NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Oman imesema kuwa, historia ya uhusiano kati ya Tanzania na Taifa hilo imejengwa kwa karne nyingi za mwingiliano wa watu, biashara, utamaduni, utawala na maisha ya jamii, urithi ambao unaendelea kuonekana kupitia lugha, mila, sanaa, vyakula na hasa majengo ya kihistoria yaliyotapakaa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, hususan Zanzibar.
Hivyo, uhifadhi wa majengo ya kihistoria hauwezi kuangaliwa kama suala la ukarabati wa majengo pekee, bali ni jukumu la kulinda kumbukumbu, utambulisho na urithi wa pamoja unaounganisha vizazi vya sasa na historia ya jamii zilizotangulia.Meneja wa Miradi na Mhandisi wa Ujenzi, Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili ameyasema hayo leo Oktoba 1,2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada kuhusu “Kuhifadhi Urithi wa Usanifu Zanzibar: Kuanzia Urejesho hadi Uendelevu-Nyumba ya Maajabu kama Mfano”.
Ni katika kongamano la Kimataifa kati ya waandishi wa habari wa Tanzania na Oman ambalo limewakutanisha pamoja na wanadiplomasia wakiwemo maafisa wa Serikali zote mbili.
Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 19 katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya ujenzi na uhifadhi wa majengo ya kihistoria kwa sasa anafanya kazi katika Wizara ya Urithi na Utalii ya Usultani wa Oman kama meneja wa mradi na mwakilishi wa mmiliki.
Pia, amehusika katika usimamizi wa miradi ya ukarabati na uhifadhi wa majengo ya kihistoria na urithi ikiwemo miradi inayohusisha Zanzibar.
Kwa uzoefu huo, anasisitiza kwamba kuhifadhi urithi wa usanifu kunahitaji mchanganyiko wa utaalamu wa kihandisi, uelewa wa historia, matumizi sahihi ya teknolojia, ushirikiano wa taasisi na jamii.
Sambamba na mpango wa kuhakikisha majengo hayo yanaendelea kuwa na thamani kwa vizazi vijavyo.
Miongoni mwa majengo yaliyopewa uzito katika mjadala huo ni Nyumba ya Maajabu (Beit al-Ajaib) ya Zanzibar, jengo ambalo limekuwa sehemu muhimu ya historia na utambulisho wa Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Ukarabati wake umeelezwa kama mfano wa namna jengo la kihistoria lililokumbwa na uharibifu mkubwa linavyoweza kufanyiwa tathmini, kuimarishwa na kurejeshwa kwa kuzingatia thamani yake ya kihistoria na usanifu.
Mradi huo ulianza mwezi Desemba 2020 kufuatia kuanguka kwa sehemu ya jengo hilo, hali iliyohitaji hatua za haraka za kiuhandisi ili kulinda sehemu zilizokuwa zimesalia.
Amesema, badala ya kuanza ujenzi mpya bila kuzingatia historia ya jengo, mkakati uliotumika ulianza kwa kufanya uchunguzi wa kina wa hali ya muundo, kubaini maeneo hatarishi na kuweka hatua za muda za kuzuia uharibifu zaidi.
Hatua hiyo inaonesha tofauti muhimu kati ya ujenzi wa kawaida na uhifadhi wa jengo la urithi.
Mhandisi huyo amesema,katika ujenzi wa kawaida lengo linaweza kuwa kujenga muundo mpya kwa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa, wakati katika uhifadhi wa urithi lengo ni kulinda kile kilichopo huku ukirejesha uimara na matumizi ya jengo bila kupoteza tabia yake ya kihistoria.
Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, mkakati wa Wizara ya Urithi na Utalii ya Oman katika uhifadhi wa majengo ya kihistoria unazingatia nguzo zinazohusisha binadamu, uimara wa jengo na historia.
Pia, amesema wanatambua kwamba jengo la kihistoria si kuta, paa, milango na madirisha pekee, bali ni sehemu ya simulizi ya jamii.
Kwa hiyo, kazi ya uhifadhi inalenga kulinda jengo lenyewe, lakini pia kulinda kumbukumbu na maarifa yanayohusishwa nalo.
Amesema, ndio maana mchakato huanza kwa utafiti na tathmini ya awali. Wataalamu hufanya uchunguzi wa kina wa hali ya jengo ikiwemo kuta, msingi, nguzo na sehemu nyingine za muundo ili kubaini kiwango cha uharibifu na maeneo yanayohitaji uangalizi maalumu.
Baada ya hapo, maeneo yaliyo katika hatari ya kuanguka huimarishwa kwa hatua za muda, ikiwemo mifumo ya uimarishaji wa wima na usawa.
Hatua hizo amesema,ni muhimu kwa sababu zinawapa wataalamu nafasi ya kufanya kazi bila kuongeza hatari ya kuanguka kwa sehemu za jengo zilizodhoofika.
Amesema, moja ya maeneo yanayoonesha jinsi teknolojia ya kisasa inavyoweza kutumika kuhifadhi urithi ni matumizi ya laser scanning katika kurekodi muundo wa jengo.
Teknolojia hiyo,Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, hutumiwa kupata kumbukumbu za kina za muundo wa jengo kabla ya kuanza kwa kazi za ukarabati.
Katika kesi mfano wa Nyumba ya Maajabu, Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, kumbukumbu za aina hiyo zilitumika kuweka taarifa za kiufundi kuhusu muundo wa jengo.
Faida yake ni kwamba wataalamu wanapata kumbukumbu sahihi inayoweza kutumika katika uchambuzi, usanifu wa hatua za ukarabati na ufuatiliaji wa mabadiliko ya jengo.
Pia, teknolojia hiyo husaidia kuhifadhi kumbukumbu ya kidijitali ya jengo ambalo linaweza kutumika kwa tafiti na kazi za baadaye.
Changamoto nyingine katika ukarabati wa majengo ya kihistoria, Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, ni kuwepo kwa tabaka au vifaa vilivyoongezwa katika vipindi tofauti bila kuzingatia vifaa vya awali.
Amesema, katika baadhi ya maeneo ya Nyumba ya Maajabu, kwa mfano, wataalamu walilazimika kuondoa tabaka za baadaye ambazo hazikuendana na mfumo wa awali wa jengo ikiwemo baadhi ya plasta za saruji.
Hatua hiyo inalenga kurejesha uwezo wa jengo kupumua na kutumia vifaa vinavyoendana na teknolojia na mazingira ya wakati lilipojengwa.
Amesema, katika uhifadhi wa urithi, matumizi ya vifaa visivyolingana na jengo la zamani yanaweza kusababisha matatizo mapya ya unyevunyevu, nyufa au kudhoofika kwa sehemu nyingine za muundo.
Miongoni mwa mbinu za kiufundi zinazotumika katika ukarabati ni kuchimbua na kujaza mianya na nyufa, pamoja na mbinu ya kushona kuta zilizopasuka.
Nyufa na mianya huchunguzwa kwanza ili kubaini chanzo na kiwango cha tatizo kabla ya kuchagua njia sahihi ya matengenezo.
Katika maeneo yenye nyufa kubwa, Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, mbinu ya kushona kuta hutumika kusaidia kurejesha mshikamano wa sehemu zilizopasuka bila kubadilisha mwonekano wa kihistoria wa jengo.
Amesema, hii ni sehemu muhimu ya falsafa ya uhifadhi, ambayo inalenga kufanya matengenezo yanayohitajika huku ikiepuka mabadiliko yasiyo ya lazima katika mwonekano na tabia ya jengo.
Vilevile, Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, uangalizi wa wataalamu hauishii kwenye kuta za nje.
Amesema, sehemu za ndani, zikiwemo dari na mifumo ya kuhimili uzito, nazo hufanyiwa ukarabati kwa kuzingatia muundo wa awali.
Katika baadhi ya maeneo, mfumo wa dari hujumuisha tabaka mbalimbali zikiwemo chokaa, mbao na viunzi vya chuma vya aina ya I-section beams kulingana na muundo wa jengo.
Amesema,lengo ni kurejesha uimara wa jengo huku ukihifadhi sifa zake za usanifu.
Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, kanuni nyingine muhimu katika uhifadhi wa majengo ya kihistoria ni matumizi ya vifaa vinavyofanana au vinavyolingana na vile vilivyotumika wakati wa ujenzi wa awali.
Hii inahusisha kutambua aina ya vifaa, mbinu za ujenzi na namna vilivyotumika katika kipindi husika.
Kwa kufanya hivyo, amesema wataalamu huepuka kuingiza vifaa vinavyoweza kubadilisha tabia ya jengo au kusababisha matatizo ya kiufundi katika siku zijazo.
Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, uhifadhi haupaswi kuchukuliwa kuwa ni kujenga upya kwa maana ya kawaida, bali ni mchakato wa kurejesha uhai wa jengo bila kufuta historia yake.
MIRADI MINGINE YA URITHI
Mbali na Nyumba ya Maajabu, Wizara ya Urithi na Utalii ya Oman inaendelea na juhudi za uhifadhi wa majengo mengine ya kihistoria Zanzibar yakiwemo Nyumba ya Pwani, Nyumba ya Sayyid Barghash, Nyumba ya Al-Matuni pamoja na maeneo mengine ya urithi.
Pia, miradi inayohusisha maeneo kama Nyumba ya Sitti Bint Saad na jumba la makumbusho imetajwa katika muktadha wa juhudi za uhifadhi.
Amesema, kila jengo lina historia, usanifu na changamoto zake, hivyo, mbinu ya ukarabati haiwezi kuwa sawa kwa kila jengo.
"Hilo ndilo linalofanya tafiti za awali, tathmini za kiuhandisi na uelewa wa historia kuwa muhimu kabla ya kuanza kazi."
Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili, ameongeza kubwa, uhifadhi wa majengo hayo unaingia ndani ya historia ndefu ya mwingiliano kati ya Oman na Afrika Mashariki.
Amesema, uhusiano huo ulihusisha biashara, uhamiaji, utawala, dini, lugha, utamaduni na maisha ya jamii katika maeneo ya pwani na visiwani.
Zanzibar ilikuwa miongoni mwa vituo muhimu vya mwingiliano huo, hali iliyoacha alama katika usanifu wa majengo, mitindo ya maisha na utamaduni wa jamii.
Athari hizo zinaonekana pia katika maeneo mengine ya pwani ya Tanzania yakiwemo Bagamoyo, Kilwa na Dar es Salaam, ambako historia ya biashara na mwingiliano wa watu imeacha urithi wa usanifu na kitamaduni.
Katika karne ya 19, wakati wa utawala wa Sultan Sayyid Said bin Sultan, Zanzibar ilipata umuhimu mkubwa katika masuala ya utawala na biashara ya Oman katika Afrika Mashariki.
Historia hiyo ilichangia kuimarika kwa uhusiano wa watu na jamii na kuacha alama ambazo bado zinaonekana katika utamaduni wa Pwani ya Afrika Mashariki.
Wakati huo huo, mjadala kuhusu uhifadhi wa urithi umeweka wazi kwamba jukumu hilo haliwezi kubebwa na serikali pekee.
Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili amesema, jukumu hilo linahitaji ushirikiano kati ya serikali, mamlaka za uhifadhi, wataalamu wa usanifu na uhandisi, taasisi za kitaaluma, jamii zinazozunguka maeneo ya urithi, sekta binafsi, taasisi za utamaduni na vyombo vya habari.
Amesema, jamii ina nafasi muhimu kwa sababu ndiyo inayozunguka na kutumia maeneo hayo kila siku.
Pia, amesema wataalamu wana nafasi ya kuhakikisha kanuni za kiufundi na kihistoria zinafuatwa, wakati taasisi za kitaaluma zinaweza kufanya tafiti na kuhifadhi maarifa.
Sekta binafsi nayo inaweza kushiriki katika uwekezaji unaozingatia uhifadhi na matumizi endelevu ya maeneo ya urithi.
Katika mjadala huo, nafasi ya vyombo vya habari imepewa umuhimu mkubwa. Magazeti, redio, televisheni na majukwaa ya kidijitali vina uwezo wa kuelimisha jamii kuhusu thamani ya majengo ya kihistoria na kueleza sababu zinazofanya yahifadhiwe.
Vyombo vya habari pia vinaweza kusaidia kurekodi simulizi za wazee, wataalamu na jamii kuhusu historia ya maeneo hayo kabla maarifa hayo hayajapotea.
Kwa upande wa Oman, historia ya vyombo vya habari yenyewe imekuwa sehemu ya mjadala wa namna magazeti na machapisho yalivyosaidia kuhifadhi kumbukumbu za kijamii, kiutamaduni na kiakili.
Profesa Dkt.Mohsin bin Hamoud Al Kundi amesema kubwa, waandishi na wahariri wa vizazi mbalimbali walitumia machapisho kama majukwaa ya elimu, mijadala ya kijamii na uhifadhi wa kumbukumbu.
Amesisitiza kuwa, uandishi wa habari kuhusu urithi haupaswi kuishia katika taarifa za matukio ya ukarabati. Unapaswa kwenda zaidi kwa kuandika historia, kufanya uchunguzi, kurekodi ushuhuda na kueleza thamani ya urithi huo kwa kizazi cha sasa.
Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili anaongeza kuwa, changamoto kubwa baada ya kukamilika kwa ukarabati si kumaliza ujenzi pekee, bali kuhakikisha jengo linaendelea kutunzwa.
Amesema, jengo lililorejeshwa linahitaji mpango wa matumizi, matengenezo ya mara kwa mara, ufuatiliaji wa hali ya muundo na usimamizi unaozingatia thamani yake ya kihistoria.
Ikiwa jengo litarejeshwa, lakini likaachwa bila mfumo wa matengenezo,Mhandisi Ahmed bin Khalfan bin Saif Al-Shukaili anasema, linaweza kuanza kuharibika tena.
"Uhifadhi wa kweli una mzunguko unaoanzia katika utafiti, tathmini, uimarishaji, ukarabati, matumizi sahihi, matengenezo na ufuatiliaji wa muda mrefu."
Tags
Chama cha Waandishi wa Habari wa Oman
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Makala
Mji Mkongwe Zanzibar
Tanzania na Oman
Waandishi wa Oman
Zanzibar na Oman