NA GODFREY NNKO
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Methusela Ntonda amezindua vitabu vya utalii na kamusi za lugha ya Kifaransa, Kiingereza, Kijapani, Kiitaliano na Kiswahili katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania, akisisitiza umuhimu wa machapisho katika kuhifadhi maarifa, kukuza utamaduni wa kusoma na kuitangaza nchi kimataifa.
Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 16, 2026 katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, ambapo maonesho hayo yameanza Oktoba 10 na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 18, mwaka huu.
Vitabu vya utalii vimechapishwa na kampuni za Mbiu na Elite, huku kamusi hizo zikichapishwa na APE Network kwa uwezeshaji kutoka Mfuko wa Utamaduni na Sanaa (TACAF).
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Ntonda amesema, maonesho ya vitabu ni jukwaa muhimu la kimataifa linalowaunganisha waandishi, wachapishaji, wasomaji, taasisi na wadau wengine kwa ajili ya kubadilishana maarifa, kutangaza machapisho na kuendeleza fursa za kibiashara.
Amesema, vitabu ni mtaji muhimu wa elimu, maarifa na ujuzi, unaochangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Pia, amebainisha kuwa, machapisho yana nafasi kubwa katika kuhifadhi historia, mila, desturi na maarifa ya wataalamu wa vizazi mbalimbali, huku yakirahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wanafunzi, watafiti na jamii kwa ujumla.
Bw. Ntonda amewahimiza waandishi na wachapishaji kuendelea kuandaa machapisho yanayokidhi mahitaji ya jamii, vikiwemo vitabu vya watoto, lugha, historia, utamaduni na sayansi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usomaji katika shule na vyuo, akieleza kuwa juhudi za makusudi zinahitajika kuwahamasisha watoto na vijana kujenga mazoea ya kusoma vitabu licha ya maendeleo ya teknolojia.
Kuhusu kamusi, amesema zina mchango mkubwa katika kuhifadhi lugha, kuimarisha mawasiliano na kukuza matumizi ya lugha katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, diplomasia, elimu na teknolojia.
Ameongeza kuwa, vitabu vya utalii ni nyenzo muhimu katika kuitangaza Tanzania, kwa kuwa vinatoa taarifa kuhusu vivutio vya nchi na kusaidia kufikisha ujumbe kwa wageni na masoko ya kimataifa.
TACAF YAWEZESHA MIKOPO SHILINGI BILIONI 2.36
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa (TACAF), Bi. Nyakaho Mahemba amesema, uandishi na tafsiri ni nyenzo muhimu katika kuhifadhi historia, mila, desturi na maadili ya Kitanzania.
Amesema, fasihi andishi huwezesha watu kuwasilisha mawazo, hisia, maarifa na uzoefu wao kupitia maandishi, huku ikichangia kujenga uzalendo, mshikamano na utambulisho wa taifa.
Bi. Mahemba amebainisha kuwa, fasihi andishi pia ni msingi wa uzalishaji wa kazi nyingine za sanaa, zikiwemo filamu, tamthilia na sanaa za maonesho, ambazo hutegemea miswada na maandishi yenye ubora.
Amesema, sekta hiyo haichangii maendeleo ya kiutamaduni pekee, bali pia hutengeneza ajira na fursa za kiuchumi kwa waandishi, wachapishaji na wasanii wengine.
Ameeleza kuwa, mfuko huo umetenga mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.36 kwa ajili ya kuwezesha miradi 104 ya fasihi andishi.
Uwezeshaji huo umesaidia kuboresha mashine za uchapishaji, miundombinu ya maduka ya vitabu na uzalishaji wa machapisho yanayotumiwa katika shule na vyuo.
Bi. Mahemba amewataka wadau na wananchi kuendelea kuthamini na kutumia Kiswahili kama nguzo muhimu ya utambulisho wa taifa, huku akihimiza uwekezaji zaidi katika uandishi, uchapishaji na tafsiri.
PATA YATAKA SERA YA TAIFA YA KUSOMA NA KUANDIKA
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji wa Vitabu Tanzania (PATA), Bw. Hermes Salla amesema, Tanzania imepiga hatua katika kuendeleza maonesho ya kimataifa ya vitabu na kukuza utamaduni wa kusoma katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesema, mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza elimu, utamaduni na uchumi.
Hata hivyo, amebainisha kuwa sekta ya uchapishaji inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo ukosefu wa sera jumuishi ya kusoma inayoweza kutoa mwongozo kwa taasisi za umma na binafsi.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali kuharakisha uandaaji wa sera ya taifa ya kusoma na kuandika ili kuimarisha hamasa ya kujifunza na kuweka mazingira bora kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya wizara inayosimamia utamaduni na Wizara ya Elimu ili kuhakikisha vitabu vinavyoandikwa nchini vinapata fursa ya kununuliwa na kutumiwa katika shule na taasisi za umma.
Aidha, ametoa wito kwa waandishi na wachapishaji wa ndani kushirikishwa kikamilifu katika maonesho ya kimataifa ili kupanua soko la machapisho ya Kitanzania, hususan fasihi ya Kiswahili.
Bw. Salla amesema, sekta ya uandishi na uchapishaji imeendelea kuwa chanzo cha ajira, ujasiriamali na mapato huku maonesho ya vitabu yakitoa fursa kwa wachapishaji wadogo na wakubwa kutangaza kazi zao na kujenga mitandao ya kibiashara.
VITABU VYA UTALII KULENGA MASOKO YA KIMATAIFA
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dkt. Jossam Mungure amesema, vitabu vilivyozinduliwa vimeandaliwa kwa lengo la kuitangaza Tanzania katika masoko mbalimbali ya kimataifa na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi.
Amesema, machapisho hayo yametolewa kwa lugha mbalimbali ili kuwafikia wasomaji wa mataifa tofauti na kuwapa taarifa kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Dkt. Mungure amesema, lengo ni kuchangia kufikiwa kwa azma ya Serikali ya kuvutia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya taasisi za utalii na wadau wa ndani na nje ya nchi ni muhimu katika kutangaza rasilimali za utalii na kufanikisha malengo yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi. Gertrude Ndaro ambaye ni Afisa Utamaduni Mkuu wa bodi hiyo amesema, vitabu hivyo vina taarifa kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Amesema, machapisho hayo yatasaidia kuitangaza Tanzania katika maeneo mbalimbali duniani, kuongeza uelewa kuhusu rasilimali za utalii na kuvutia wageni wengi zaidi.
Hata hivyo, uzinduzi wa vitabu hivyo unaweka msisitizo katika nafasi ya uandishi na uchapishaji kama nyenzo za kuendeleza elimu, kuhifadhi urithi wa taifa na kukuza utalii, huku maonesho hayo yakiendelea kuwa jukwaa la kuunganisha wadau wa sekta ya vitabu na kupanua fursa za biashara ndani na nje ya nchi.
Tags
Habari
Kamusi za Lugha
Maktaba Kuu ya Taifa
Maonesho ya Vitabu
Mfuko wa Utamaduni na Sanaa
Vitabu vya Utalii


