Mitihani Kidato cha Nne 2026: NECTA yasajili watahiniwa 667,040

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesema, jumla ya watahiniwa 667,040 wamesajiliwa kufanya mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2026 ambapo kati ya 664,085 ni watahiniwa wa shule na 22,955 ni watahiniwa wa kujitegemea.
Pia, kati yao wavulana ni 297,309 sawa na asilimia 46.16 na wasichana 297,776 sawa na asilimia 53.84 na watahiniwa wa shule 910 ni wenye uhitaji maalum.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Ally Mohammed ameyasema hayo leo Oktoba 18, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea kuhusu maandalizi ya mitihani hiyo itakayofanyika Oktoba 19, 2026 hadi Novemba 6, 2026.

Vilevile, baraza hilo limeonya kuwa, halitasita kufuta matokeo ya mtahiniwa yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu katika Mtihani wa Kidato cha Nne wa mwaka 2026.

Katibu Mtendaji huyo amesema, maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika yakiwemo usambazaji wa karatasi za mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka nyingine muhimu katika halmashauri na manispaa zote za Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema, kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimekamilisha maandalizi ya vituo, kutoa mafunzo kwa wasimamizi na kuweka mikakati ya kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.

Profesa Mohamed amesema, usalama wa vituo umeimarishwa ili kuhakikisha mtihani unafanyika kwa utulivu.

Amesisitiza kuwa, wasimamizi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa umakini, uadilifu na weledi, kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya mitihani, ili kuhakikisha kila mtahiniwa anapata haki yake na kufanya mtihani ndani ya muda uliopangwa.

Amesema, watahiniwa wenye mahitaji maalum wanapaswa kupatiwa mazingira yanayowawezesha kufanya mtihani kwa usawa yakiwemo maandishi ya nukta nundu kwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu.

Aidha, watahiniwa hao wanapaswa kuongezewa muda wa dakika 20 kwa kila saa katika somo la Hisabati ya Msingi na dakika 10 kwa kila saa katika masomo mengine, kwa mujibu wa mwongozo wa baraza hilo.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Ally Mohammed.

Baraza limewataka wamiliki wa shule kutokuingilia majukumu ya wasimamizi wakati wa mtihani, huku wakuu wa shule wakitakiwa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na NECTA na kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mitihani.

Wakati huo huo, baraza limesema halitasita kufuta kituo chochote cha mtihani endapo litathibitisha kuwepo kwa matukio au vitendo vinavyohatarisha usalama wa mtihani.

Hatua hiyo inalenga kulinda uadilifu wa mchakato wa mitihani na kuhakikisha matokeo yanayotolewa yanaakisi uwezo halisi wa watahiniwa.

NECTA pia imezitaka jamii na wananchi kuhakikisha watu wasiohusika hawaingii katika maeneo ya shule yanayotumika kama vituo vya mitihani katika kipindi chote cha mtihani, ili kuwawezesha watahiniwa kufanya mitihani yao katika mazingira ya amani na utulivu.

Profesa Mohamed ameongeza kuwa, Mtihani wa Kidato cha Nne una umuhimu mkubwa kwa kuwa hupima umahiri wa wanafunzi katika masomo waliyosoma kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne.

Amesema, matokeo yake pia hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano na kozi mbalimbali za kitaaluma zikiwalemo afya, kilimo na ufundi kote nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here