MSF yaimarisha unyonyeshaji Liwale kupitia wahudumu jamii

LINDI-Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeendelea kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kunyonyesha kupitia Wahudumu wa Afya ya Jamii, hususan katika eneo la Kimambi lililopo Wilaya ya Liwale Mkoa wa Lindi.
Akizungumza wakati wa mjadala uliofanyika Kimambi kuadhimisha Siku ya Kunyonyesha Duniani, Afisa Uhamasishaji wa Afya wa MSF, Shangwe amewahimiza wazazi kuanza kunyonyesha watoto wao ndani ya saa moja baada ya kujifungua, akieleza kuwa hatua hii husaidia kuimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto.

Shangwe pia amewahimiza wazazi kuepuka kuwapa watoto wachanga wenye umri wa miezi 0 hadi 6 maziwa ya ng’ombe, akisisitiza kuwa, maziwa ya mama yana virutubisho muhimu kwa ukuaji na afya ya mtoto.

Amesema, kunyonyesha pia kuna manufaa kwa mama, ikiwa ni pamoja na kupunguza hatari ya baadhi ya matatizo ya kiafya kama vile saratani ya matiti, huku kunyonyesha mara kwa mara pia kukisaidia katika kupanga nafasi kati ya uzazi na mwingine.

“Kunyonyesha si jukumu la mama pekee, bali kunahitaji ushiriki wa familia nzima, wakiwemo baba, ambao wanapaswa kuhakikisha mama anapata muda wa kutosha wa kupumzika na mazingira yenye usaidizi ili aweze kumhudumia mtoto wake,”amesema.

Mohammed Abdallah Mtende, Muuguzi-Mkunga na Msimamizi wa Zahanati ya Kimambi amesema, Wahudumu wa Afya ya Jamii wamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu unyonyeshaji pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto.

Amesema, awali baadhi ya wanawake, hususan katika jamii za wafugaji, hawakuwa wakiwapa watoto wao maziwa ya mama mara tu baada ya kujifungua, badala yake waliwapa maziwa ya ng’ombe ili waweze kuendelea na kazi za nyumbani, jambo ambalo alisema lilichangia changamoto mbalimbali za kiafya miongoni mwa watoto.

Mtende amesema, elimu ya afya inayotolewa na wahudumu wa Afya ngazi ya jamii imechangia kuboresha tabia kutafuta huduma za afya, hususan miongoni mwa wanawake wajawazito na walezi wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Amesema, sasa watu wengi zaidi wanahudhuria vipindi vya elimu ya afya na kutafuta taarifa kuhusu huduma zinazopatikana, zikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto katika vituo vya afya.

Mussa Mshamu Litako, Mhudumu wa Afya ya Jamii kutoka Kijiji cha Kimambi ambaye amefanya kazi hiyo kwa takribani miaka minne tangu MSF ilipoanza kutoa huduma katika eneo hilo, alisema elimu ya afya imeleta mabadiliko makubwa katika matumizi ya huduma za afya.

Amesema, alipoanza kufanya kazi hiyo, kulikuwa na upungufu wa uelewa katika jamii. Baadhi ya wazazi hawakuwa wakiwapeleka watoto wao katika vituo vya afya walipougua, huku baadhi ya wanawake wakichelewa kuanza huduma za kliniki za wajawazito.

Wengine walifika kwa mara ya kwanza kliniki wakiwa tayari na ujauzito wa miezi sita, saba au hata minane.

“Kujiandikisha katika huduma za kliniki za wajawazito mapema ni muhimu kwa sababu huwawezesha wahudumu wa afya kutambua na kudhibiti mapema matatizo yanayoweza kujitokeza, kama vile shinikizo la juu la damu, upungufu wa damu na maambukizi, hivyo kuwawezesha wanawake kupata matibabu au rufaa kwa wakati inapohitajika,”ameeleza.

Amepongeza MSF kwa kuwezesha utoaji wa elimu ya afya kupitia Wahudumu wa Afya ya Jamii na kuwahusisha viongozi wa kaya, hususan wanaume.

Amesema, njia hii imesaidia kukabiliana na changamoto zilizokuwepo awali, ambapo Wahudumu wa Afya ya Jamii walikuwa wakikumbana na ugumu wa kutoa elimu ya afya moja kwa moja kwa wanawake bila msaada na ushiriki wa viongozi wa kaya.

Kwa mujibu wa Litako, jamii sasa inaendelea kuamini zaidi huduma za afya, huku kituo hicho kikipokea wastani wa watoto 150 hadi 160 katika siku za chanjo, ambazo hufanyika mara moja kwa mwezi.

Hadija Lipinga mkazi wa Kimambi na mama wa mapacha ameishukuru MSF kwa msaada alioupata baada ya kujifungua watoto wake wakiwa na umri wa ujauzito wa miezi saba, huku kila mmoja akiwa na uzito wa takribani kilo moja, katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale.

Hadija amesema, watoto wake walikaa hospitalini kwa takribani mwezi mmoja, ambapo alipata msaada na elimu kutoka kwa wataalamu, hususan kuhusu namna sahihi ya kuwanyonyesha watoto waliozaliwa kabla ya wakati.

Amesema, elimu hiyo ilimsaidia kuelewa mbinu sahihi za kunyonyesha na umuhimu wa maziwa ya mama kabla ya kuanza kuwapa watoto vyakula vingine.

Huko Kimambi, idadi ya akina mama wanaohudhuria kliniki za wajawazito kwa wakati, kutafuta huduma za afya ya mama na mtoto na kufuata kanuni bora za unyonyeshaji inaendelea kuongezeka. Maendeleo haya yameungwa mkono na ushirikiano.

Wahudumu wa Afya ya Jamii. Kupitia ushirikiano huo, uelewa wa jamii umeongezeka, huku upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya mama na mtoto ukiendelea kuimarika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here