Prof. Mkenda aiagiza MUST kutathmini ubunifu wa gesi ya Lusano

MBEYA-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameiagiza Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kuwasilisha ndani ya mwezi mmoja taarifa ya tathmini ya ubunifu wa kuzalisha gesi unaofanywa na mbunifu Lusano Luvanda, ili kubaini usalama, ufanisi na uwezekano wa teknolojia hiyo kutumika kibiashara.
Prof. Mkenda ametoa agizo hilo Oktoba 9, 2026, alipofanya ziara katika chuo hicho na kutembelea maeneo mbalimbali ya ubunifu wa wanafunzi na watafiti, ikiwemo teknolojia ya kuzalisha gesi ya haidrojeni kwa kutumia maji na malighafi zinazopatikana nchini.

Amesema, ubunifu huo unahitaji kufanyiwa tathmini ya kina na jopo la wanasayansi kutoka MUST pamoja na taasisi nyingine za elimu na utafiti, ili kuthibitisha usalama wa teknolojia hiyo, namna inavyofanya kazi na uwezekano wa kutumia gesi inayozalishwa kwa shughuli za kupikia na huduma nyingine.

Aidha, amesema tathmini hiyo inapaswa kuangalia gharama za uzalishaji wa gesi hiyo na kuzilinganisha na gharama za gesi inayotumika nchini, ambayo kwa kiasi kikubwa huagizwa kutoka nje, ili kubaini kama teknolojia hiyo inaweza kuwa mbadala wenye gharama nafuu.
Prof. Mkenda amesisitiza umuhimu wa kulinda haki miliki ya mbunifu huyo wakati tathmini na hatua za kuendeleza teknolojia hiyo zikiendelea, akieleza kuwa ubunifu wa Watanzania unapaswa kupewa nafasi ya kukua na kuendelezwa hadi kufikia hatua ya kuwa bidhaa inayoweza kutumika kibiashara.

Vilevile, ameitaka MUST kuhakikisha hatua za kusajili kampuni inayohusishwa na ubunifu huo ( Eco Flame clean Energy) zinafanyika mapema, ili endapo tathmini ya kisayansi itathibitisha usalama na ufanisi wa teknolojia hiyo, kampuni iweze kuanza uzalishaji na usambazaji wa gesi kwa taasisi zinazohitaji.

Amesema, Serikali iko tayari kusaidia kuwezesha tathmini ya kisayansi ya ubunifu huo, akibainisha kuwa teknolojia zitakazothibitishwa kuwa salama na zenye tija zinaweza kupewa kipaumbele katika taasisi za elimu, hususan maeneo yenye upatikanaji wa maji.
Mbunifu Lusano Luvanda amesoma nchini mwaka 2021 alihitimu kidato cha Nne katika shule ya Sekondari ya Serikali Forest iliyopo mkoani Mbeya na kujiunga na MUST mwaka 2022 kozi ya kilimo biashara na Teknolojia ambapo amehitimu diploma 2025

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here