Tume ya Jaji Lila: Wananchi wa kata 14 Ubungo njooni kutoa ushahidi Oktoba 12-16, 2026

NA DIRAMAKINI

TUME ya Rais ya Kuchunguza Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imewataka wananchi wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, kujitokeza kutoa ushahidi na taarifa zitakazosaidia kubaini waliohusika katika matukio hayo.

Wilaya ya Ubungo ina jumla ya kata 14 ambazo ni Goba, Kibamba, Kimara, Kwembe, Mabibo, Makuburi, Makurumla, Manzese, Mbezi, Mburahati, Msigani, Saranga, Sinza, na Ubungo.

Tume hiyo inayoongozwa na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, itapokea ushahidi wa wananchi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kuanzia Oktoba 12 hadi 16, 2026.
Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Shaban Ally Lila akizungumza jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo, Jaji Lila amesema, tume hiyo inalenga kupata taarifa zitakazosaidia kubaini watu waliohusika katika kusababisha ghasia, vurugu na uvunjifu wa sheria.

Sambamba na kupata maelezo kutoka kwa wananchi waliopata madhara kutokana na matumizi ya nguvu wakati wa kudhibiti matukio hayo.

Amesema, tume hiyo tayari imefanya shughuli zake katika wilaya za Kigamboni, Ilala na Temeke na sasa imehamishia shughuli hizo Ubungo ili kuwapa wakazi wa eneo hilo fursa ya kueleza wanachokifahamu kuhusu matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.

Jaji Lila amewahimiza wananchi wenye taarifa muhimu kujitokeza mbele ya tume hiyo bila kusita, akiwahakikishia kuwa usalama wao utazingatiwa na taarifa watakazowasilisha zitashughulikiwa kwa usiri mkubwa.

Amesema, ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kusaidia tume kupata maelezo yatakayowezesha kuchunguza matukio hayo na kubaini wahusika kwa kuzingatia taarifa zitakazokusanywa.

WANANCHI WANAWEZA KUTOA TAARIFA KWA NJIA YA SIMU

Kwa mujibu wa Jaji Lila, wananchi ambao hawataweza kufika katika ofisi za tume wanaweza kuwasilisha taarifa zao kupitia namba ya simu 0737305449 au barua pepe barua@tumeuchunguzi.go.tz.

Aidha, amefafanua kuwa, kuhitimishwa kwa shughuli za tume katika wilaya za Kigamboni, Temeke na Ilala hakumaanishi kuwa wananchi ambao hawakupata fursa ya kutoa ushahidi katika maeneo hayo wamepoteza haki ya kufanya hivyo.

Amesema, wananchi hao wanakaribishwa kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo na kuwasilisha ushahidi au maelezo yao kwa ajili ya kusaidia uchunguzi unaoendelea.

Jaji Lila amesisitiza kuwa, tume inaendelea kuwapa wananchi fursa ya kushiriki katika mchakato huo kwa kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kubainisha ukweli kuhusu matukio ya ghasia na ukiukwaji wa sheria yaliyohusishwa na kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here