DOHA-Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha bajeti inayozingatia jinsia (Gender-Responsive Budgeting-GRB) kama nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo jumuishi ya miundombinu.
Mhe. Balozi Omar amebainisha hayo wakati akielezea uzoefu wa Tanzania katika kuandaa bajeti inayozingatia misingi ya kijinsia wakati wa mjadala ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB), kando ya Mkutano wake Mkuu wa Mwaka 2026, uliofanyika Doha nchini Qatar.
Balozi Omar katika mdahalo huo uliobeba kauli mbiu ya “ufunguaji wa fursa za miundombinu inayozingatia jinsia”, alieleza kuwa, Tanzania imekuwa ikitekeleza bajeti inayozingatia jinsia tangu mwishoni mwa miaka ya 1990.
Alisisitiza kuwa, msingi wa mipango ya Serikali ni kutoa kipaumbele kwa watu, jambo linalohitaji uelewa mpana wa demografia ya nchi.
Alisema kuwa,Tanzania hutumia sensa ya watu inayofanyika kila baada ya miaka 10 ili kubaini mwelekeo wa ukuaji wa idadi ya watu na muundo wake, jambo ambalo ni muhimu katika kupanga na kutekeleza bajeti.
Mhe. Balozi Omar alifafanua kuwa,bajeti inayozingatia jinsia siyo kutenga bajeti tofauti kwa ajili ya wanawake, bali ni kuhakikisha kuwa rasilimali za umma zinapangwa, zinatengwa, na kutekelezwa kwa kuzingatia mahitaji mahususi ya jinsia zote.
Katika mwaka huu, Serikali imezindua taarifa ya bajeti ya kijinsia (gender budget statement) inayounganisha hali halisi ya kijinsia nchini na mipango ya bajeti na kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji ili kulenga maeneo mahususi ya kijinsia.
“Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, ikiwemo kuboresha upatikanaji wa takwimu zilizogawanywa kijinsia (disaggregated data) na kuimarisha uchambuzi wa kijinsia,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na wadau wa maendeleo kama UN Women na AIIB, akibainisha kuwa ushirikiano huo unaleta utaalamu wa kiufundi, ushahidi katika mipango, na uzoefu wa kimataifa.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali lazima ichukue uongozi na umiliki wa mchakato huo ili kuwajibika kwa wananchi huku akionya dhidi ya mifumo sambamba inayoweza kuletwa na wafadhili, akisisitiza kuwa misaada inapaswa kuingia ndani ya mifumo iliyopo ya Serikali ili kuepuka gharama zisizo za lazima.
Amesema Mkakati wa Tanzania unalenga kuimarisha mnyororo wa thamani kuanzia kubaini pengo la kijinsia, kuweka vipaumbele vya kitaifa, kupanga bajeti, kubuni miradi, hadi kupima matokeo ya utekelezaji wake.
Akizungumzia manufaa ambayo Tanzania inatarajia kupata kupitia Benki hiyo, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Serikali itaitumia Benki hiyo kutekeleza baadhi ya miradi yake ya maendeleo ya kimkakati, ikiwemo miradi ya reli, nishati na teknolojia za kidijitali, ambapo mazungumzo kati ya Serikali na Benki hiyo yanaendelea.
Tanzania iliidhinishwa kuwa mwanachama wa AIIB mwaka 2023 na kukamilisha rasmi mchakato wa uanachama mwaka 2025. Tanzania ni miongoni mwa wanachama wasio wa kikanda (non-regional members), huku AIIB ikiwa na jumla ya wanachama 111 kwa sasa.
Tags
Bajeti inayozingatia Jinsia
Balozi Khamis Mussa Omary
Doha Qatar
Habari
Kimataifa
Wizara ya Fedha Tanzania







