DAR ES SALAAM- Serikali imesisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasilimali za maendeleo nchini huku ikihakikisha kuwa rasilimali hizo zinaendana na vipaumbele vya taifa na kuingizwa ipasavyo katika mipango na bajeti za Serikali ili kukuza uchumi wa nchi.
Msisitizo huo ulitolewa na Kamishna wa Fedha za Nje, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, kupitia Hotuba yake iliyosomwa na Afisa Usimamizi wa Fedha Mkuu, Idara ya Bajeti, Wizara ya Fedha, Bw. Amede Andrea, wakati wa kufungua mafunzo elekezi ya mwaka 2026.
Ni kuhusu Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework – DCF), yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, Tanzania Bara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango – Zanzibar, yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar Es Salaam.
Alisema, ushiriki wa washirika wa maendeleo, taasisi za Serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia ni muhimu katika kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo zinaleta matokeo yenye manufaa kwa taifa.
"Uelewa wa pamoja wa mifumo na michakato hii ni muhimu katika kuhakikisha kuwa misaada ya maendeleo inaendana na vipaumbele vya taifa, inawasilishwa ipasavyo katika michakato ya mipango na bajeti ya Serikali, na inasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji,” alisema Bw. Bade.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kamishna wa Fedha za Nje, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha- Zanzibar, Bw. Yusuph Ibrahim alisema kuwa, majadiliano yaliyofanyika yameimarisha uelewa wa umuhimu wa kuoanisha misaada ya maendeleo na vipaumbele vya taifa, kuimarisha michakato ya mipango na bajeti ya Serikali, na kukuza uwazi na uwajibikaji.
“Nawahimiza washiriki wote kutumia maarifa waliyoyapata katika taasisi zao na yaliyopatikana kupitia mafunzo haya, kuwa na mazungumzo endelevu, uratibu wenye ufanisi na ushirikiano imara, na kuhakikisha kuwa rasilimali za ushirikiano wa maendeleo zinachangia kufikia malengo ya maendeleo ya Tanzania,” alisema Bw. Ibrahim.
Aliongeza kuwa, ni muhimu kwa wadau kuendeleza ushirikiano wenye misingi ya ubia, uwajibikaji wa pamoja na dhamira ya kufikia maendeleo endelevu.
Akizungumza kwa niaba ya washirika wa maendeleo ya Tanzania, waliohudhuria mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini Tanzania, Bi. Lise Breuil, aliishukuru Wizara ya Fedha pande zote mbili (Tanzania Bara na Zanzibar), kwa kuandaa mafunzo hayo, huku akiahidi kuwa Balozi kwa washirika wengine wa maendeleo.
Mafunzo hayo ya mwaka 2026 yamewakutanisha Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Washirika wa Maendeleo kupitia Development Partners Group (DPG), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), pamoja na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO).
Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uelewa na uratibu miongoni mwa wadau ili kuhakikisha ushirikiano wa maendeleo unatekelezwa kwa ufanisi na kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Tags
Habari
Maendeleo
Matumizi ya Rasilimali
Serikali
Uchumi wa Tanzania
Uwajibikaji
Uwazi
Wizara ya Fedha



