NA GODFREY NNKO
KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6.25 katika robo ya nne ya mwaka 2026, kinachomalizika Desemba, 2026 hatua inayolenga kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi nchini.
Uamuzi huo umetangazwa leo Oktoba 8, 2026 jijini Dar es Salaam na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba wakati akizungumza na viongozi wa benki, taasisi za fedha na waandishi wa habari kuhusu tiba hiyo.
Gavana Tutuba amesema, uamuzi huo umefikiwa baada ya Kamati kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia, ambapo makadirio yanaonesha kuwa, uchumi wa Tanzania utaendelea kukua huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kubaki ndani ya lengo la muda wa kati la kati ya asilimia tatu na tano.
“Uamuzi huu unatokana na makadirio ya Benki Kuu yanayoonesha kuwa uchumi utaendelea kukua na mfumuko wa bei utabaki ndani ya lengo,” amesema Gavana Tutuba.
Kamati hiyo ilifanya mkutano wake Oktoba 7, 2026 ambapo ilifanya tathmini ya mazingira ya uchumi na kubaini kuwa hakuna sababu ya kubadilisha kiwango cha CBR kutoka asilimia 6.25 kilichotumika katika robo ya tatu ya mwaka 2026, iliyomalizika Septemba.
Gavana Tutuba amesema, kuendelea na kiwango hicho kunatarajiwa kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei, na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea katika mazingira yanayofaa.
Akizungumzia mwenendo wa uchumi wa dunia, Gavana Tutuba amesema, Kamati imeendelea kufuatilia kwa karibu athari za migogoro inayoendelea katika Mashariki ya Kati, ambayo imeendelea kuathiri masoko ya dunia, hususan mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa mafuta na mbolea.
Amesema, hali hiyo imechangia ongezeko la bei za baadhi ya bidhaa katika masoko ya dunia, huku bei ya mafuta ikiendelea kuwa juu na katika siku za hivi karibuni kufikia zaidi ya dola 100 za Marekani kwa pipa.
Gavana Tutuba amesema, mwenendo huo unaweza kuongeza gharama za uzalishaji na usafirishaji, hali ambayo inaweza kuwa na athari katika bei za bidhaa na huduma katika nchi mbalimbali, ikiwamo Tanzania.
Aidha, amesema migogoro hiyo imechangia matarajio ya kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia mwaka 2026 ikilinganishwa na mwaka 2025.
Amesema, Benki ya Dunia imefanya marekebisho ya makadirio yake ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2026 kutoka asilimia 2.9 hadi asilimia 2.5.
“Kwa kiasi kikubwa, mwenendo wa uchumi wa dunia unaendelea kutegemea namna mgogoro wa Mashariki ya Kati utakavyoendelea. Ikiwa utamalizika mapema, kuna uwezekano wa hali ya ukuaji wa uchumi wa dunia kurejea na kuwa nzuri zaidi,”amesema.
Gavana Tutuba amesema, ongezeko la bei za mafuta katika masoko ya dunia limeendelea kuongeza shinikizo la mfumuko wa bei duniani, huku Shirika la Fedha Duniani (IMF) likikadiria kuwa mfumuko wa bei duniani unaweza kufikia zaidi ya asilimia nne mwaka 2026.
Kutokana na mazingira hayo, Gavana Tutuba amesema, benki kuu nyingi duniani zimeendelea kuwa makini katika utekelezaji wa sera za fedha, huku baadhi zikisitisha hatua za kupunguza viwango vya riba na nyingine zikichukua msimamo wa kusubiri ili kutathmini mwenendo wa uchumi.
Amesema, Tanzania pia imeamua kuendelea na kiwango cha CBR cha asilimia 6.25 baada ya Kamati kutathmini hali hiyo na kuona kuwa kiwango hicho bado kinaendana na mazingira ya uchumi wa ndani.
Gavana Tutuba pia amesema, Kamati imebaini kuwa bei ya dhahabu katika masoko ya dunia imeendelea kuwa juu na inatarajiwa kubaki katika viwango vinavyosaidia kuongeza mapato yatokanayo na mauzo ya dhahabu nje ya nchi.
Amesema, hali hiyo inatarajiwa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa fedha za kigeni nchini na kusaidia ustahimilivu wa Shilingi ya Tanzania katika mazingira ya sasa ya uchumi wa dunia.
Akizungumzia mwenendo wa uchumi wa ndani, Gavana Tutuba amesema, Kamati imefanya tathmini ya taarifa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (OCGS).
Amesema, taasisi hizo zimekamilisha zoezi la kubadili mwaka wa msingi unaotumika katika kukokotoa Pato la Taifa (GDP), hatua inayolenga kuboresha uhalisia na usahihi wa takwimu za uchumi.
Kwa upande wa Tanzania Bara, amesema mwaka wa msingi umebadilishwa kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2019, hatua ambayo imeleta mabadiliko katika ukubwa wa Pato la Taifa.
Kwa mujibu wa takwimu hizo mpya, Pato la Taifa la Tanzania Bara kwa mwaka 2025 limefikia takriban Shilingi trilioni 234.1, sawa na dola za Marekani bilioni 90.3, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 203.07 zilizokuwa zimekadiriwa kwa kutumia mwaka wa msingi wa 2015.
Kwa upande wa Zanzibar amesema, Pato la Taifa limefikia Shilingi trilioni 9.24, sawa na dola za Marekani bilioni 3.6, kutoka takriban Shilingi trilioni 7.03 sawa na dola za Marekani bilioni 2.3, zilizokuwa zikikokotolewa kwa kutumia mwaka wa msingi wa 2015.
Gavana Tutuba amesema, maboresho hayo ya takwimu yana umuhimu katika kutoa picha sahihi zaidi ya ukubwa na muundo wa uchumi wa Tanzania, hivyo kusaidia Serikali na wadau wengine kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kiuchumi.
Amesema, NBS na OCGS zinaendelea kuboresha mifumo ya takwimu na kuwezesha maandalizi ya takwimu za kitaifa kwa kuzingatia mbinu na viwango vinavyokubalika kimataifa.
Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kukutana tena Januari 6, 2027 ambapo Januari 6, 2027 taarifa ya Riba ya Benki Kuu (CBR) itatangazwa kwa robo ya kwanza ya mwaka huo.
Tags
Benki Kuu ya Tanzania
Breaking News
Habari
Riba ya Benki Kuu (CBR)
Uchumi wa Tanzania
Uchumi wa Zanzibar
