NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imesema itaanza kufanya Operesheni ya kukamata gari zinazosafirisha maiti ambazo zinahusishwa kusafirisha dawa za kulevya nchini.
Hayo yamebainishwa Septemba 29, 2926, jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu ya oparesheni iliyofanyika nchini kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.
Alisema, Katika Oparesheni waliyoifanya katika mikoa 14 wamebaini uwepo wa maiti zinazosafirshwa hasa kwenda Kanda ya Kaskazini kuhusika kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi.
“Sasa tunatangaza rasmi tutazikamata maiti zote zitakazohusika na usafirishwaji wa dawa hizo pamoja na magari na watu watakaobainika na jambo hilo tutawakamata na kutahifisha magari hayo,” amesema.
Ameongeza kuwa, katika Oparesheni hiyo iliyofanyika kwa kipindi hicho cha miezi mitatu wamefanikiwa kukamata kilogramu 18,078.41 katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro,Arusha, Mororgoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Hata hivyo amesema, mikoa ya Morogoro na Tabora imekuwa kinara katika Kilimo cha zao la bangi na hatua mbalimbali zinaendelea ili kudhibiti zao hilo kwenye mikoa hiyo.
Lyimo amesema pia, Oparesheni hiyo hiyo wamebaini pikipiki kutumika zaidi katika kusafirisha bangi na wamekamata pikipiki 40, Bajaji moja, magari nane yaliyohusishwa na kusafirisha dawa hizo.
Amesema magari hayo ni pamoja na Toyota Harrier yenye namba T. 878 ASJ, Toyota Land Cruiser namba T. 234 BUR, Toyota IST namba T215 DCJ Toyota Noah namba T. 231 AWP, Toyota Alphard namba T. 870 EDE na Toyota Discovery.
Gari lingine lililokamatwa ni basi la Kampuni ya Ratco lenye namba T. 443 likisafirisha bunda 238 zenye uzito wa kilogramu 125.33 likitokea Tanga kwenda Dar es Salaam.
Pia, amesema katika kipindi hicho wamewakamata raia wa kigeni sita akiwemo raia wawili wa Afrika Kusini wakiwa na gramu 65.8 za bangi, raia wa Kenya mmoja akiwa na gramu 3.89 za mirungi, raia wa Nigeria mmoja akiwa na gramu 4.6 za bangi, na raia wa Uturuki mmoja akiwa na gramu 1.87 za skanka.
DCEA, imewataka wananchi kutoa kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Tags
Dawa za Kulevya Tanzania
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
