BANGKOK- Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema, kuna umuhimu wa nchi wanachama wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia kuweka ushirikiano thabiti kati ya sera za fedha na bajeti ili kudumisha utulivu wa uchumi na ustahimilivu katika mazingira ya sasa ya mishtuko ya kimataifa.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo wakati wa Mkutano wa Kundi la Kwanza la nchi wanachama wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) uliofanyika kando ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa IMF na Benki ya Dunia inayofanyika jijini Bangkok nchini Thailand.
Amesema kwa upande wa Tanzania, katika kusimamia na kukabiliana na mitikisiko ya kiuchumi, imefanya marekebisho ya sheria ili kuruhusu Serikali kuiongezea mtaji Benki Kuu, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa kitaasisi.
Mhe. Balozi Omar alibainisha vipaumbele vitatu muhimu vinavyoongoza jitihada za nchi, ikiwemo kuimarisha uratibu na utayari, ambapo Serikali inaoanisha mtiririko wa fedha na mipango ya kukopa na tathmini ya ukwasi ya Benki Kuu ili kuhakikisha kunakuwa na outekelezaji mzuri wa bajeti na sera za fedha.
“Pili ni ulinzi wa kaya zilizo hatarini wakati wa majanga ambapo Tanzania inasisitiza kuwa misaada yoyote wakati wa mitikisiko ya kiuchumi inapaswa kuwa ya walengwa mahususi, ya muda mfupi, na yenye ufadhili wa kuaminika, hasa ikizingatiwa athari za bei za mafuta duniani” alisema Mhe. Balozi Omar
Alilitaja jambo la tatu kuwa ni ulinzi wa uwekezaji unaochochea ukuaji na ustahimilivu wa uchumi ikihusisha kuwekeza katika mtaji wa rasilimali watu na matumizi muhimu ya kijamii, huku ikizingatia mkakati wa mapato ya kati ili kupanua wigo wa kifedha na kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje.Tanzania imetoa wito kwa Shirika la Fedha la Kimataifa pamoja na taasisi nyingine za fedha, kuendelea kutoa msaada wa kiufundi na fursa za nchi wanachama kujifunza kutoka kwa wenzao ili kuimarisha utabiri wa fedha, usimamizi wa madeni na uchambuzi wa sera.
Tags
Balozi Khamis Mussa Omary
Bangkok
Benki ya Dunia (WB)
Habari
IMF
Kimataifa
Mikutano ya IMF
Mikutano ya WB


