Waziri wa Fedha ashiriki ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya AIIB

DOHA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar ameshiriki ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB), ambayo Tanzania ni nchi mwanachama asiye wa kikanda (Non-Regional Member) unaojadili namna ya nchi wanachama wanavyoweza kuimarisha ujenzi wa Miundombinu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Bi Zou Jiayi, Rais wa Benki ya AIIB, ameeleza dira mpya ya benki hiyo inayolenga kuongeza maradufu ufadhili wa kila mwaka kufikia dola bilioni 700 ili kukuza maendeleo ya miundombinu katika nchi wanachama wa taasisi hiyo.

Katika hotuba yake, Rais Zou alisisitiza kuwa benki hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa kitaaluma na kuzingatia miundombinu inayounga mkono ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya kidijitali, na maendeleo yanayomlenga binadamu.

Alibainisha kuwa,uvumbuzi ndio njia kuu ya kuleta matokeo chanya na kwamba benki hiyo itaendelea kuboresha mfumo wake wa biashara na vyombo vya kifedha.
Rais Zou alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, akibainisha kuwa maendeleo yanahitaji ushirikiano wa sekta binafsi na washirika wengine wa maendeleo.

Alieleza kuwa, Asia pekee inahitaji takriban dola trilioni 3 kwa mwaka katika uwekezaji wa miundombinu, kiasi ambacho serikali pekee haziwezi kukidhi.

Benki hiyo imeahidi kudumisha viwango vya juu vya uadilifu na kuendelea kuwa na maono ya kimataifa huku ikizingatia maendeleo ya Asia na kuimarisha ushirikiano na nchi wanachama.

Alitaja maeneo sita ya kipaumbele kupitia mpango mkakati mpya wa taasisi hiyo kuwa ni: Ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi; Uchumi mpya, Mabadiliko ya kidijitali; Uunganishaji wa kikanda; Uhifadhi wa mazingira; na Maendeleo yanayomlenga binadamu.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano huo, Rais Zou Jiayi alisema kuwa hadi kufikia mwaka 2026, AIIB ina nchi wanachama 111 (kati ya idadi hii, wakikanda ni 53 na wasio wa kikanda ni 58) waliokubaliwa na imeidhinisha zaidi ya dola bilioni 76 Marekani kwa miradi 384 ya miundombinu katika nchi hizo.
Alisema kuwa, Benki hiyo sasa inatafuta kuongeza kiwango na ubora wa shughuli zake huku ikidumisha kanuni za uendelevu wa kifedha, benki imara, na ufanisi wa kiutendaji.

Mwaka 2025, Tanzania ilijiiunga na taasisi hii kama Mwanahisa Mpya na Mkutano wa mwaka huu, ni mkutano wa kwanza kushiriki kama mwanachama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here