NA DIRAMAKINI
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki amewahamasisha wananchi wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi mbele ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ili kutoa ushahidi, ushauri na taarifa walizonazo kuhusu matukio hayo.
Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Shaban Ally Lila inaendelea kupokea na kusikiliza maoni, ushahidi na taarifa kutoka kwa wananchi wa Temeke katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampasi ya Elimu (DUCE) kilichopo Chang’ombe kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.
Akizungumza leo, Sheikh Kishki amesema, ujio wa Tume hiyo katika Wilaya ya Temeke ni fursa muhimu kwa wakazi wa eneo hilo kushirikiana na Tume kwa kutoa taarifa wanazozifahamu kuhusu ghasia na ukiukwaji wa sheria uliojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Habari njema kwa wananchi wa Temeke, Tume ya Jaji Lila tayari imefika Temeke na ipo hapa DUCE. Wananchi wa Temeke, wafanyakazi wa Temeke na wana wa TMK wenzangu, ninawaomba kwa heshima na taadhima, njooni kwa wingi ili kukutana na Tume hii na kutoa ushirikiano, ushahidi au taarifa zozote mlizonazo kuhusu ghasia za Oktoba mwaka jana,” amesema.
Sheikh Kishki amesisitiza kuwa,ushiriki wa wananchi katika mchakato huo ni muhimu kwa masilahi mapana ya Taifa, akitumia methali ya Kiswahili inayosema, “Usipoziba ufa, utajenga ukuta,” kuhimiza hatua za mapema katika kushughulikia changamoto zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
Amesema, wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kueleza wanachokifahamu kwa Tume ili kusaidia katika jitihada za kujenga mazingira bora ya amani, usalama na utulivu nchini.
“Kwa maslahi mapana ya Tanzania, tujitokeze kwa wingi ili kuisaidia Tume yetu. Wana wa Temeke, huu ni wajibu wetu kwa ajili ya mustakabali wa Tanzania, kwa ajili ya amani, usalama na utulivu wa nchi yetu,” amesema.
Aidha, Sheikh Kishki amdwataka wananchi wenye ushahidi, ushauri, vielelezo au taarifa nyingine zinazoweza kusaidia kazi ya Tume kutumia fursa hiyo kuwasilisha taarifa zao.
“Ninawaomba wale wote wenye ushahidi, ushauri, dalili au chochote kile kinachoweza kusaidia, njooni. Tushirikiane ili Tanzania iendelee kuwa nchi tulivu na salama,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa amani katika jamii, Sheikh Kishki amerejea mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) akisisitiza kuwa, amani ni miongoni mwa neema kubwa zinazopaswa kulindwa na kuthaminiwa na jamii.
Sheikh Kishki amesema, amani, afya njema na upatikanaji wa chakula cha siku ni miongoni mwa neema muhimu katika maisha ya binadamu, hivyo wananchi wanapaswa kushirikiana katika kulinda amani na utulivu wa nchi.
Tume hiyo inaendelea na zoezi la kusikiliza wananchi wa Temeke ndani ya eneo la Chuo cha DUCE hadi Oktoba 9, 2026, ambapo wananchi wenye taarifa zinazohusiana na matukio yanayochunguzwa wanahimizwa kutumia fursa hiyo kuwasilisha ushahidi na maoni yao.
Sheikh Kishki amesisitiza kuwa, ushiriki wao ni muhimu katika kujenga msingi wa amani, usalama na utulivu wa Tanzania.
Tags
Chang'ombe
Dar es Salaam
Sheikh Nurdin Kishki
Temeke
Tume ya Haki Jinai
Tume ya Jaji Lila
Wananchi Temeke

