NA GODFREY NNKO
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetenga Shilingi trilioni 1.06 kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.6 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 916.7 zilizotengwa mwaka uliotangulia, huku wanafunzi wasiopungua 300,000 wakitarajiwa kunufaika na mikopo na programu mbalimbali za ufadhili.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia akizungumza na wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari nchini (hawapo pichani) Oktoba 12, 2026 katika kikao hicho kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.Aidha, HESLB imeeleza kuwa, ongezeko la uwekezaji katika ufadhili wa wanafunzi, maboresho ya mifumo ya kidijitali na kuimarika kwa ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa majukumu yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia ameyasema hayo Jumatatu, Oktoba 12, 2026 katika Hoteli ya KingJada iliyopo Morocco Square jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, taasisi hiyo imeendelea kupanua wigo wa ufadhili ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata elimu ya juu na mafunzo ya ngazi ya stashahada, sambamba na kuimarisha uendelevu wa mfuko.
Dkt. Kiwia amesema, katika kipindi hicho, HESLB imebadilika kutoka taasisi iliyolenga zaidi kutoa mikopo na kuwa taasisi inayosimamia mnyororo mzima wa ufadhili wa wanafunzi, kuanzia hatua ya maombi, uchambuzi na upangaji wa mikopo hadi malipo, huduma kwa wateja na urejeshaji wa fedha.
Amesema, hatua hizo zimewezekana kutokana na ushirikiano kati ya Serikali, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti, watumishi, vyuo vya elimu ya juu, wanafunzi, waajiri na wadau wengine wanaohusika katika mnyororo wa utoaji na urejeshaji wa mikopo.
Amesisitiza kuwa, mafanikio ya HESLB hayapaswi kupimwa kwa kiasi cha fedha kilichotolewa pekee, bali pia kwa idadi ya vijana wanaopata fursa ya kusoma, wahitimu wanaojiunga na soko la ajira na mchango wa elimu katika kuboresha maisha ya wananchi na maendeleo ya taifa.
Bajeti ya ufadhili yazidi kuongezeka
Akifafanua mwenendo wa uwekezaji katika elimu ya juu, Dkt. Kiwia amesema, Serikali imeendelea kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo na ruzuku, hatua inayowezesha kupanuka kwa idadi ya wanafunzi wanaopata ufadhili.
Pia, amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026, HESLB ilitumia Shilingi bilioni 916.7 kuwahudumia wanafunzi 289,932, huku bajeti ya mwaka wa masomo 2026/2027 ikipanda hadi Shilingi trilioni 1.06.
Ongezeko hilo la asilimia 15.6 amesema, linaonesha dhamira ya kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa Watanzania wenye sifa na mahitaji ya kifedha.
Dkt. Kiwia amesema, HESLB ilitangaza awamu ya kwanza ya upangaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027 Jumamosi, Oktoba 10, 2026, ambapo jumla ya wanafunzi 165,775 walipangiwa ufadhili wenye thamani ya Shilingi bilioni 535.7.
Ufadhili huo unahusisha wanafunzi wa shahada ya awali, stashahada, wanafunzi wanaoendelea na masomo pamoja na wanufaika wa programu ya Samia Scholarship waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali nchini.
Katika kundi la wanafunzi wapya wa shahada ya awali, wanafunzi 74,769 walipangiwa mikopo yenye thamani ya Sh246.88 bilioni.
Wengine 8,538 wa ngazi ya stashahada walipangiwa mikopo ya Shilingi bilioni 22.9 huku wanafunzi 873 wakipangiwa ruzuku ya Shilingi bilioni 4.5 kupitia Samia Scholarship.
Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, wanafunzi 79,115 walipangiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 252.4.
Aidha, wanafunzi 1,554 wa stashahada walipangiwa mikopo ya Shilingi bilioni 3.8, huku wanufaika 926 wa Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Shilingi bilioni 5.1.
Dkt. Kiwia amesema, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanaendelea na masomo yao bila kukatizwa na changamoto za kifedha.
Ufadhili wa stashahada na sayansi waongezwa
Amesema, HESLB imeendelea kupanua ufadhili katika ngazi ya stashahada ili kuwapa vijana fursa ya kupata ujuzi wa kitaaluma unaohitajika katika soko la ajira na shughuli za uzalishaji.
Vilevile, amefafanua kuwa, katika mwaka wa masomo 2026/2027, wanafunzi 24,978 wanatarajiwa kugharimiwa katika ngazi hiyo wakiwemo wanafunzi wapya 14,000.
Amesema, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada ulianza mwaka wa masomo 2023/2024, ikiwa ni hatua ya kupanua fursa za ufadhili zaidi ya ngazi ya shahada ya awali.
Katika kipindi hicho, HESLB pia iliongeza kiwango cha fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa shahada ya awali kutoka Shilingi 8,500 hadi Shilingi 10,000 kwa siku.
Pia, kwa upande wa ufadhili wa wanafunzi wenye ufaulu wa juu, hasa katika maeneo yanayochochea maendeleo ya taifa, Dkt. Kiwia amesema, Samia Scholarship imeendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi hizo.
Ameeleza kuwa, programu hiyo ilianzishwa mwaka wa masomo 2022/2023 na kuwafadhili wanafunzi 636, huku mwaka wa masomo 2024/2025 ikipanuliwa ili kuwajumuisha wanafunzi 80 wa shahada ya uzamili.
Kwa mwaka wa masomo 2026/2027, wanafunzi 2,738 wanatarajiwa kunufaika na Samia Scholarship katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) wakiwemo wanafunzi wapya 1,000.
Amesema, upanuzi huo unaonesha umuhimu wa kuwekeza katika elimu na mafunzo yanayowaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa sasa na wa baadaye.
HESLB yajipanga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Akizungumzia mwelekeo wa baadaye, Dkt. Kiwia amesema, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni sehemu ya juhudi za kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga mfumo bora na jumuishi wa elimu na mafunzo.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, dira hiyo inaweka lengo la angalau asilimia 25 ya Watanzania kupata elimu ya juu ifikapo mwaka 2050, jambo linalohitaji kupanua fursa za udahili, ufadhili na upatikanaji wa huduma za elimu.
Amesema, HESLB itaendelea kubuni njia mpya za kugharimia elimu, kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi na kutumia mifumo ya kidijitali ili kuhudumia idadi kubwa zaidi ya wanafunzi kwa ufanisi.
Dkt. Kiwia amesisitiza kuwa, mikopo itaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanafunzi wenye sifa kupata elimu ya juu, hasa wale ambao familia zao haziwezi kumudu gharama zote za masomo.
Makusanyo ya mikopo yafikia Shilingi trilioni 1.91
Katika eneo la urejeshaji wa mikopo, Dkt. Kiwia amesema, HESLB imepiga hatua katika ukusanyaji wa fedha zinazorejeshwa na wanufaika waliomaliza masomo, hali inayosaidia kuongeza uwezo wa mfuko kugharimia wanafunzi wengine.
Amesema, kuanzia mwaka wa fedha 2005/2006 hadi Juni 2026, HESLB ilikuwa imekusanya jumla ya Shilingi trilioni 1.91 kati ya Shilingi trilioni 2.77 za mikopo iliyofikia wakati wa kurejeshwa, sawa na ufanisi wa ukusanyaji wa asilimia 69.
Amebainisha kuwa, makusanyo yameendelea kuongezeka katika miaka ya karibuni. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, HESLB ilikusanya takribani Shilingi bilioni 177, huku makusanyo ya mwaka 2024/2025 yakifikia Shilingi bilioni 194.
Hata hivyo, mafanikio makubwa zaidi yalirekodiwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo HESLB ilikusanya Shilingi bilioni 235.5 kati ya lengo la Shilingi bilioni 220, sawa na asilimia 107 ya lengo lililowekwa.
Dkt. Kiwia amesema, kiwango hicho ndicho kikubwa zaidi cha makusanyo ya mikopo kuwahi kurekodiwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Amesema, mafanikio hayo yamechangiwa na mikakati mbalimbali ya ukusanyaji, ushirikiano na taasisi za kimkakati pamoja na kampeni za kuhamasisha wanufaika kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo.
Miongoni mwa kampeni hizo ni Fichua na Kiduchu Fresh Tunasonga, ambayo ilizinduliwa Aprili 2026 kwa lengo la kuwawezesha wanufaika wenye kipato kidogo kuanza kurejesha mikopo yao kwa kiasi kinachoendana na uwezo wao.
Amesema, HESLB inatarajia kuendelea kuongeza makusanyo katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku lengo likiwa kukusanya zaidi ya Sh220 bilioni.
Hata hivyo, amebainisha kuwa, bado kuna changamoto ya wanufaika ambao hawajaanza kurejesha mikopo yao, huku kiasi cha takribani Shilingi bilioni 800 kikihusishwa na wanufaika wanaodaiwa na ambao hawajajitokeza kurejesha fedha hizo.
Amesema, changamoto hiyo inahitaji juhudi zaidi za kuwafikia wahitimu, hususan wale wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi, ambao wakati mwingine ni vigumu kuwatambua na kufuatilia uwezo wao wa kurejesha mikopo.
Dkt. Kiwia amesisitiza kuwa, urejeshaji wa mikopo si suala la kisheria na kifedha pekee, bali pia ni wajibu wa kijamii unaowezesha vijana wengine kupata fursa ya elimu.
“Mnufaika anaporejesha mkopo wake, anaongeza fursa kwa kijana mwingine mwenye uhitaji kupata elimu,” amesema Dkt. Kiwira.
Mifumo ya kidijitali kuboresha huduma
Katika eneo la teknolojia, Dkt. Kiwia amesema, HESLB imeendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha maombi, upangaji wa mikopo, malipo na mawasiliano kati ya taasisi hiyo na wanufaika.
Amesema, hatua hizo zinalenga kupunguza matumizi ya karatasi, kupunguza muda wa kushughulikia maombi na malalamiko, na kuhakikisha wanafunzi wanapata taarifa kwa wakati.
Miongoni mwa mifumo inayotumika ni Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo (OLAMS), Akaunti Maalum ya Mwombaji (SIPA), programu ya HESLB kwa simu janja na Mfumo wa Usimamizi wa Malipo ya Ada (DiDiS).
Kupitia mifumo hiyo, waombaji na wanufaika wanaweza kufuatilia taarifa zao, kufanya baadhi ya taratibu za usajili na uthibitishaji kwa njia ya kidijitali na kurahisisha mchakato wa malipo.
Aidha, HESLB imeanzisha matumizi ya mifumo saidizi inayotumia akili unde, ikiwemo Bwanaboom na Bibiboom, kwa lengo la kutoa majibu ya haraka kuhusu huduma za mikopo na masuala yanayohusiana na ufadhili.
Dkt. Kiwia amesema, matumizi ya teknolojia hayalengi kuwa na mifumo ya kisasa pekee, bali kuhakikisha huduma zinakuwa za haraka, sahihi, zinazofikika kwa urahisi na zinazozingatia mahitaji ya wateja.
Ameongeza kuwa, taasisi hiyo itaendelea kuimarisha huduma kupitia ofisi za kanda, kituo cha huduma kwa wateja na mifumo ya kidijitali ili kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi wakati wa kuomba au kufuatilia mikopo yao.
HESBL yatambuliwa kwa viwango vya kimataifa
Akieleza mafanikio ya kiutendaji, Dkt. Kiwia amesema, HESLB imeendelea kuimarisha mifumo yake ya usimamizi, uwajibikaji na utoaji wa huduma, hatua iliyoisaidia kupata utambuzi katika maeneo mbalimbali ya utendaji.
Amesema, taasisi hiyo imepata uthibitisho wa kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015 katika usimamizi wa mifumo ya ubora, na kusisitiza kuwa jukumu lililopo ni kuhakikisha viwango hivyo vinaendelea kuzingatiwa katika utoaji wa huduma.
Pia, amesema HESLB imehitimisha Mpango Mkakati wa Tano wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 kwa utekelezaji wa asilimia 82.
Katika kipindi hicho, taasisi imepata hati safi za ukaguzi, huku asilimia 80 ya hoja za ukaguzi wa hesabu zikifungwa. Vilevile, asilimia 72 ya waombaji waliokidhi vigezo walipangiwa mikopo.
Amesema, HESLB imezindua Mpango Mkakati wa Sita wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031, unaolenga kuibadili taasisi hiyo kuwa Mfuko wa Taifa wa Kugharimia Wanafunzi wenye wigo mpana zaidi wa fursa za ufadhili.
Mpango huo, amdeleza utazingatia ubunifu, weledi, uwajibikaji, kujali wateja na usawa katika utoaji wa huduma, sambamba na kuimarisha uwezo wa taasisi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wanafunzi.
Ushirikiano na taasisi mbalimbali waimarishwa
Dkt. Kiwia amesema, HESLB imeendelea kushirikiana na taasisi za serikali na sekta nyingine katika kuendeleza programu maalumu za ufadhili.
Ametoa mfano wa ushirikiano uliorasimishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika mwaka wa masomo 2026/2027 kwa ajili ya kufadhili wanafunzi wa shahada za uzamili kupitia programu ya Mwalimu Julius K. Nyerere Memorial Masters’ Degree Scholarship.
Pia ametaja ushirikiano na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), unaolenga kufadhili wanafunzi wanaoishi katika eneo la hifadhi na wanaokwenda kusomea taaluma zinazohusiana na uhifadhi.
Amesema, ushirikiano huo unaonesha umuhimu wa kuhusisha taasisi mbalimbali katika kupanua fursa za elimu na kuhakikisha programu za ufadhili zinakidhi mahitaji ya kitaifa katika sekta muhimu za maendeleo.
Katika kuimarisha uratibu wa huduma, HESLB pia imeendelea kufanya vikao na maafisa mikopo wa vyuo. Septemba 2026, zaidi ya maafisa mikopo 200 walikutana na Menejimenti ya HESLB katika kikao cha 15, kwa lengo la kujadili changamoto zilizojitokeza katika mwaka wa masomo 2025/2026 na kupendekeza maboresho ya utoaji wa huduma na matumizi ya mifumo ya TEHAMA.
Changamoto bado zipo
Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Kiwia amesema, HESLB bado inakabiliwa na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuboresha zaidi huduma kwa wanafunzi na kuimarisha uendelevu wa Mfuko.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na hitaji la kuboresha mawasiliano na wanafunzi, vyuo na wadau wengine ili kuhakikisha taarifa muhimu zinawafikia kwa wakati.
Pia amesema, usahihi wa taarifa zinazowasilishwa na waombaji na vyuo ni muhimu katika kuhakikisha mikopo inapangwa kwa wanafunzi wanaostahili bila ucheleweshaji usio wa lazima.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amebainisha kuwa, HESLB imekuwa ikifanya juhudi za kuunganisha mifumo yake na mifumo ya vyuo, lakini baadhi ya vyuo bado havijakamilisha mchakato huo ulioanza zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Katika eneo la urejeshaji, amesema kipaumbele ni kuimarisha uwezo wa kuwafikia wahitimu wote wanaodaiwa, hasa walio katika sekta isiyo rasmi, ili kuongeza makusanyo na kuhakikisha fedha za mikopo zinarejea kwenye mzunguko wa ufadhili.
Amesema, kadri idadi ya wanafunzi wanaohitaji ufadhili inavyoongezeka, ndivyo umuhimu wa urejeshaji wa mikopo unavyoongezeka, kwa kuwa uendelevu wa Mfuko unategemea uwezo wa kuunganisha fedha za Serikali na marejesho ya wanufaika.
Wanafunzi wahimizwa kutumia njia za mawasiliano
Dkt. Kiwia amewahimiza wanafunzi na wanufaika kutumia njia rasmi za mawasiliano za HESLB wanapohitaji ufafanuzi au wanapokumbana na changamoto katika huduma.
Amesema, taasisi hiyo ina Dawati la Huduma kwa Wateja kupitia namba 0736 66 55 33, Mfumo Jumuishi wa Wateja (DOCEP) kupitia namba 0736 66 55 34 na huduma ya WhatsApp kwa ujumbe kupitia namba 0739 66 55 33.
Aidha, wanufaika wanaweza kupata majibu kupitia chatbot ya Bwanaboom inayopatikana kwenye tovuti ya HESLB, www.heslb.go.tz.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, HESLB pia inapokea malalamiko na mrejesho kupitia mfumo wa e-Mrejesho, akieleza kuwa malalamiko ya wananchi ni sehemu muhimu ya kubaini maeneo yenye mapungufu na kuboresha utoaji wa huduma.
Amewahimiza wateja ambao hawajaridhishwa na huduma kuwasilisha mrejesho wao kupitia njia hizo ili hatua stahiki zichukuliwe kwa uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Wahariri watakiwa kuelimisha Watanzania
Wakati huo huo, Dkt. Kiwia ameviomba vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na HESLB katika kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mikopo, ruzuku, masharti ya ufadhili na wajibu wa wanufaika.
Amesema, vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kuunganisha taasisi hiyo na umma kwa kuwasaidia wanafunzi, wazazi, walezi, waajiri na wanufaika kuelewa taratibu za huduma na umuhimu wa kurejesha mikopo.
Amesisitiza kuwa, HESLB itaendelea kuboresha mifumo yake ili iwe ya kidijitali zaidi, inayowajibika, inayosikiliza mahitaji ya wananchi na yenye uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya wanafunzi bila kushusha ubora wa huduma.
Dkt. Kiwia amesema, mafanikio ya mfuko yanategemea ushirikiano wa wadau wote, kwa kuwa kila mkopo unaotolewa ni uwekezaji katika maisha ya kijana, huku kila mkopo unaorejeshwa kwa wakati ukiwa fursa ya kumwezesha mwanafunzi mwingine kupata elimu.
Amesema, HESLB itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kupanua fursa za elimu ya juu na kuchangia katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.


