NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametangaza mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kufuatia kukamilika kwa mazungumzo na maridhiano ya kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, hatua inayotamatisha rasmi mchakato wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar leo Oktoba 3,2026 Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kuweka wazi hatua zilizofikiwa katika kuunda Serikali hiyo ya maridhiano, kuanzia kusainiwa kwa makubaliano hadi kuteuliwa kwa viongozi mbalimbali kutoka pande zote mbili.
Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa, mchakato huo ulihusisha mambo makuu matatu, mosi ni makubaliano ya maridhiano.
Amesema, katika hatua hii CCM na ACT-Wazalendo zilisaini makubaliano ya pamoja ya kushirikiana katika kuunda serikali na kuendelea kujadili masuala mengine ya kitaifa.
Pili, ilikuwa ni uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais, ambapo baada ya kupokea jina kutoka ACT-Wazalendo, Rais Dkt. Mwinyi alimteua Mheshimiwa Othman Masud kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Tatu, ni Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Mawaziri, ambapo chama hicho kilipeleka majina ya wawakilishi wa viti maalum na nafasi nne za uwaziri zilizotengwa kwa mujibu wa katiba, ambazo sasa zimejazwa kupitia uteuzi rasmi uliofanyika.
Ameeleza kuwa, ACT-Wazalendo iliwasilisha majina manne kwa uteuzi wa mawaziri, kwa kuzingatia nafasi nne za chama hicho katika Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Katiba.
Rais Dkt. Mwinyi amesema, masuala ya Mipango yamehamishiwa Ofisi ya Rais, Ikulu. Kufuatia mabadiliko hayo, iliyokuwa Wizara ya Fedha na Mipango sasa itaitwa Wizara ya Fedha, ikiendelea kuongozwa na Mhe. Dkt. Juma Malik Akil.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema sekta ya Kazi imehamishiwa iliyokuwa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji, ambayo sasa itaitwa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji. Kufuatia mabadiliko hayo, iliyokuwa Wizara ya Kazi na Uwekezaji sasa itaitwa Wizara ya Uwekezaji, ikiendelea kuongozwa na Mhe. Shariff Ali Shariff.
Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji itakuwa na naibu mawaziri wawili, ambapo mmoja atasimamia Kazi na Ajira na mwingine atasimamia Vijana na Uwezeshaji.
Kwa upande wa mawaziri, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum amehamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, huku Mhe. Anna Athanas Paul akihamishiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Mhe. Shaaban Ali Othman ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Mipango na Usimamizi wa Utendaji Serikalini.
Mhe. Masoud Ali Mohamed, aliyekuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Uhusiano wa Jamii, huku Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga akiwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi.
Aidha, Mhe. Ali Suleiman Ameir Mrembo ameteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.
Vilevile, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (ACT- Wazalendo) ameteuliwa kuwa Waziri wa Afya, Mhe. Omar Said Shaaban (ACT- Wazalendo) kuwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, na Mhe. Dkt. Nasra Nassor Omar (ACT-Wazalendo) kuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale.
Mhe. Dkt. Mohamed Ali Suleiman, (ACT- Wazalendo), ameteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu.
Mawaziri wanaoendelea katika nafasi zao ni pamoja na:
1. Mhe. Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora.
2. Mhe. Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi.
3. Mhe. Riziki Pembe Juma, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
4. Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.
5. Mhe. Rahma Kassim Ali, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi.
6. Mhe. Lela Muhamed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.
7. Mhe. Suleiman Masoud Makame, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo.
8. Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.
9. Mhe. Nadir Abdullatif Alwardy, Waziri wa Maji, Nishati na Madini.
Kwa upande wa naibu mawaziri, Mhe. Hassan Khamis Hafidh ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Hamad Omar Bakari amehamishiwa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, na Mhe. Mboja Ramadhan Mshenga amehamishiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Aidha, Mhe. Dkt. Salum Sudi Hamid atakuwa Naibu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mhe. Bakari Hamad Bakari atakuwa Naibu Waziri wa Fedha, na Mhe. Juma Hassan Thabit Kaponda atakuwa Naibu Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale.
Mhe. Zawadi Amour Nassor na Mhe. Seif Kombo Pandu watakuwa naibu mawaziri katika Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.
Mhe. Zawadi atashughulikia masuala ya Vijana na Uwezeshaji, huku Mhe. Seif akishughulikia masuala ya Kazi na Ajira. Aidha, Mhe. Khadija Salum Ali amehamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Naibu mawaziri wanaoendelea katika nafasi zao ni pamoja na:
1. Mhe. Ali Abdulgullam Hussein, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
2. Mhe. Salha Mohamed Mwinjuma, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi.
3. Mhe. Mohamed Sijamini Mohamed, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu.
4. Mhe. Badria Atai Masoud, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.
Miradi ya Kimkakati
Akijibu maswali ya wanahabari kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Rais Dkt.Mwinyi amethibitisha kuwa,Serikali imejipanga kukamilisha miradi yote mikubwa ndani ya kipindi kilichobaki cha miaka minne hadi kufikia mwaka 2030.
Mheshimiwa Rais amesisitiza kuwa, nguvu kubwa imeelekezwa katika miundombinu inayohusiana na mashindano ya kandanda ya Afrika (AFCON 2027), akibainisha kuwa ujenzi wa viwanja, barabara na miundombinu husika unakwenda kwa kasi nzuri na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni,mwakani.
Aidha, miradi mingine kama upanuzi wa Bandari ya Mpigapwani, uanzishwaji wa shirika la ndege la Zanzibar, reli ya kisasa, na usafiri wa majini wa water taxis ipo katika hatua za mwisho za maandalizi na michoro.
Wakati huo huo, Rais Dkt Mwinyi amesisitiza kuwa,uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unalenga kuleta utulivu, kuondoa migawanyiko ya kisiasa na kuwaunganisha Wazanzibari katika ajenda moja ya maendeleo.
"Nchi inahitaji amani na umoja ili iendelee kupata maendeleo. Wakati watu wanalumbana na kugombana ni kazi kubwa sana, matarajio yangu ni kwamba kupitia serikali hii tutaweka kipaumbele katika kuwaletea wananchi maendeleo,"amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Tags
ACT Wazalendo
Baraza la Mawaziri Zanzibar
Breaking News
CCM Zanzibar
Dkt.Hussein Ali Mwinyi
Habari
Mabadiliko Baraza la Mawaziri
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Uteuzi
