NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi limemkamata Faustine Zakaria ambaye ni kinyozi kwa tuhuma za kuharibu fedha halali za Tanzania, baada ya kuonekana katika picha mjongeo akifagia noti alizokuwa amezitawanya sakafuni pamoja na nywele zilizotokana na shughuli za unyoaji na uchafu mwingine ndani ya saluni yake.
Picha mjongeo hiyo, ambayo mtuhumiwa alirekodiwa kwa ridhaa yake huku akifahamu wazi kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria na baada ya kurekodi aliisambaza picha hizo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii Agosti 23, 2026, hatua iliyowezesha mamlaka za kisheria kufuatilia tukio hilo na kuchukua hatua stahiki.
"Jeshi la Polisi linakamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara baada ya taratibu za kiuchunguzi kukamilika.
"Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuheshimu, kulinda na kutunza fedha za Tanzania ambazo ni alama ya utambulisho na heshima ya taifa, kwa kuepuka vitendo vyote vya kuzidhalilisha au kuziharibu."

