DAR ES SALAAM- Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa Mwongozo wa Ushauri kwa Wasafiri Na. 18 wa tarehe 17 Oktoba, 2026, unaoanza kutumika mara moja ili kuimarisha afua za afya ya jamii zinazohusu usafiri wa kimataifa.
Mwongozo huo unakuja kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na hivi karibuni kupatikana kwa mgonjwa wa Ebola nchini Kenya aliyesafiri akitokea DRC.
Kwa mujibu wa mwongozo uliosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace E. Magembe, hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia Kanuni za Afya Kimataifa za mwaka 2005, kama zilivyorekebishwa mwaka 2024, na Sheria ya Afya ya Jamii ya Tanzania ya mwaka 2009.
Wizara imetangaza masharti yafuatayo kwa wasafiri wa kimataifa:
1. Kujaza Fomu ya Afya
Wasafiri wote wanatakiwa kujaza kwa uaminifu Fomu ya Ufuatiliaji wa Afya ya Msafiri mtandaoni kupitia:
https://afyamsafiri.moh.go.tz KABLA ya kuanza safari ya kuja Tanzania au wanapowasili.
Wanapaswa kutoa taarifa sahihi na kuhifadhi msimbo wa QR wa uthibitisho au namba ya kumbukumbu kwa ajili ya uhakiki na mamlaka za afya mipakani wanapowasili.
2. Uchunguzi wa Afya Mipakani
Wasafiri wote watafanyiwa uchunguzi wa afya, ikiwemo kupimwa joto la mwili, katika mipaka ya kuingia nchini, yaani viwanja vya ndege, vituo vya mipakani vya nchi kavu na bandari.
Mtu anayehisiwa kuwa na ishara na dalili za ugonjwa wa Ebola au ugonjwa mwingine wowote wa kuambukiza atahudumiwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Kitaifa wa Uchunguzi wa Afya kwa Wanaingia na Kutoka Nchini.
3. Taarifa za Afya na Kuripoti
Wasafiri wote watapewa taarifa za afya na kushauriwa kufuatilia hali zao za afya na kuripoti ishara na/au dalili za ugonjwa wa Ebola au ugonjwa mwingine wowote wa kuambukiza katika kituo cha afya kilicho karibu, kituo cha mipakani, au kuwasiliana na mamlaka kupitia namba ya simu 199 bila malipo au barua pepe: poe@afya.go.tz.
4. Ufuatiliaji wa Lazima
Ufuatiliaji wa lazima wa hali ya afya utafanyika kwa wasafiri walio katika hatari kubwa kwa kipindi cha siku 21, kupitia ujumbe wa kila siku unaotumwa au njia nyingine za mawasiliano, kwa mujibu wa Mwongozo wa Kitaifa wa Uchunguzi wa Afya kwa Wanaingia na Kutoka Nchini.
Wasafiri wanatakiwa kutoa ushirikiano na kujibu ujumbe katika kipindi chote cha ufuatiliaji, hata baada ya kutoka nchini ndani ya kipindi hicho.
5. Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi
Wasafiri wote na waendeshaji wa vyombo vya usafiri LAZIMA wazingatie hatua za Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi, kama vile usafi wa mikono, matumizi ya vitakasa mikono na kuepuka mgusano wa kimwili usio wa lazima.
6. Usafi wa Vyombo vya Usafiri
Chombo chochote cha usafiri kinachobeba mtu, mizigo au mabaki ya mwili wa binadamu yanayohusishwa na ugonjwa wa Ebola au ugonjwa mwingine wowote wa kuambukiza kitafanyiwa usibuaji na utakasaji katika vituo vya Mamlaka za Afya Mipakani ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa.
ZINGATIA:
- Wasafiri wanaotoka Tanzania kwenda nje ya nchi, wanashauriwa kuzingatia masharti ya kuingia katika nchi wanazokwenda au wanazopitia.
- Ushauri huu utapitiwa na kuhuishwa mara kwa mara kadri itakavyohitajika.
