RIYADH-Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Z. Homera, ameongeza ujumbe wa Sekta ya Nishati katika Mkutano wa 17 wa Mawaziri wa Jukwaa la Kimataifa la Nishati (International Energy Forum - IEF17), unaofanyika jijini Riyadh, Saudi Arabia, kuanzia tarehe 11 hadi 12 Oktoba 2026.
Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera akishiriki Mkutano wa 17 wa Jukwaa la Nishati Duniani jijini Riyadh, Saudi Arabia leo.
Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al Saud, chini ya kaulimbiu isemayo “Usalama wa Nishati na Malengo ya Pamoja katika Nyakati Mpya.”
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mwanamfalme Abdulaziz bin Salman Al Saud amesisitiza umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya ana kwa ana baina ya nchi wanachama ili kutathmini mikakati iliyopo na kuweka mipango mipya itakayohakikisha usalama na uendelevu wa nishati duniani.
Amesisitiza dhamira ya Saudi Arabia ya kuendelea kuwa mdau muhimu katika kuimarisha usalama na uendelevu wa nishati duniani, kwa kushirikiana na nchi washirika katika kukabiliana na changamoto zinazokabili sekta hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jukwaa la Kimataifa la Nishati, Jassim Alshirawi, amesema kaulimbiu ya mkutano huo imezingatia hali ya sasa ya dunia, hususan changamoto zinazohusu uhakika wa upatikanaji wa nishati na kuhakikisha nishati endelevu inapatikana kwa wote.
Jukwaa la Kimataifa la Nishati linaunganisha zaidi ya nchi wanachama 70 kutoka maeneo mbalimbali duniani, zikiwemo nchi zinazozalisha na zile zinazotumia nishati.
Jukwaa hilo hutoa nafasi ya majadiliano na kubadilishana uzoefu kuhusu mwenendo wa masoko ya nishati, usalama wa upatikanaji wake na ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni fursa ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya nishati, kubadilishana uzoefu na kujadiliana kuhusu mikakati ya kuimarisha usalama wa nishati kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Tags
Dr Juma Homera
Habari
IEF17
Jukwaa la Nishati Duniani
Kimataifa
Riyadh
Wizara ya Nishati Tanzania


