Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 si utajiri tu, ni hazina kwa Watanzania

NA DIRAMAKINI

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imesema, Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 inalenga kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma, kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika shughuli za Serikali na kupanua ushiriki wa wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani katika fursa za kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 2,2026 mkoani Morogoro na Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba wakati wa mafunzo kwa wahariri, waandishi wa habari na wamiliki wa mitandao ya kijamii.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Wizara ya Fedha yamelenga kuwaongezea wanahabari uelewa kuhusu sera hiyo na kuwajengea uwezo wa kuhabarisha umma kwa usahihi.

Kamishna huyo amesema, kuanzishwa kwa sera hiyo ni hatua ya mwanzo katika safari ya kuimarisha usimamizi wa mnyororo wa ugavi nchini, huku mafanikio yake yakitegemea uwepo na utekelezaji madhubuti wa sheria, kanuni, miongozo, mifumo na taratibu zitakazobainisha majukumu ya kila mdau.

Amesema, sera hiyo haijikiti katika eneo la ununuzi pekee, bali inahusisha mnyororo mzima wa shughuli unaoanzia katika kutambua mahitaji, uzalishaji, upatikanaji wa bidhaa na huduma, usafirishaji, uhifadhi na hatimaye matumizi.
Bw.Haraba amesema, lengo ni kuhakikisha kila hatua katika mnyororo wa ugavi inasimamiwa kwa ufanisi ili kupunguza upotevu wa rasilimali, kuboresha ubora wa huduma na bidhaa na kuhakikisha Serikali pamoja na wananchi wanapata thamani inayostahili kutokana na fedha zinazotumika.

“Utekelezaji wa sera unahitaji ushiriki wa kila mdau. Wizara ina jukumu la kutoa miongozo, lakini utekelezaji wake ni jukumu la wadau wote, wakiwemo wanahabari, wananchi na wafanyabiashara."

Bw.Haraba amesema, Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 pia imeweka msisitizo katika kuwapa nafasi wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani kunufaika na fursa zinazotokana na shughuli za Serikali.

Amesema, ili wananchi na wafanyabiashara wanufaike na fursa hizo, ni muhimu kuwa na uelewa wa taratibu, mifumo na vigezo vinavyotumika katika upatikanaji wa zabuni za Serikali.

Kamishna huyo ameongeza kuwa,wananchi wanapaswa kutumia mifumo iliyowekwa kutambua fursa zinazotangazwa, kushiriki katika zabuni na kufuatilia utekelezaji wa sera ikiwemo kuhakikisha fursa zilizotengwa kwa makundi mbalimbali zinawafikia walengwa.

Ametoa mfano wa fursa zinazotengwa kwa makundi maalumu, akisema wananchi wanaweza kunufaika endapo watajipanga, kusajiliwa katika mifumo husika na kushiriki katika taratibu za zabuni kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

Pia, amewataka wananchi na wadau wengine kufuatilia utekelezaji wa sera na kutoa mrejesho pale wanapobaini changamoto, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu na ufafanuzi kuhusu utekelezaji wake.
Vilevile, Bw.Haraba amesema,vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanafahamu maudhui ya sera hiyo, fursa zinazotokana nayo na namna wanavyoweza kushiriki katika utekelezaji wake.

“Tunategemea waandishi wa habari waeleze kwa kina fursa na mambo mengine yaliyopo kwenye sera, ili wananchi waelewe na waweze kushiriki,” amesema Kamishna huyo.

Amesema,uelewa mpana wa wananchi kuhusu sera, sheria na mifumo ya ununuzi wa umma ni muhimu katika kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa jamii katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii, Bw.Mathias Canal amewataka waandishi wa habari kutumia maarifa waliyoyapata katika mafunzo hayo kuelimisha umma kuhusu fursa, wajibu na manufaa yanayoweza kupatikana kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025.

Amesema, waandishi wanapaswa kuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi kwa kutoa taarifa sahihi, zenye kina na zinazoeleza kwa uwazi athari, fursa na manufaa ya sera kwa jamii, badala ya kuripoti taarifa bila kuzichambua.

Bw.Camal amesema,utekelezaji wa sera hiyo unaweza kutoa fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani, sambamba na kuchochea uwazi, ufanisi na maendeleo ya uchumi.

“Tunapaswa kufanya kazi kubwa ya uhakiki wa ukweli. Mawasiliano na wataalamu na viongozi wanaohusika na sera hii ni muhimu katika kujenga habari zenye weledi,”amesema Bw.Canal.

Pia, amesisitiza kuwa,waandishi wanapaswa kuchambua utekelezaji wa sera kwa kujiuliza maswali muhimu kuhusu nani anawajibika, nini kinapaswa kufanyika na wananchi wanawezaje kunufaika na fursa zilizopo.
Ameongeza kuwa,vyombo vya habari vinaweza kusaidia wananchi kuelewa mnyororo mzima wa utekelezaji wa sera, kuanzia dira, sera, sheria, kanuni na miongozo hadi hatua ya utekelezaji na uwajibikaji.

Katika mafunzo hayo, washiriki walipata uelewa kuhusu tofauti na uhusiano uliopo kati ya Dira, sera, sheria, kanuni na miongozo, pamoja na namna Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 inavyohusiana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inaweka mwelekeo wa kimkakati wa maendeleo ya nchi kwa kulenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani.

Kwa upande mwingine, Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 inatoa mwongozo wa kuimarisha nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, kupunguza upotevu wa rasilimali, kuongeza ufanisi katika miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Msingi wa utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma unaungwa mkono na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Na. 10 ya mwaka 2023, pamoja na kanuni na miongozo inayotolewa kwa ajili ya kufafanua namna taasisi za umma zinavyopaswa kutekeleza majukumu yake.

Hivyo, Dira huweka mwelekeo mpana wa maendeleo ya taifa, sera hutafsiri mwelekeo huo katika maeneo ya utekelezaji, wakati sheria huweka masharti ya kisheria yanayopaswa kuzingatiwa.

Kanuni na miongozo nayo hutoa maelekezo ya kiutendaji, huku mifumo ya kielektroniki ikisaidia katika utekelezaji, usimamizi, ufuatiliaji na utunzaji wa taarifa.
Aidha, mtiririko huo wa kimkakati unaenda sambamba na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika usimamizi wa manunuzi ya umma ikiwemo Mfumo wa Manunuzi ya Umma wa Kielektroniki (NEST).

Mifumo hiyo inalenga kuwezesha usajili, utangazaji wa fursa, ushiriki wa wazabuni, uhifadhi wa taarifa na ufuatiliaji wa shughuli za ununuzi wa umma kwa njia inayoweza kuongeza uwazi na ufanisi.

Aidha, takwimu na taarifa zinazopatikana kupitia mifumo hiyo pamoja na ripoti za Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) zinaweza kutumika katika kufuatilia utekelezaji wa sera na sheria ikiwemo ushiriki wa makundi maalumu katika fursa za ununuzi wa umma.

Mafunzo hayo yametolewa na wataalamu mbalimbali wa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano na wanataaluma Dkt.Maige Makaseke Mwasimba kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na Dkt.Hezron Makundi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hata hivyo, mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa wanahabari na wamiliki wa majukwaa ya mitandao ya kijamii kuhusu mfumo wa usimamizi wa mnyororo wa ugavi, uhusiano wake na mipango ya maendeleo ya taifa na nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here