Tanzania na Poland zaimarisha ushirikiano wa kiuchumi na ufadhili wa Miradi ya SGR

BANGKOK- Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amekutana kwa mazungumzo ya pande mbili na Waziri wa Fedha na Uchumi wa Poland, Mhe. Andrzej Domański kujadili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kifedha kati ya nchi hizo mbili, kikao kilichofanyika kando ya Mikutano ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia jijini Bangkok nchini Thailand.
Mazungumzo hayo yalilenga kutathmini maendeleo ya ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Poland, hususan katika ufadhili wa miradi ya kimkakati ya miundombinu kupitia Shirika la Bima ya Mikopo ya Mauzo ya Nje la Poland (KUKE), pamoja na kubaini fursa mpya za ushirikiano wa maendeleo.

Poland imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), unaolenga kuimarisha usafiri, kurahisisha biashara na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi katika ukanda.
Viongozi hao wamejadili pia uwezekano wa kupanua ushirikiano katika maeneo yenye manufaa ya pamoja, kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania na fursa za uwekezaji zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza tija.

Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na washirika wake wa kimataifa ili kuvutia uwekezaji, kupata rasilimali za kufadhili miradi ya kimkakati na kuharakisha utekelezaji wa Dira 2050 kwa manufaa ya wananchi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, na baadhi ya maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha ya Tanzania na nchini Poland.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here