NA DIRAMAKINI
WAKALA wa Vipimo (WMA) mkoani Dodoma umewatoa hofu wananchi na kutoa onyo kali kwa wafanyabiashara na mawakala wa gesi ya kupikia wanaofanya biashara bila kuwa na mizani iliyohakikiwa katika maduka yao.
Wakala huo umesisitiza kuwa, kitendo hicho ni ukiukaji wa wazi wa sheria za vipimo na kinahatarisha haki za mlaji.
Akizungumza wakati jana wa kati wa zoezi la ukaguzi wa kushtukiza uliolenga wauzaji wa gesi ya kupikia jijini Dodoma, Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Bw.Said Ibrahim alieleza kuwa, lengo kuu la ukaguzi huo ni kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa ipasavyo kupitia vipimo sahihi vya bidhaa wanazonunua kila siku.
Akifafanua zaidi kuhusu wajibu wa wafanyabiashara, Bw. Ibrahim amesisitiza kuwa,kila mteja anayenunua mtungi wa gesi anapaswa kupimiwa ili kujiridhisha na uzito sahihi kabla ya kuondoka na bidhaa hiyo.
“Mteja yeyote anayenunua mtungi wa gesi anayo haki ya msingi ya kuhakikisha mtungi unapimwa kwanza ili kujiridhisha na uzito sahihi kabla ya kuondoka nao kwenda nyumbani. Wafanyabiashara wanapaswa kutambua kuwa kutokuwa na mizani katika duka la kuuzia gesi ni kosa kisheria,”ameeleza Bw. Ibrahim.
Zoezi hilo la ukaguzi lilibaini kuwa,baadhi ya mawakala wakubwa na wauzaji wa rejareja wamekuwa wakiuza bidhaa hiyo bila kuwa na mizani au kutumia mizani ambayo haijahakikiwa na Wakala wa Vipimo, jambo ambalo linaenda kinyume na Sheria ya Vipimo nchini.
WMA imewakumbusha wauzaji wote kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukiuka taratibu hizi.
"Tunaomba mawakala wakubwa wahakikishe wanawaelimisha wale wote wanaowauzia ili nao wawe na mizani kwenye vituo vyao vya mauzo. Mtu anapochukua mtungi anapaswa kuhakikisha anaupima kwanza kabla ya kumpelekea mteja au kabla mteja hajaupeleka nyumbani.”
Wakala wa Vipimo umesisitiza kuwa, operesheni hiyo ni endelevu kote mkoani Dodoma ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha zao wanaponunua gesi ya kupikia na kulinda usalama na haki za walaji kwa ujumla.

