Jihan Dimack: Mtanzania wa kwanza kutwaa Miss Grand Duniani

NA DIRAMAKINI

MWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya urembo ya Miss Grand International 2026, Jihan Dimack ametwaa taji la mashindano hayo baada ya ushindani mkali uliohusisha warembo kutoka mataifa mbalimbali duniani, katika hatua iliyovuta hisia za mashabiki wa urembo ndani na nje ya Tanzania.
Jihan amepata ushindi huo leo Oktoba 10, 2026 jijini Bangkok, Thailand ambapo ushindi huo umeiweka Tanzania katika nafasi ya kujivunia katika jukwaa la kimataifa la urembo.

Aidha, Jihan ametumia nafasi yake kuwasilisha ujumbe unaosisitiza umuhimu wa amani, upendo, umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali.

Katika kipengele cha kuwasilisha ujumbe kuhusu amani duniani, Jihan ameeleza kuwa, migogoro na machafuko yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya dunia yamesababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha, familia, makazi na matumaini yao ya maisha bora.

Amesisitiza kuwa, kila mtoto anastahili kukua katika mazingira salama na yenye amani, badala ya kuishi katika hofu inayosababishwa na vita na migogoro.

Akieleza uzoefu wake kama Mtanzania, Jihan amesema, anajivunia kuzaliwa katika nchi inayotambuliwa kwa misingi ya amani, upendo na umoja, akibainisha kuwa Watanzania wanaamini watu wanaweza kuishi na kufanya kazi pamoja bila kujali tofauti za asili, dini au mila zao.

Jihan ameeleza kuwa, misingi hiyo ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Tanzania na mfano wa namna jamii zenye tofauti za kijamii na kiutamaduni zinavyoweza kujenga maisha ya pamoja kwa kuheshimiana na kuvumiliana.

Pia, amesisitiza kuwa amani haipaswi kutafsiriwa kama udhaifu, bali ni ishara ya ujasiri unaowezesha watu kukubali tofauti zao na kutambua ubinadamu unaowaunganisha.

Amesema kuwa, licha ya tofauti zilizopo miongoni mwa watu, tofauti hizo hazipaswi kuwa sababu ya uhasama, bali zinapaswa kuwa fursa ya kuimarisha mshikamano na kujenga dunia yenye ushirikiano.

“Bila kujali tofauti zetu, sisi si maadui, bali sisi ni wamoja,” amdsema Jihan katika ujumbe wake aliouwasilisha jukwaani.

Aidha, amewataka watu duniani kote kuweka ubinadamu mbele kwa kuimarisha upendo, kueneza amani na kujenga mazingira ambayo kila mtu anaweza kuishi bila hofu ya kupoteza maisha au kuvunjika kwa matumaini yake.
Ujumbe wake umelenga kuhamasisha jamii kutambua kuwa, amani ni jukumu la kila mtu, linalohitaji uvumilivu, kuheshimiana na utayari wa kuishi pamoja licha ya tofauti za kiimani, kikabila na kitamaduni.

Vilevile, kwa Tanzania ushindi wa Jihan unaambatana na ujumbe unaosisitiza umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa amani na umoja, huku ukiwakumbusha Watanzania nafasi yao katika kuhamasisha mshikamano na maelewano katika jamii.

Jihan amehitimisha ujumbe wake kwa wito kwa watu wote, bila kujali wanakotoka, kuruhusu ubinadamu kutawala mioyo yao na kuendeleza juhudi za kueneza amani na upendo duniani.

Ushiriki wake katika mashindano hayo umeunganisha jukwaa la urembo na ujumbe wa kijamii, ukionesha namna washiriki wanavyoweza kutumia nafasi zao kuhamasisha masuala yanayogusa maisha ya watu na mustakabali wa dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here