NA GODFREY NNKO
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeyataka majeshi ya ulinzi na usalama nchini kuimarisha uelewa kuhusu miliki ubunifu ili kulinda bunifu zinazozalishwa na taasisi hizo, kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zake, pamoja na kutumia fursa za ubunifu kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 12, 2026 na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa wakati akifungua mafunzo kuhusu miliki ubunifu kwa majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika mkoani Morogoro.Bw. Nyaisa amesema, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea maafisa wa majeshi uelewa kuhusu aina mbalimbali za miliki ubunifu zinazoweza kulindwa kisheria, zikiwemo alama za biashara na huduma, hataza za uvumbuzi, maumbo bunifu na aina nyingine za haki za miliki ubunifu.
Amesema, ushiriki wa majeshi katika mafunzo hayo unaonesha kuwa, pamoja na kutekeleza majukumu ya msingi ya kulinda mipaka ya nchi, raia, mali zao, amani na utulivu, taasisi hizo pia zina nafasi muhimu katika kukuza uchumi kupitia uzalishaji mali, biashara, uwekezaji na ubunifu wenye tija.
“Warsha hii itaangazia umuhimu na mchango wa miliki ubunifu katika taasisi za majeshi nchini, ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza. Tutaangalia namna bunifu zinavyoweza kusajiliwa na kulindwa, pamoja na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na huduma zinazotolewa na taasisi hizi zinatambulika na kulindwa kisheria,” amesema Bw. Nyaisa.
Bw. Nyaisa amesema, uelewa kuhusu miliki ubunifu utaziwezesha taasisi hizo kutambua thamani ya bunifu zinazozalishwa na kuhakikisha haki zake zinalindwa dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa.
Amesema, hatua hiyo itasaidia pia kuongeza matumizi ya bunifu katika kuboresha bidhaa na huduma, kuimarisha utambulisho wa bidhaa sokoni na kufungua fursa zaidi za kibiashara na uwekezaji.
Aidha, ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuleta mabadiliko katika namna taasisi za majeshi zinavyotengeneza na kuwasilisha bidhaa zao kwa watumiaji, hususan katika masuala ya ufungashaji, uwekaji wa lebo na uchaguzi wa majina ya bidhaa.
UELEWA HUU NI MUHIMU KWA MAJESHI
Amesema, kupitia uelewa huo, taasisi hizo zitaweza kuboresha namna zinavyotambulisha bidhaa zake na kuhakikisha alama na majina yanayotumika yanazingatia taratibu za kisheria za usajili na ulinzi wa miliki ubunifu.
Bw. Nyaisa amepongeza hatua zinazochukuliwa na majeshi katika kupanua shughuli zake za uzalishaji na utoaji wa huduma kwa umma, akisema mabadiliko hayo yanaonesha kuwa taasisi hizo zina mchango unaozidi majukumu yake ya kawaida ya kiusalama.
Amesema, bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na taasisi hizo, zikiwemo zinazopatikana kupitia shughuli za Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Magereza, zinaonesha umuhimu wa kutoa elimu ya miliki ubunifu ili kuongeza thamani ya bidhaa hizo na kuimarisha ushindani wake sokoni.
Katika hatua nyingine, Bw. Nyaisa ameipongeza Mzinga Corporation kwa kusajili na kulinda kisheria ubunifu wa kifaa kinachotumia pilipili kuwafukuza tembo bila kusababisha madhara kwa binadamu na mazingira, kinachojulikana kama Pepper Thunder Flash Device.
Amesema, hatua hiyo ni mfano mzuri wa namna taasisi zinavyoweza kutambua thamani ya ubunifu wake na kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha unapata ulinzi unaostahili.
HONGERENI SANA MZINGA COOPERATION
“Kipekee, niwapongeze Mzinga Corporation kwa kuchukua hatua ya kulinda ubunifu wao kisheria. Mfano huu unaonesha umuhimu wa taasisi kutambua thamani ya bunifu zinazozalishwa na kuhakikisha zinapata ulinzi unaostahili,” amesema Bw. Nyaisa.
Ameeleza kuwa, kulinda bunifu kisheria ni hatua muhimu katika kuhakikisha taasisi zinaendelea kunufaika na kazi za ubunifu zinazozalishwa na wataalamu wake, huku zikichochea uendelezaji wa teknolojia na matumizi ya maarifa katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Magereza Makao Makuu, Kitila Kitandu, ameishukuru BRELA kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema taasisi za majeshi hazijihusishi na majukumu ya kiusalama pekee, bali pia uzalishaji wa bidhaa na ubunifu wa teknolojia mbalimbali.
Kitandu amesema, mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa taasisi hizo kupata maarifa yatakayozisaidia kuboresha shughuli zake za uzalishaji mali na kuhakikisha bunifu zinazotokana na kazi za wataalamu wake zinatambuliwa na kulindwa kisheria.
JKT: ELIMU YA MILIKI BUNIFU NI MUHIMU
Naye Mkurugenzi wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi JKT, Kanali Ephraim Kituhile amesema kuwa, Jeshi la Kujenga Taifa, kwa mfano linajihusisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, sambamba na majukumu yake ya malezi ya vijana na ulinzi.
Pia, amesema elimu kuhusu miliki ubunifu itasaidia kuongeza ufanisi katika shughuli hizo na kutoa fursa ya kupiga hatua zaidi katika kuboresha bidhaa na huduma zinazozalishwa na taasisi za majeshi.
“Tunashukuru sana kwa nafasi hii. Kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa, tunajihusisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kupitia kilimo, uvuvi na ufugaji. Kupitia fursa hii, tunatarajia kwenda hatua mbele zaidi katika kuboresha shughuli zetu,” amesema.
Ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya BRELA na taasisi za majeshi ni muhimu katika kuhakikisha bunifu zinazozalishwa ndani ya taasisi hizo zinapata ulinzi unaostahili, huku bidhaa zake zikiendelea kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya watumiaji.
Mafunzo hayo yanaweka msisitizo katika umuhimu wa taasisi za umma kutambua miliki ubunifu kama nyenzo ya kulinda haki za wabunifu, kuongeza thamani ya bidhaa, kuboresha huduma na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
BRELA inasisitiza kuwa, kuimarisha usajili na ulinzi wa miliki ubunifu, taasisi za majeshi zinaweza kuongeza manufaa ya bunifu zake, kuimarisha utambulisho wa bidhaa zake na kuchangia zaidi katika jitihada za taifa za kukuza uzalishaji, biashara na uwekezaji.


