NA DIRAMAKINI
SERIKALI imezindua rasmi Mwongozo wa Kuchopeka Elimu ya Fedha katika Mitaala ya Elimu ya Juu, Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kuwajengea vijana maarifa ya kusimamia fedha na rasilimali kwa tija katika ulimwengu wa kidijitali.


Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 2,2026 katika Ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akiwa ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir.Akizungumza katika hafla hiyo,Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir amesema, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 imeweka matarajio makubwa ya kujenga uchumi wenye ushindani na tija unaotegemea rasilimali watu wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Amesema, kama Taifa hatuwezi kufikia matarajio hayo bila kuwa na wananchi hususani vijana wenye uwezo wa kupanga na kusimamia fedha zao kwa ufasini, kuweka akiba, kuwekeza, kukopa kwa uwajibikaji na kutumia rasilimali walizonazo kwa busara.
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa, kwa msingi huo uwezo wa wananchi kusimamia fedha zao si suala la ustawi wa wananchi binafsi pekee, bali ni msingi muhimu wa kujenga uchumi imara, jumuishi, endelevu pamoja na kuimarisha uwezo wa taifa kufikia malengo yake ya maendeleo.
Amesema,mwongozo huo umeanisha namna ya sekta ya elimu inatavyoshiriki katika utekelezaji wake kwa kuweka bayana majukumu ya Wizara, Taasisi za Urekebu na Taasisi za Elimu ya Juu.
Pia, amesema msingi wa mwongozo huo unaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 20 na 23, Mfumo wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha ya mwaka 2023/28, Mpango kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha mwaka 2021-2029/2030 pamoja na lengo la nne la Mpango wa Maendeleo Endelevu.
“Leo kijana anaweza kupata huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali kwa haraka na kwa urahisi zaidi kuliko hapo awali, ambapo bila ya kuwa na uelewa na maarifa ya kutosha ya fedha urahisi huo unaweza kusababisha maamuzi yenye gharama kubwa kwa mtu binafsi na kwa familia,” amesema.

Amefafanua kuwa, maudhui ya mwongozo huo ni msingi wa umahiri katika elimu ya kifedha, ambapo mwongozo huo utatekelezwe kikamilifu na matokeo yake yaonekane katika maisha, uwezo na maamuzi ya wahitimu nchini.
Pia, amesema anatarajia kuona mabadiliko katika ngazi nne muhimu ikiwemo Mitaala inayokisi elimu ya fedha, kuwa na ufundishaji na upimaji unaojenga umahiri katika maeneo hayo, kuwa na wanafunzi wanaoweza kutumia maarifa na umahiri huo katika maisha yao ya kila siku.
Sambamba na kuwa na wahitimu wanaoweza kufanya maamuzi sahihi na yenye uwajibikaji wa kifedha wanapoingia katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri huyo amesema, wizara itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwa mratibu mkuu wa utekelezaji wa mwongozo huo, pamoja na kuhakikisha viashiria vya elimu ya fedha zinaingizwa katika mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya sekta ya elimu na pia taarifa za utekelezaji zinakusanywa, kuchambuliwa na kutumika kwa wakati ili kuboresha sera, mipango na utekelezaji wa shughuli za kifedha.
Aidha, ametoa rai kwa wizara kuendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na NACTVET ili kufanya mapitio ya pamoja ya utekelezaji wa mwongozo huo mara kwa mara.
Ni kwa lengo la kutathmini maendeleo yaliyofikiwa ili kubaini changamoto na mapungufu na kuchukua hatua stahiki za kuboresha utekelezaji wake pale panapohitajika.
Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Kifedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo amesema,mwongozo wa elimu ya fedha unalenga makundi mawili, ambayo ni wananchi walio ndani na nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Gavana wa BoT, amesema, kwa walio ndani ya mfumo wa elimu, mchakato umeandaa wakufunzi watakaotoa elimu ya fedha katika ngazi ya elimu ya juu.
Naibu Gavana huyo amesema, elimu hiyo inalenga kutolewa bila kuathiriwa na maslahi ya kibiashara, huku hadi Juni 2026 jumla ya wakufunzi 1,736 wakiwa wamehitimu na kuwa tayari kushiriki katika mchakato huo.
Kwa upande wa wananchi walio nje ya mfumo rasmi wa elimu, amesema zaidi ya watu milioni 1.8 wamefikiwa kupitia njia mbalimbali za utoaji elimu ya fedha.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi amesema,elimu ya fedha sio jukumu la sekta ya fedha pekee yake, ni jukumu la Wizara ya Elimu, pia ni suala la maendeleo ya watu na msingi wa ustawi wa uchumi wa taifa letu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Amosi John Henock amesema, uzinduzi wa mwongozo huo ni muendelezo wa kimkakati wa juhudi za kuimarisha elimu katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kupitia masomo ya biashara na uchumi.
Naye Kaimu Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha, Dionisia Mjema amesema,Dira ya Taifa ya 2050 imeteua sekta ya fedha kuwa ni sekta ya kuchochea uchumi, ambapo katika matokeo ya uchumi yaliyofanyika sekta hiyo inaongoza.
Amesema, hayo yote yametokana na kuimarisha uratibu wa masuala ya fedha nchini tokea kupewa Wizara hiyo kusimamia jukumu la fedha na ujumuishaji wa wananchi kiuchumi, ambapo wameandaa Mpango Mkuu wa Utekelezaji katika sekta ya fedha ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 2020-2021/30.Mjema ameeleza katika mpango huo moja ya maeneo ya kimkakati ni kumlinda mtumaji wa huduma za fedha na uelewa wa masuala ya fedha, ambao umetoa lengo ifikapo 2030 asilimia 80 ya wananchi wawe na uelewa wa masuala ya fedha, mchango wa fedha katika uchumi ufikie asilimia 10, ujumuishaji wa sekta ya benki ufikie asilimia 50, Bima asilimia 50, Hifadhi ya Jamii asilimia 20 na masoko ya mitaji asilimia tano.
Kwa upande wake Kamishna wa Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Yussuf Ibrahim Yussuf amesema,Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 imeweka muelekeo wa kujenga uchumi wa kipato cha kati na cha juu unaoleta ustawi kwa wananchi wote.
Amesema,ili kufikia azima hiyo wanategemea uwekezaji katika rasilimali watu, elimu zenye ubora na mafunzo ya fedha unaochochea mageuzi ya kiuchumi, ambapo elimu ya fedha inamchango wa kimkakati katika kuunganisha maeneo hayo na kuimarisha uwezo wa wananchi katika kushiriki maendeleo.




Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Bw. Kenedi Komba amesema, mwongozo huo unalenga kuongeza uelewa wa masuala ya fedha, ikiwemo upangaji wa bajeti, taarifa za mikopo na uwezo wa kulinganisha viwango vya riba, hususan kwa wahitimu wa vyuo.
Amesema, kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu katika kipindi hiki cha kidijitali kumerahisisha sana michakato mbalimbali ya kifedha, lakini mchakato huo unawaweka wananchi hususan wanafunzi katika hatari ya mikopo isiyopangwa, ulaghai wa kifedha, uwekezaji usio salama na kutumia huduma ambazo masharti yake hayaeleweki.
Komba amesema, mwongozo huo unalenga kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi na salama katika matumizi ya huduma za kifedha kidijitali.



