubuti na endelevu za kukabiliana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini.


Tags
Dawa za Kulevya Vyuoni
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)