NA GODFREY NNKO
UMOJA wa Mabenki Tanzania (TBA) umeipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) unaolenga kuimarisha utulivu wa uchumi na kuongeza imani katika mfumo wa fedha nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Oktoba 8, 2026 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam na Kaimu Mwenyekiti wa TBA ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank, Bi. Isabela Maganga katika mkutano wa kutangaza Kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa Robo ya Nne 2026.
Akizungumza mbele ya viongozi wa sekta ya fedha na waandishi wa habari, Mwakilishi huyo wa TBA amempongeza Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba pamoja na uongozi wa benki hiyo kwa uamuzi huo.
Amesema, uamuzi huo unaonesha dhamira ya Benki Kuu katika kuhakikisha uchumi unaendelea kuwa imara katika kipindi ambacho mazingira ya kiuchumi duniani yanaendelea kukabiliwa na kutokuwa na uhakika.
Bi.Maganga amesema, uamuzi huo si tamko la sera pekee, bali unaakisi kiwango cha imani na uimara wa uchumi wa Tanzania, huku sekta ya fedha ikiwa na nafasi muhimu katika kutafsiri hatua za sera kuwa fursa za kukuza huduma za kifedha na uchumi kwa ujumla.
“Katika dunia yenye kutokuwa na uhakika, Benki Kuu imechagua utulivu. Hili si tamko la sera pekee, bali linaonesha imani na uimara wa uchumi wetu,” amesema Mwakilishi huyo wa TBA.
Amesema, TBA na wadau wa sekta ya fedha kwa ujumla wanaunga mkono kikamilifu hatua zinazochukuliwa na BoT, na wamejipanga kushirikiana na Benki Kuu katika kutekeleza sera hizo kwa vitendo.
Pia, amefafanua kuwa, mabenki yataendelea kuboresha na kupanua huduma za kifedha kwa Watanzania, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma hizo, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha, TBA imeupongeza uongozi wa BoT kwa ushirikiano na msaada unaoendelea kutolewa kwa sekta ya fedha, ikisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Benki Kuu na taasisi za fedha ni muhimu katika kujenga sekta imara na yenye uwezo wa kuhimili changamoto za kiuchumi.
TBA imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano usioyumba kwa BoT na kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya fedha katika kuhakikisha hatua za sera zinatafsiriwa kuwa ongezeko la huduma za kifedha, ukuaji wa sekta ya benki na maendeleo endelevu ya uchumi wa Tanzania.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Gavana Emmanuel Tuba amesema, kamati hiyo imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6.25 katika robo ya nne ya mwaka 2026, kinachomalizika Desemba, 2026.
Amesema, hatua hiyo inalenga kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi nchini.
Pia, amewaeleza washiriki wa mkutano huo ambao umeangazia masuala mbalimbali ya kiuchumi kuwa, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kukua kwa kasi na kufikia wastani wa asilimia 32.5 katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba, 2026.
Gavana Tutuba amesema, ukuaji huo umewezesha wafanyabiashara, kampuni na wananchi kupata fedha kupitia benki kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Aidha, amesema sekta ya benki imeendelea kuwa imara na yenye uwezo wa kustahimili changamoto, ikiwa na mitaji, ukwasi na faida ya kutosha. Mikopo chechefu imeendelea kuwa chini ya kiwango kinachokubalika, ikiwa asilimia 2.5 Agosti 2026, dhidi ya ukomo wa asilimia 5.
Vilevile, amesema akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha, ikiwa zaidi ya dola bilioni 6, kiasi kinachotosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa takribani miezi 4.3.
Gavana Tuba amesema, mkutano ujao wa Kamati ya Sera ya Fedha utafanyika Januari 6, 2027, ambapo uamuzi wa CBR kwa robo ya kwanza ya mwaka 2027 utafanywa, huku uamuzi huo ukitarajiwa kutangazwa Januari 7, 2027.
Tags
Benki za Tanzania
Benki Kuu ya Tanzania
Habari
Habari za Leo
Riba ya Benki Kuu (CBR)
Uchumi wa Tanzania
Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA)

