Naibu Waziri Khadija Salum asisitiza vijana kuelimishwa kuhusu madhara ya Dawa za Kulevya

ZANZIBAR- Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Khadija Salum Ali amesisitiza umuhimu wa kuwaelimisha vijana kuhusu madhara ya Dawa za Kulevya ili kuwajengea uelewa wa kujikinga na matumizi ya dawa hizo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Mhe. Khadija ameyasema hayo Oktoba, 2026 alipofungua Semina Elekezi ya Madhara ya Dawa za Kulevya kwa Vijana, iliyofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi, Saateni, Zanzibar.

Amesema kuwa, dawa za kulevya ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri afya, kuvunjika kwa familia kupitia migogoro, kuchochea uhalifu, ukatili na udhalilishaji, kuathiri maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii, hususan vijana ambao ni nguvu kazi muhimu katika maendeleo ya Zanzibar.

Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu na uhamasishaji ili kuwasaidia vijana kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao.
Aidha, Mhe. Khadija ameeleza kuwa, mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa Serikali, wazazi na walezi, taasisi za elimu, Viongozi wa dini,viongozi wa jamii pamoja na vijana wenyewe.

Naibu Waziri huyo amewahimiza vijana kutumia fursa zinazopatikana katika elimu, ujasiriamali na shughuli mbalimbali za maendeleo ili kujenga maisha bora na yenye tija.
Ameongeza kuwa, jamii inapaswa kuacha mazoea na kuepuka muhali katika kupambana na dawa za kulevya ambazo zinapelekea udhalilishaji na ukatili, bali jamii izidishe ushirikiano katika kuimarisha malezi, kutoa ushauri na msaada kwa vijana wanaokabiliwa na changamoto zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kutumia dawa za kulevya.

Aidha, ameahidi ushirikiano kati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar katika kuendeleza juhudi za kutoa elimu, kupunguza udhalilishaji unaotokana na sababu ya dawa za kulevya pamoja na kuimarisha kinga na kulinda ustawi wa vijana katika Jamii.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ufunguzi wa semina hiyo ni Kamishna Mkuu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanali Burhani Zuberi Nassoro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg, Khatib Mwadin Khatib, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii. Ndg, Siti Abasi Ali, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii wa Wizara hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here