Miaka 27 bila Mwalimu Nyerere: Sekta ya Maji yachangia mapambano dhidi ya ujinga, umasikini na maradhi

NA DIRAMAKINI

LEO ni kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni miaka 27 ya kumbukizi, na Sekta ya Maji katika kumbukizi hii inajipambanua kuwa moja ya wachangiaji wakubwa katika kutokomeza maadui watatu ambao Mwalimu Julius Nyerere alipambana nao kila kukicha yaani Ujinga, Umasikini na Maradhi.

MAJI YANAVYOONDOA UJINGA NA KULETA UTULIVU MASHULENI

Huduma ya maji inawafikia wananchi na kuondoa muda mwingi unaotumika kutafuta maji, na mashuleni kuleta utulivu kwa wanafunzi. Wanafunzi wanapata muda wa kusoma na kufaulu vizuri.

Pamoja na hilo, huduma imeondoa maradhi yaliyosababishwa na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama. Maji safi na salama yameokoa kiwango kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kutibu wananchi.

Kadhalika, maji yanatumika kusisimua huduma nyingine za uchumi na kuongeza ubora wa bidhaa mbalimbali, hivyo kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Maji ni injini ya uchumi kwa ujumla.

UPATIKANAJI WA MAJI WAONGEZEKA KUFIKIA ASILIMIA 85.2 VIJIJINI

Sekta ya Maji imeendelea kupata mafanikio katika maeneo mbalimbali muhimu, yakiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya maji kutokana na juhudi zinazoendelea za Serikali.

Hivi sasa upatikanaji wa huduma ya maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 83.0 mwaka 2024 hadi asilimia 85.2 mwaka 2025, na mijini huduma imeongezeka kutoka asilimia 91.6 hadi asilimia 92.5.

Pamoja na hilo, jumla ya vijiji 10,758 kati ya vijiji 12,333 vimefikiwa na huduma ya maji ya uhakika.

Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vilivyosalia 1,575, kwa lengo la kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma na kuhakikisha idadi kubwa ya wananchi wanafikiwa na maji safi na salama.

BAJETI YA SEKTA YA MAJI YAONGEZEKA HADI TRILIONI 1.12

Katika kuhakikisha miradi ya maji mijini na vijijini inatekelezwa kwa wakati na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi, Serikali imeongeza bajeti ya Sekta ya Maji kutoka Shilingi 898,276,453,000 hadi kufika Shilingi 1,120,194,614,000.

Hatua hii itawezesha kutekeleza miradi 1,188 midogo na miwili mikubwa. Fedha hizo zitatumika kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji pamoja na ubora wake.

Katika mwaka 2026/27, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 400 kati ya vijiji 1,575 ambavyo havina huduma ya maji.
Hatua hii inalenga kuongeza kasi ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama, ambapo jumla ya wananchi 1,440,256 watanufaika.

MIRADI MIKUBWA YA KIMKAKATI KIDUNDA NA FARKWA

Serikali imeanza na kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji na upatikanaji wa maji.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Kidunda, lenye thamani ya Shilingi bilioni 329.47 na utekelezaji wake hadi Septemba 2026 umefika asilimia 65.7.

Ujenzi wa Bwawa la Farkwa, kwa ajili ya kuongeza upatikanaji na uhakika wa huduma ya maji katika Jiji la Dodoma na maeneo yanayolizunguka.

Mradi huo una thamani ya takribani Shilingi bilioni 312. Bwawa hilo linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 400.

Mradi wa maji kutoka Mto Rufiji kwenda Dar es Salaam na Pwani ambapo Wizara ya Maji imekamilisha upembuzi yakinifu. Lengo ni kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.

GRIDI YA TAIFA YA MAJI NA MRADI WA NYANGAO

Miradi ya Gridi ya Taifa ya Maji ni mpango wa kimkakati wa kitaifa wa muda mrefu unaolenga kuunganisha vyanzo vikuu vya maji nchini kupitia mtandao wa usafirishaji wa maji kwa wingi.

Mpango huo unahusisha vyanzo vikuu kama Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, Mto Rufiji, Mto Ruvu, Mto Pangani, Mto Wami, Mto Kagera, Mto Malagarasi, Mto Great Ruaha pamoja na mabwawa makubwa ya kimkakati kama vile Bwawa la Julius Nyerere, Bwawa la Kidunda na Bwawa la Farkwa.

Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji vijijini. Miongoni mwa miradi ni mradi wa maji Ruangwa, Lindi na Nachingwea unaotekelezwa kwa kutoa maji Mto Nyangao kwenda Wilaya tatu za Lindi, Ruangwa na Nachingwea kwa gharama ya Shilingi bilioni 119.56.

Mradi unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha kupeleka maji kwenye vijiji 29. Hadi mwezi Septemba 2026, utekelezaji umefika asilimia 77.

MATARAJIO YA MBELE

Tanzania tunaweza kusema safari tulipotoka ni mbali na tunapoenda ni karibu zaidi katika huduma ya maji. Serikali inaendelea kuhakikisha vijiji vyote 1,575 visivyokuwa na huduma ya maji vinapata huduma hiyo.
Pia, utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kukamilisha Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji ikiwa ni nyenzo muhimu ya kupanga maendeleo ya rasilimali za maji kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here