Zan Timiza ETF yaorodheshwa DSE baada ya kukusanya Sh Bilioni 9.46 mauzo ya awali

NA DIRAMAKINI

SOKO la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeorodhesha Mfuko wa Uwekezaji wa Zan Timiza (ETF), hatua inayoongeza bidhaa za uwekezaji katika soko la mitaji na kutoa fursa zaidi kwa wananchi kushiriki katika uwekezaji kwa lengo la kujenga utajiri.
Mfuko huo, unaosimamiwa na Zan Securities Limited, umeorodheshwa jana baada ya kufanikiwa kukusanya Sh bilioni 9.46 kupitia mauzo ya awali, ikilinganishwa na lengo la Sh bilioni tano, sawa na asilimia 189.3 ya lengo lililowekwa.

Mafanikio hayo yanaonesha mwitikio mkubwa wa wawekezaji kwa fursa za uwekezaji zinazopatikana kwa urahisi.

Akizungumza katika hafla ya kuorodhesha mfuko huo iliyofanyika jana, Kamishna wa Malipo ya Nje katika Wizara ya Fedha, Rished Bade amesema, mafanikio hayo ni hatua muhimu inayodhihirisha uwezo wa kukusanya rasilimali za ndani na kuimarisha soko la mitaji nchini.

"Hatua hii itapanua fursa za uwekezaji na kuimarisha nafasi ya masoko ya mitaji katika kukusanya fedha za muda mrefu kwa ajili ya maendeleo ya taifa, kwani ni ubunifu muhimu unaowawezesha wawekezaji kushiriki katika soko rasmi la mitaji.”
Mfuko huo ni wa kwanza wa aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki unaowekeza katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), maarufu kama Fund of Funds (FoF), kuorodheshwa katika soko la hisa la taifa.

Katika mauzo ya awali, wawekezaji wadogo walichangia asilimia 99 ya ununuzi wa vipande vya mfuko huo, huku wawekezaji wa taasisi na makampuni wakichangia asilimia moja.

Bade amesema, kuorodheshwa kwa mfuko huo kunasaidia kutekeleza malengo ya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza, kuongeza ukwasi sokoni na kukusanya mitaji ya ndani.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Zan Securities, Raphael Masumbuko amesema, kuorodheshwa kwa mfuko huo ni hatua muhimu katika kupanua ushiriki wa wananchi katika soko la mitaji, hususan kwa kufanya fursa za uwekezaji zipatikane kwa urahisi zaidi kwa Watanzania wa kawaida.

“Ufanisi wa mauzo haya haupimwi tu kwa kiasi cha fedha kilichokusanywa, bali pia kwa idadi na aina ya wawekezaji walioshiriki, hususan Watanzania wa kawaida,” amesema.

Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa Soko wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Exaut Julius amesema, mafanikio hayo yanaonesha kuendelea kuwepo kwa imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika soko la mitaji, pamoja na kuwepo kwa mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na mamlaka hiyo.

Amesema, hatua hiyo itachangia kuongeza ukwasi katika soko la hisa na kupanua ushiriki wa wawekezaji, kwa kuwa inawawezesha kutambua thamani halisi ya vipande vyao na kujua thamani halisi ya uwekezaji wao.
"Kwa hiyo, kuorodheshwa kwa mfuko huu kunatarajiwa kuongeza kiwango cha biashara na ukwasi katika soko,” amesema.

Naye Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa DSE, Emmanuel Nyalali amesema, kuorodheshwa kwa mfuko huo ni hatua nyingine katika kuongeza aina mbalimbali za bidhaa za uwekezaji zinazopatikana sokoni, akibainisha kuwa soko la hisa endelevu linapaswa kutoa fursa zaidi ya hisa na hati fungani pekee.

Amesema, upanuzi wa bidhaa za uwekezaji unaweza kuwawezesha wananchi wenye uwezo tofauti wa kifedha kushiriki katika kujenga utajiri na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kupanua fursa za uwekezaji kunapaswa kwenda sambamba na elimu ya fedha, upatikanaji wa taarifa sahihi na uelewa wa wazi kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza katika uwekezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here