NHC yaunganisha benki tisa kufungua fursa umiliki wa nyumba kwa Watanzania

 DAR ES SALAAM- Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah amesema, ushirikiano kati ya shirika na taasisi za fedha ni nyenzo muhimu katika kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba bora na za kisasa.

Akizungumza katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja kilichofanyika leo, Oktoba 16, 2026, katika mradi wa Kawe 711, Dar es Salaam, Bw. Abdallah amesema NHC inaendelea kuimarisha ushirikiano na benki mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya nyumba kwa wananchi, wakiwemo Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).

“Tunataka kutimiza ndoto ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba. Hili linawezekana kupitia ushirikiano na mabenki yanayotoa mikopo kwa Watanzania waliopo nchini na wanaoishi nje ya nchi,” amesema.

Katika hafla hiyo, benki na taasisi tisa za fedha ambazo ni CRDB Bank, NMB, NBC, Azania Bank, Absa Bank, Equity Bank, Bank of Africa, Tanzania Commercial Bank (TCB) na First Housing Finance zimeungana na NHC kueleza fursa mbalimbali za mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi, wafanyabiashara, wawekezaji na Watanzania wanaoishi nje ya nchi.

Bw. Abdallah amesema, lengo la kuzikutanisha benki hizo na wananchi ni kuwawezesha wateja kupata taarifa za mikopo moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa fedha, kulinganisha masharti ya ukopeshaji na kufanya maamuzi sahihi kuhusu umiliki wa nyumba.

Akizungumza kwa niaba ya Azania Bank, Bw. Sampson Mahindi amesema benki hiyo imekuwa na ushirikiano na NHC kwa takribani miaka 15, ambapo imewezesha Watanzania wengi kumiliki nyumba katika miradi mbalimbali, ikiwemo Kawe na Iyumbu, Dodoma.
Ameeleza kuwa, Azania Bank inatoa mikopo ya nyumba yenye muda wa marejesho unaofikia miaka 25, huku baadhi ya miradi ikiwa na utaratibu maalumu wa riba ya asilimia 9, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa marejesho kwa wanunuzi wa nyumba.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Equity Bank amesema benki hiyo ina ushirikiano wa muda mrefu na NHC na uzoefu mkubwa katika utoaji wa mikopo ya nyumba. Ameeleza kuwa benki hiyo inaweza kutoa mkopo unaofikia Shilingi bilioni 3.5 kwa mkopaji mmoja, kulingana na vigezo vya ukopeshaji.

Naye Meneja wa Mikopo ya Nyumba wa TCB, Bi. Maria Mbuta, amesema benki hiyo inatoa mikopo inayozingatia mahitaji na uwezo wa kifedha wa mteja, ikiwemo mikopo ya kununua, kujenga na kukarabati nyumba.

Kwa upande wa Absa Bank, wawakilishi wake wameeleza kuwa benki hiyo inaweza kutoa mkopo unaofikia asilimia 90 ya bei ya nyumba, hadi Shilingi bilioni moja, huku ikitoa huduma maalumu za kifedha kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Mwakilishi wa First Housing Finance, Bi. Fausta Arnold, amesema taasisi hiyo imejikita katika utoaji wa mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi na wafanyabiashara, yenye muda wa marejesho unaofikia miaka 20.

Ameipongeza NHC kwa kujenga nyumba zenye ubora na kuwahimiza wananchi kutumia fursa za mikopo zinazopatikana.

Wawakilishi wa CRDB Bank, NMB, NBC na Bank of Africa pia wameungana na taasisi nyingine za fedha kuhamasisha wananchi kutumia huduma za mikopo ya nyumba, huku NMB ikieleza uwepo wa utaratibu wa marejesho unaoweza kuzingatia mzunguko wa mapato ya mteja.

MWEKEZAJI ATOA USHUHUDA, AWATAKA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Kezma Inc. Limited, Bw. Mablu Kiambali, ambaye tayari amenunua nyumba ya NHC, amewahamasisha Watanzania kuwekeza katika sekta ya nyumba, akieleza kuwa umiliki wa nyumba si kwa ajili ya makazi pekee, bali pia ni fursa ya kujenga uchumi kupitia upangishaji.

Amesema, nyumba inaweza kutumika kwa makazi binafsi au kupangishwa na kumwingizia mmiliki kipato cha ziada, hata akiwa ameajiriwa au anaishi nje ya nchi.
Ameipongeza NHC kwa kuendeleza miradi yenye ubora na kuwahimiza Watanzania kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta ya milki, badala ya kusubiri hadi watakapokuwa na fedha zote za kununua nyumba.

KAWE 711: MAKAZI YA KISASA YENYE FURSA ZA UWEKEZAJI

Akizungumzia mradi wa Kawe 711, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amesema mradi huo wenye nyumba 122 umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya maisha ya kisasa, ukiwa na huduma muhimu zikiwemo mifumo ya kuhifadhi maji, majenereta ya dharura, viwanja vya michezo na bwawa la kuogelea.

Amesema mradi huo upo takribani mita 50 kutoka Bahari ya Hindi, eneo ambalo linaongeza mvuto wa makazi hayo na fursa ya kukua kwa thamani ya nyumba katika siku zijazo.

“Kuna kumiliki nyumba, lakini kuna kumiliki nyumba katika eneo zuri. Thamani ya nyumba inategemea eneo ilipo, eneo ilipo na eneo ilipo,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa, NHC itaendelea kuendeleza miradi ya nyumba katika maeneo yenye miundombinu na mazingira bora, huku ikishirikiana na taasisi za fedha kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata fursa za kumiliki nyumba.

Ushiriki wa taasisi hizo tisa za fedha katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja umeonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya NHC na sekta ya fedha katika kupanua fursa za umiliki wa nyumba na uwekezaji nchini.

Kupitia ushirikiano huo, wananchi wanapata nafasi ya kuchagua huduma za mikopo zinazolingana na uwezo wao wa kifedha, huku NHC ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuongeza fursa za upatikanaji wa makazi bora kwa Watanzania.
Huna fedha zote za kununua nyumba? Haimaanishi huwezi kumiliki nyumba. Fursa za mikopo zipo, chukua hatua kutimiza ndoto yako!

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here