NA MARY GWERA,
Mahakama-Zanzibar
WASHIRIKI wa Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) tarehe 07 Oktoba, 2026 wamefanya ziara za utalii katika Maeneo mbalimbali Visiwani Zanzibar.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, (mwenye fulana ya kijivu), Jaji Mkuu wa Kenya, Mhe. Martha Koome (mwenye gauni ya kijani) pamoja na Washiriki wengine wakiwa katika Shamba la Viungo Kizimbani Zanzibar walipotembelea shamba hilo tarehe 07 Oktoba, 2026.
Safari ya ziara hizo ilianzia katika Hoteli ya Verde majira ya saa 3 Asubuhi ukiwa umegawanyika katika maeneo yapatayo manne.
Baadhi ya Majaji Wakuu wa Ukanda huo pamoja na Washiriki wengine wa Mkutano huo waliongozwa na Mwenyeji wao ambaye ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla katika Kisiwa cha Kihistoria kijulikanacho kwa jina la ‘Prison Island’ na Fukwe iitwayo Nakupenda ambapo walipata kufahamu historia mbalimbali.
Kundi lingine lilielekea katika Shamba la Serikali la Viungo-Kizimbani (Kizimbani Spice Farm) pamoja na Nungwi likiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Jaji Mkuu wa Kenya, Mhe. Martha Koome pamoja na Viongozi na Wadau wengine wa Mahakama wa Ukanda huo.
Katika maeneo hayo washiriki wamejionea Viungo mbalimbali vikiwa bado shambani katika maumbo ya mimea/miti. Viungo hivyo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinatumika majumbani katika mapishi na vingine vikitumika kama tiba; viungo hivyo ni pamoja na Mdalasini, hiriki, tangawizi, manjano, karafuu, Vanila, Mchaichai, mbilimbi, pilipili manga, nazi, kukumanga na vingine.
Kadhalika, katika eneo la Nungwi Visiwani humo, Washiriki hao walitembelea eneo la Bwawa la kufugia Kasa na Samaki ambapo walipata fursa ya kujionea viumbe hao ambao wanafurahisha machoni kutokana na uzuri na upekee wake pamoja na Wanyama wengine waliopo katika eneo hilo wakiwemo Kobe, Pundamilia, Mamba, ndege aina ya Kasuku, digidigi, Ngedere na Nungunungu.
Aidha, kundi lingine la Majaji Wakuu na Washiriki wengine wa Mkutano wa SEACJF wametembelea Mji Mkongwe (Stone Town) Zanzibar ambapo wamejionea Kanisa la Minara Miwili, Beit al-Ajaib ambalo ni jengo la kihistoria na la kifahari lililopo visiwani humo.
Ziara hizo za Kitalii zimeonesha kukuna nyoyo za wengi kufuatia vitu na historia walivyoona kwa macho na kusikia.
Sehemu ya eneo la Shamba la Viungo-Kizimbani Zanzibar.
Mwongoza Watalii kutoka Shamba la Viungo Kizimbani Zanzibar, Bw. Said Rashid akitoa maelezo ya aina ya Viungo mbalimbali vilivyopo katika shamba hilo wakati sehemu ya Majaji Wakuu na Washiriki wengine wa Mkutano wa SEACJF walipotembelea eneo hilo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (mwenye kofia nyeusi) akiwa katika utalii pamoja na sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Kusini na Mashariki wa Afrika (SEACJF) wakiwa katika Kisiwa cha Prison Island-Zanzibar.
Usikivu makini kwa Mwongoza Watalii (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa maelezo ya Viungo mbalimbali vilivyopo katika Shamba la Viungo-Kizimbani Zanzibar.
Utalii ukiendelea ndani ya Shamba la Serikali la Viungo lililopo Kizimbani Zanzibar tarehe 07 Oktoba, 2026.
Picha ya pamoja mara baada ya kuhitimisha ziara ya Kitalii katika Shamba la Viungo la Kizimbani-Zanzibar tarehe 07 Oktoba, 2026. Wa nne kushoto ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, wa tano kushoto ni Jaji Mkuu wa Kenya, Mhe. Martha Koome, wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu pamoja na washiriki wengine waliotembelea Shamba hilo.Burudani baada ya Utalii katika Shamba la Viungo Kizimbani Zanzibar.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akiwaunga mkono wajasiriamali wadogo waliopo eneo la Shamba hilo. Mwenye fulana nyeusi ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Bi. Winifrida Mokaya.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu pamoja na wengine wakinunua viungo kwa wajasiriamali wadogo waliopo katika eneo la Shamba la Viungo Kizimbani-Zanzibar.
Muonekano wa baadhi ya Kasa na Samaki wakiwa kwenye Bwawa eneo la Nungwi Zanzibar.
Zoezi la kuwalisha Kasa likiendelea.
Kobe.
Nungunungu.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kushoto) pamoja na Mshiriki mwingine wa Mkutano wa SEACJF kwa pamoja wakiwalisha Ndege aina ya Kasuku wakati wa ziara ya kitalii iliyofanyika tarehe 07 Oktoba, 2026 Nungwi Visiwani Zanzibar.
Jaji Mkuu wa Kenya, Mhe. Martha Koome (mwenye gauni ya rangi ya kijani na nyeupe) akifurahia pamoja na wenzake walipotembelea Shamba la Viungo la Serikali lililopo Kizimbani Zanzibar.
Tags
George Mcheche Masaju
Habari
Kimataifa
Majaji katika Utalii
SEACJF Annual Conference 2026
Utalii Zanzibar


