MOROGORO-Serikali imevitaka vyombo vya habari kutumia nafasi yake kama kiungo kati ya Serikali na wananchi kwa kufuatilia na kuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, pamoja na kutoa nafasi kwa wananchi kuelewa, kushiriki na kutoa mrejesho kuhusu utekelezaji wa Sera hiyo.
Wito huo umetolewa na Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wahariri, waandishi wa habari na wamiliki wa mitandao ya kijamii, yaliyofanyika katika Hoteli ya Timeless mjini Morogoro, ambayo yalilenga kuwaongezea uelewa washiriki kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi na nafasi yao katika kuifikisha kwa umma.
Bw. Haraba alisema, mafanikio ya Sera hayaishii katika kuandaliwa na kuzinduliwa kwake, bali yanapimwa zaidi kupitia namna inavyotekelezwa, matokeo yanayopatikana na kiwango ambacho wananchi na wadau mbalimbali wanashiriki katika utekelezaji wake.
Alisema, katika hatua hiyo, vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kufuatilia utekelezaji wa Sera, kubaini maeneo yanayohitaji ufafanuzi, kuibua changamoto na kuhakikisha taarifa zinazohusu hatua za utekelezaji zinawafikia wananchi kwa wakati.
"Tunachofanya hapa ni kuwapa elimu na kuwaongezea ujuzi ili mtakaporejea katika vyombo vyenu vya habari muweze kutumia kalamu zenu kuelimisha umma kuhusu Sera hii,” alisema Bw. Haraba.
Aliongeza kuwa, uelewa wa wananchi kuhusu Sera unapaswa kwenda sambamba na kufahamu wajibu wao, fursa zinazopatikana pamoja na namna wanavyoweza kushiriki na kunufaika na utekelezaji wake.
Aidha, alisema vyombo vya habari vinaweza kusaidia kujenga mfumo wa mawasiliano wa pande mbili kwa kuwasilisha kwa wananchi taarifa kutoka Serikalini na, wakati huo huo, kuifikishia Serikali mrejesho wa wananchi kuhusu utekelezaji wa Sera kwa kuwa taarifa za utekelezaji zinapowasilishwa kwa lugha inayoeleweka na kuhusishwa na maisha halisi ya wananchi, huongeza uelewa na kuwapa fursa ya kufuatilia namna Sera inavyotekelezwa katika maeneo yao.
Alieleza kuwa, mrejesho huo ni muhimu katika kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji na kusaidia Serikali na wadau wengine kuchukua hatua zinazostahili.
Naye Mwenyekiti wa Wadau wa Mitandao ya Kijamii waliohudhuria mafunzo hayo, Bw. Mathias Canal, alisema mafunzo hayo yamekuwa na matokeo chanya kwa washiriki, hasa katika kuongeza uelewa ambao utawasaidia kuhabarisha umma kuhusu Sera hiyo.
Alisema, Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ina fursa nyingi ambazo wanahabari wanaweza kuzifikisha kwa umma ili wananchi waweze kuzifahamu na kuzitumia.
“Tunashukuru Wizara ya Fedha kwa mafunzo haya. Hakika kila mmoja wetu amepata mwanga mpya kuhusu Sera hii, hasa katika maeneo yanayowiana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Bw. Canal.
Tags
Habari
Mafunzo kwa Waandishi
Mafunzo kwa Wahariri
Sera ya Taifa ya Ugavi
Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi 2025
Wizara ya Fedha Tanzania











